Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia,Arusha
Tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini zimethibitisha kuwa sekta ya habari kwa kipindi kirefu imekuwa ikiongozwa na wanaume zaidi na pia maudhui ya vyombo hivyo bado hayajazingatia vya kutosha sauti za wasio na sauti ambao ni wanawake na makundi mengine ya pembezino.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi wa vyombo vya habari kwa waandishi wanawake waandamizi yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji Imani Daud Aboud amesema iwapo wanawake wakiwa kwenye vyombo vya maamuzi watashiriki kuchukua hatua za kuleta maendeleo kwani watazungumzia kwa uzoefu, msisitizo na hisia changamoto zinazowakabili.
Jaji Imani amesema haki zinazohamasishwa katika vyombo vya habari pia zimeelezwa bayana katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mkataba huo unatumika na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu hivyo taasisi ya habari ina mchango mkubwa katika kuhamasisha haki za binadamu pamoja na kuendeleza kazi ya Mahakama hiyo.
“Tukiwa na vyombo vya habari makini, vyenye weledi na vinavyozingatia maslahi ya Jamii na nchi kwa ujumla, vitaweza kutimiza dhima yake na kuleta mchango mkubwa kijamii, kisiasa na kiuchumi, hivyo nitoe pongezi kwa Baraza la Habari Tanzania kwa kuandaa mafunzo mafunzo haya ambayo pia maadili ya wanahabari ni moja ya masuala muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele” Alisema Jaji Imani.
Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga amesema mafunzo hayo yanatokana na utafiti uliofanywa na Baraza hilo mwaka 2019 uliojulikana kama Breaking the Glass Ceiling ambao umethibitisha kuwa bado Kuna upungufu hususani katika nafasi za uongozi na pia maudhui yanayozingatia usawa wa kijinsia katika vyombo vya habari, hivyo mafunzo haya yatakuwa ni dira ya kupata viongozi mahiri wanawake watakaochangia kuleta mabadiliko katika sekta ya habari.
Amesema licha ya mafunzo hayo kulenga kuwainua wanawake lakini bado vyombo vya habari vina wajibu wa kuandika jinsia zote kwa usawa kwani kwa kuandika jinsia moja pekee haitaweza kuleta mabadiliko kwenye Jamii.
“Mafunzo haya ni ya awamu ya sita tangu tumeanza kutekeleza mradi wa miaka mitano kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanawake ulioanza mwaka 2019 na utamalizika mwaka 2025 na hadi sasa tumeshatoa elimu hii kwa wanawake 128 nchini” alisema Mukajanga.
Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake ikiwemo Itifaki ya Maputo (2003), Azimio la Beijing (Being Platform of Action) pamoja na Mkataba wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC 2008) inayosisitiza ushiriki sawa wa wanawake kufikia asilimia 50/50 kwenye nyanja ya maamuzi, serikalini na taasisi binafsi.