Gazeti la uchunguzi la JAMHURI limetwaa tuzo mbili za uandishi bora wa habari (Excellence in Journalism Awards Tanzania – EJAT) kwa mwaka 2018, tuzo zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Hatua hiyo ni sehemu tu ya mafanikio ya gazeti hilo ambalo mwaka jana liliongoza dhidi ya vyombo vingine vyote vya habari Tanzania Bara na Zanzibar vilivyohusishwa kwenye utafiti wa ubora wa maudhui kwa vyombo vya habari nchini kwa mwaka huo wa 2018.

Utafiti huo ulifanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Spurk Media Consulting Ltd ya Uswisi.

Lakini kama hiyo haitoshi, mwishoni mwa wiki, Gazeti la JAMHURI limekuwa gazeti pekee la kila wiki lililoibuka kidedea kwa kutwaa tuzo ya haki za binadamu na utawala bora; pili, kipengele cha mafuta, gesi na madini.

Katika vipengele vyote hivyo, JAMHURI limeibuka kidedea si tu dhidi ya magazeti yote yanayotoka mara moja kwa wiki nchini, bali hata mengine yote yanayotoka kila siku.

Ushindi huo mnono kwa JAMHURI ulitokana na kazi za kihabari za Naibu Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Manyerere Jackton, ambaye pia aliingia katika kundi la washindani wa kumpata mwandishi bora wa jumla kwa mwaka 2018. Mbali na Manyerere, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile alishinda nafasi ya pili katika kipengele cha masuala ya kodi.

Shughuli ya makabidhiano hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu na usimamizi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), sambamba na wadau wake wengine wa masuala ya ubora wa habari.

Habari mojawapo iliyoandikwa na Manyerere Jackton ilihusu wizi wa fedha za serikali unaodaiwa kufanywa na mkurugenzi, habari hii ilishinda katika kipengele cha haki za binadamu na utawala bora, lakini habari nyingine iliyoshinda katika kipengele cha mafuta, gesi na madini ilihusu wizi wa madini ya vito aina ya tanzanite.

Akizungumzia ushindi huo wa Gazeti la JAMHURI, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile, amesema ni hatua nzuri kwa Gazeti la JAMHURI ambalo ubora wake wa maudhui ya habari umewahi kuthibitishwa na taasisi ya utafiti ya Spurk Media Consulting Ltd ya Uswisi na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

“Tunachoweza kuahidi ni kuendeleza ubora wetu kama ambavyo imedhihirika kwa mujibu wa utafiti. Jambo la kujivunia ni kwamba timu ya uhariri imekuwa na watendaji wenye uzoefu wa kutosha katika masuala ya habari za uchunguzi na tasnia ya habari kwa ujumla wake,” amesema Balile ambaye licha ya nafasi hiyo ya Mhariri Mtendaji ni mmoja wa wakurugenzi wamiliki wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited inayomiliki Gazeti la JAMHURI.

Wakurugenzi wengine wamiliki ni pamoja na Mkinga Mkinga na Manyerere Jackton. Mkinga Mkinga pia amewahi kuwa mshindi wa jumla wa tuzo za umahiri katika uandishi wa habari mwaka 2014.

Kwa upande wake, Manyerere, ambaye pia amewahi kushinda tuzo ya umahiri wa uandishi wa habari mwaka 2014 katika kipengele cha uhifadhi, mazingira na utalii, alizungumzia ushindi huo wa mwishoni mwa wiki akisema, kiini cha ushindi huo ni nguvu ya pamoja na utendaji miongoni mwa wafanyakazi wote wa Gazeti la Jamhuri.

“Nimefurahia mno ushindi huu, lakini nyuma ya furaha yangu ni nguvu ya pamoja ya watumishi wote wa Gazeti la JAMHURI. Juhudi zao za pamoja, kila mmoja kwa nafasi yake, ndizo zimefanikisha ushindi huu. Naamini nguvu hiyo itadumu, na kwa kweli sina shaka na wafanyakazi wenzangu wa JAMHURI,” amesema Manyerere.

Lakini Mhariri Mkuu wa Gazeti la JAMHURI, Mkinga Mkinga, amezungumzia ushindi huo akisema ni jambo alilolitarajia kwa kuwa gazeti hilo limekuwa likifanya kazi zake wakati wote kwa kuzingatia weledi wa viwango vya juu katika kufanya habari za uchunguzi.

“Nilitarajia ushindi mkubwa zaidi. Sijui nini kimetokea, lakini si haba. Utakumbuka Gazeti la JAMHURI ndilo lililotangazwa kuwa chombo cha habari bora zaidi kwa mwaka 2018, mwaka ambao ndizo tuzo hizi zimeshindanishwa. Na waliofanya utafiti Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Spurk Media Consulting Ltd ya Uswisi ndio hao waliolitambua JAMHURI kuwa ndiyo chombo bora zaidi cha habari. Kwa hiyo tumeupokea ushindi huu kwa mikono miwili na kama alivyosema Mhariri Mtendaji, tutaendeleza juhudi zaidi ili kubaki katika kilele cha mafanikio,” amesema Mkinga.

Naye Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Jamhuri, Joan Mrema, amesema anajivunia juhudi zinazofanywa katika kazi na watumishi wa kampuni hiyo, akisisitiza juhudi hizo ziendelee.

“Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa JAMHURI nawapongeza washindi wetu, Manyerere Jackton na Deodatus Balile aliyetutoa kimasomaso kwenye kipengele cha umahiri wa habari za masuala ya kodi kwa kushika nafasi ya pili. Ushindi huu ni hamasa kubwa sana kwetu wafanyakazi,” amesema Joan.

Mbali na washindi hao wa JAMHURI, wengine walioshinda tuzo hizo katika maeneo mengine ni pamoja na Salome Kitomari wa Gazeti la Nipashe na Yohani Gangway kutoka Radio Sauti.

Washindi zaidi katika vipengele vingine ni Betty Tesha wa Shirika la Utangazaji (TBC Taifa) ambaye habari yake imehusu namna gani ajali za barabarani zinachangia umaskini katika familia. Orodha zaidi ya washindi inawahusisha Salma Mrisho wa Star TV, Dafrosa Ngairo wa Azam TV, Dotto Bulendo wa DW, Adam Lutta wa Gazeti la Habari Leo na Geoffrey  Ismaely wa Gazeti la Majira.

Wengine ni Husna Mohamed kutoka chombo cha habari cha Zanzibar Leo, Janeth Joseph wa Gazeti la Mwananchi na mpiga picha bora za habari akiwa Octavian Gwalakwila kutoka Azam TV.

Orodha zaidi inawahusisha pia Rahel Palangyo kutoka Habari Leo, aliyeshinda kipengele cha michezo na utamaduni, Paul Kagenzi kutoka redio inayoitwa Sauti ya Tabora na Mariam Mziwanda wa Gazeti la Uhuru.

Juma Kapipi wa Azam Two kutokea Tabora naye alikuwa miongoni mwa washindi katika kipengele kimojawapo kati ya vipengele takriban 20 vilivyoshindaniwa.

By Jamhuri