Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Clement Mswanyama, amewadanganya walimu na Watanzania kwa ujumla juu ya umiliki wa mali za walimu, JAMHURI linathibitisha.

Hivi karibuni, Mswanyama ameitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma na bila aibu akawaambia uongo kuwa Chama cha Walimu Tanzania kinamiliki hisa 99 za Kampuni ya Teachers Development Company Limited (TDCL), huku Katibu Mkuu wa CWT akimiliki asilimia 1, kumbe si kweli.

Katika mkutano huo alioufanya Dodoma kwa mbwembwe kukanusha habari zilizochapishwa na Gazeti la Uchunguzi la JAMHURI, Mswanyama amesema: “Wenzetu waliotuandika taarifa ambazo si za kweli, za kujali, za kupotosha makusudi, tumewapa fursa, waombe radhi kupitia gazeti lao, hilo tena front page, baada ya hapo tutakwenda mbele ya sheria kama watakataa kufanya hivyo, kwa sababu ni upotoshaji wa makusudi, na wanawatumia watu, ambao walikuwa viongozi wa chama cha walimu wakashindwa uongozi, wametumia kila mbinu za kutafuta kuingia kwenye uongozi wameshindwa na mambo ya demokrasia kwa sababu huo ni uchaguzi.

“Sasa uchaguzi unapokushinda ukashindwa kukamilisha malengo yako, basi ukubali matokeo. Lakini ndiyo wanaanza kutembea na karatasi kupotosha ukweli. Hao sasa wanaoandika hizo taarifa ndiyo watakwenda kuthibitisha kutoa taarifa hizo mahahakamani, kwani Chama cha Walimu kiko vizuri, na ningetumia fursa hii kuwambia walimu wenzetu nchi nzima kuwa na amani, mali ziko salama na chama kiko salama.

“Na wawapuuze, wanaojitahidi kupotosha, ukweli wa Chama cha Walimu. Chama cha Walimu ni miongoni mwa vyama 20 vikubwa vilivyo hapa nchini, vyama vya wafanyakazi, lakini ndiyo chama na ni miongoni mwa chama kinachofanya vizuri, katika usimamizi na utunzaji wa fedha zake, kwani vitu vinaonekana. Tumejenga majengo mikoa yote Tanzania, na yanaonekana, tumejenga majengo kila mkoa, tuna jengo na maghorofa mawili, matatu kila mkoa. Kila wilaya kuna majengo na kuna viwanja, na kuna magari kila wilaya, magari mapya, kila mkoa. Mali zote rasilimali zote za chama kuna mgawanyo, kuanzia makao makuu mpaka chini kwenye tawi, lakini kuna watu wanatuchonganisha…”

Mswanyama amejitokeza kusema uongo huu baada ya awali Gazeti hili makini la uchunguzi JAMHURI kuwa limechapisha habari za kiuchunguzi zinazoonyesha kuwa kuna “upigaji” mkubwa ndani ya CWT kiasi cha kuzalisha mgogoro kati ya uongozi na wanachama wao.

Habari zilizochapishwa na JAMHURI zimeonyesha kuwa uchunguzi uliofanywa na vyombo viwili huru; ambavyo ni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati Maalumu ya Kuchunguza Kampuni ya Maendeleo ya Mwalimu (TDCL) iliyoanzishwa Aprili 7, 2003 umebainisha kuwa TDCL si mali ya walimu.

Kwa mujibu wa Katiba ya TDCL (MEMART) ina mtaji wa Sh milioni 10, zilizogawanywa kwenye hisa moja moja yenye thamani ya Sh 100,000 kila moja. Hata hivyo, kampuni imebainika kuwa ilisajiliwa na watu wawili kama mali yao, ambao ni Justinian Rwehumbiza mwenye hisa 50 na Juma Abdallah (1). Baadaye katika kufoji nyaraka, wanahisa waliongezeka, ila si CWT au walimu bali ni viongozi.

“Kibaya zaidi Chama cha Walimu kilijenga jengo kwa gharama ya shilingi 5,943,000,000.00 na kutolikabidhi kwa TDCL [kisheria],” inasema sehemu ya taarifa ya kamati iliyokuwa na wajumbe Hamisi Lissu (Mwenyekiti), Nuru B. E. Shenkalwa (Katibu), Amina Kisenge (Mjumbe), Abubakar Allawi (Mjumbe) na Moses Mnyazi (Mjumbe aliyejitoa).

Uchunguzi unaonyesha kuwa pamoja na TDCL kutokuwa mali ya walimu ingawa ilianzishwa mahususi kuendesha miradi ya walimu, bado kampuni hii iliingia mkataba na Kampuni ya GIMCO Africa inayoendesha jengo la Kitegauchumi cha Mwalimu kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam.

JAMHURI lilipoanza kuchapisha taarifa hizi, wiki mbili zilizopita Mswanyama alizungumza na JAMHURI, akasema: “Haya mambo hayana ukweli, yametungwa. Mali za walimu ziko salama kabisa. Kuhusu TDCL tulianzisha kwa kutumia wakurugenzi wa muda, vikao rasmi vilipendekeza majina. MEMAT (katiba ya kampuni) inasema kampuni inaendeshwa na wanahisa. Bodi ya wadhamini inamiliki hisa 99 kwa niaba ya wanachama wote. Katibu Mkuu anamiliki hisa asilimia moja.”

Mwenyekiti huyo aliendelea kulieleza JAMHURI: “Waliotumika mwanzo wamekwishajiondoa, akiwamo Margaret Sitta, Juma Abdallah, Yahaya Msulwa. Hata Justinian Rwehumbiza amekwishajiondoa, na anasema kuna watu wanamshawishi asijiondoe kwa kuwa kampuni iliyofunguliwa ni yake na mwenzake, kwa hiyo lazima kwanza alipwe shilingi bilioni moja. Tunajua kuna mwenzetu ndiye anayechochea haya mambo,” amesema Mswanyama bila kumtaja huyo mwenzao anayedhani anachochea mtafaruku huo wa usalama wa mali za wanachama wa CWT.

Uongo wa Mswanyama

JAMHURI linafahamu na linathibitisha kuwa Mswanyama ni mwongo, katika hili anadanganya walimu na umma. Uchunguzi uliofanywa katika ofisi za Msajili wa Kampuni (Brela), unaonyesha kuwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita (Jumapili) hakuna mabadiliko ya umiliki wa TDCL. Kampuni hii bado inamilikiwa na watu binafsi na si walimu. Kilichotokea CWT walipeleka maombi ya “kurekebisha” hali baada ya walimu kupiga kelele wakitaka kurejeshewa umiliki wa mali zao, ila wamegonga mwamba.

Uchunguzi unaonyesha barua ya Brela yenye Kumb. Na. MIT/RC/45719/13 ya Aprili 30, 2018 inayojibu hoja za wadau waliokuwa wanatafuta usahihi wa kampuni hii, inathibitisha kuwa Kampuni ya TDCL imesajiliwa Aprili 7, 2003 kwa mtaji wa Sh milioni 10, uliogawanyika kwenye hisa za Sh 100,000 kila moja.

 Inaonyesha kuwa hadi wakati huo haikuwa na Katibu wa Kampuni. Wanahisa wa kampuni hii hadi muda huo walikuwa ni Justinian Rwehumbiza mwenye hisa 50, Juma Abdallah (1), Margaret Sitta (10) na Yahaya Bakari Msulwa (10). Hadi hapo hakuna cha umiliki wa walimu au CWT. Wakurugenzi wa kampuni hiyo ni Felician Tarimo na Justinian Rwehumbiza. Barua hiyo imesainiwa na Leticia Zavu kwa niaba ya Msajili wa Kampuni.

CWT walitaka kufanya mabadiliko. Ikumbukwe katika mkutano mkuu wa mwaka 2016, walimu walidanganywa kuwa wanaimiliki TDCL kwa asilimia 99 kupitia wadhamini na asilimia 1 kupitia kwa Katibu Mkuu. Uongo huu Mswanyama anaendelea kuusambaza hadi leo.

Desemba 14, mwaka 2017 Rais John Magufuli aliwaambia CWT katika mkutano mkuu wao pale Dodoma kuwa kampuni zao ikiwamo Benki ya Mwalimu zina matatizo makubwa yanayopaswa kurekebishwa. Kwa Mswanyama kujaribu kuonyesha kuwa CWT ni mali ya walimu wakati si kweli, anajenga mazingira ya kuonyesha Rais Magufuli hakusema kweli mbele ya walimu, suala ambalo halikubaliki.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Novemba 12, 2018 barua ya Brela kwenda kwa Katibu Mkuu wa CWT yenye Kumb. Na. MITM/RC/45719/17, inasema: “Rejea barua yako yenye Kumb. Na. AB.225/320/01A/69 ya Oktoba 11, 2018… Kampuni tajwa hapo juu imesajiliwa na taarifa zake ni kama ifuatavyo:-

“Wakurugenzi ni Felician Tarimo na Justinian Rwehumbiza. Na wanahisa ni Justinian Rwehumbiza (50), Juma Abdallah (1), Margaret Sitta (10) na Yahaya Bakari Msulwa (10).

“Napenda kukujulisha kwamba katika orodha ya makampuni yaliyoorodheshwa kwenye barua yako ya Oktoba 11, 2018, Kampuni iliyosajiliwa na ofisi ya Msajili wa Makampuni ni; Teachers Development Co Limited kwa namba 45719.

“Mnamo tarehe 5 Mei, 2011, kampuni iliwasilisha makubaliano ya kikao kilichotoa maamuzi ya kuwanyang’anya hisa, wanahisa Margaret Sitta (10), Juma Abdallah (1), Yahaya Bakari Msulwa (10). Maamuzi hayo yaliwasilishwa, lakini hayakusajiliwa kutokana na mapungufu ya kisheria.

“Kampuni vilevile tarehe 5, Mei 2011 ilijaza fomu ya kuwapatia hisa wanahisa wapya waliotajwa kwa majina ya Secretarial (Secretary) General aliyepewa hisa (1) na Registered Trustee of Chama cha Walimu Tanzania (20), lakini mabadiliko hayo hayajasajiliwa kutokana na mapungufu ya kisheria.

“Mnamo tarehe 15, Aprili 2014 Kampuni iliwasilisha fomu ya kugawa hisa kwa Registered Trustees of Chama cha Walimu Tanzania (9), lakini fomu hiyo haijasajiliwa kutokana na mapungufu ya kisheria.

“Angalizo, kuhusu ombi la Baraza la Wadhamini la msaada wa kisheria wa kuondoa mgogoro wa wamiliki wa hisa, tunapenda kukushauri kufikisha mgogoro huo mahakamani kwa sababu ndiyo chombo rasmi kinachoweza kutatua mgogoro huo kisheria.” Barua imesainiwa na Leticia Zavu kwa niaba ya Msajili wa Kampuni. Wanahisa wawili wa TDCL kati ya wanne wamekwishafariki dunia.

JAMHURI linathibitisha pasi na shaka kuwa hadi wiki iliyopita kwa uchunguzi lilioufanya kwenye ofisi za Brela, hakuna kilichobadilika. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif, JAMHURI linafahamu kuwa tayari ameanza kazi ya kurekebisha tatizo hilo, kwani amekutana na baadhi ya waliokuwa wamiliki wa hiyo kampuni na kukubaliana nao wajiondoe katika umiliki wa TDCL na kurejesha hisa hizo kwa CWT.

 Mtu wa mwisho kutia saini makubaliano ya kurejesha hisa hizo ni mzee Rwehumbiza, ambaye ametia saini makubaliano mbele ya mwanasheria wa CWT na Seif atawaandikia Brela kuomba marekebisho hayo yafanyike kwa masilahi mapana ya mali za walimu.

Alipohojiwa na JAMHURI kuhusiana na hili, amesema: “Ni kweli wala hili halina kificho. Nimewaandikia Brela kurekebisha tatizo hili lililokuwapo kwa nia ya kurejesha mali za CWT mikononi mwa chama, na naamini marekebisho yatafanyika.”

Utata wa jina la kampuni

Kuhusu utata katika jina halisi la kampuni inayomilikiwa na CWT kati ya Teachers Development (T) Limited, Teachers Development Company Limited (TDCL) na Teachers Development Co. Ltd, Mswanyama ameliambia JAMHURI wiki iliyopita kuwa kampuni halisi ya chama hicho ni Teachers Development Company Limited (TDCL), na akafafanua kuwa kilichosababisha hali hiyo ni ukosefu wa umakini kwa watu ambao walikuwa wakiandika majina ya kampuni hiyo.

“Unajua sisi ni wataalamu katika masuala ya elimu, haya yalikuwa makosa ya kiuandishi. Kuna waliokuwa wakiandika (T) Limited, wengine wanaweka Co. Ltd, lakini uhakika ni kwamba kampuni ya Chama cha Walimu ni TDCL,” anaeleza Mswanyama.

Ameeleza kuwa makosa hayo yalikwisha kurekebishwa na majina yote kufutwa na kwamba majina hayo yalikuwa yakiwapa utata hata watumishi wa Brela. Hata hivyo, ukifanya “official search” bado katika mtandao wa Brela kampuni hii inasomeka Teachers Development Corporation Limited, ingawa kwenye majalada ukifanya upekuzi, inasomeka Teachers Development Company Limited.

Mswanyama bado anaendelea kusema uongo kwa kuwahakikishia walimu kuwa wanamiliki TDCL kwa kusema: “TDCL inawezaje kuwa mali ya mtu binafsi wakati ni kampuni pekee inayoendesha jengo la Mwalimu? Hii ni kampuni tanzu kama zilivyo kampuni nyingine na iliundwa makusudi ili kuendesha jengo hilo. Sisi katiba haituruhusu kujihusisha na biashara, ili kuweza kuliendesha jengo la Mwalimu ilibidi tufungue hiyo Kampuni ya TDCL kama tanzu ambayo kazi zake zote zinaratibiwa chini ya uangalizi wetu,” anaeleza.

Pia amejibu hoja ya kufungua benki kwa Sh bilioni 15 wakati kwa sheria za kibenki mtaji unaotakiwa ni Sh bilioni 4, amesema mtaji ulikuwa mkubwa kwa sababu benki walitaka iwe ya umma.

“Kuanzisha benki lazima uongozwe na Benki Kuu. Sisi tulitaka iwe ni benki ya umma, hivyo hata mtaji wake ulibadilika kinyume cha mtaji wa benki binafsi. Walimu wanamiliki hisa 51 na pointi kadhaa, na mashirika mengine nayo yanamiliki hisa 48 na mapointi kadhaa, kwa hiyo hili suala ni la uelewa, watu wanatakiwa kuelimishwa juu ya hilo,” anasema Mswanyama.

Kuhusu baadhi ya viwanja na majengo ya chama hicho hati zake kutoonekana amesema, hati zipo na kwamba zimetunzwa kwa Kabidhi Wasihi Mkuu.

“Penye wengi kuna mengi, kuna watu wazembe, na wengine hawako makini, lakini nikwambie mali zote zimesajiliwa na hati hizo zipo. Hata hilo jengo la Mbeya unalosema hati yake ipo, tungewezaje kujenga kwenye uwanja bila kuwa na hati?” amehoji Mswanyama.

Katibu Bodi ‘aliyesimamishwa’

Kutokana na hali hiyo, aliyekuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini CWT ambaye amekuwa akipigwa vita na wenzake kadhaa, miongoni mwao wakiwamo kwenye kamati ya utendaji taifa ya CWT, Hellen Mbezi, amelieleza JAMHURI kuwa chama hicho kinaharibiwa na baadhi ya viongozi wake wa kitaifa.

Amesema ili chama hicho cha walimu kiweze kuwanufaisha walimu wote, viongozi wa chama hicho wakiwamo Rais, Makamu wake na Mweka Hazina wa chama wanatakiwa kujiuzulu, lakini pia wadhamini washitakiwe kila mmoja awajibike kisheria kuhusu namna alivyohusika kulinda ama kufuja mali za walimu.

Anadai kuwa miongoni mwa viongozi hao wamehusika moja kwa moja kuhujumu mali za CWT zikiwemo Sh milioni 203 za viwanja 29 vya CWT mkoani Morogoro.

Mali nyingine alizodai zimekuwa kwenye hatari ni majengo ya CWT kukosa hati, likiwemo jengo la walimu lililoko mkoani Mbeya, lakini pia baadhi ya viongozi ‘kujibinafsishia’ Kampuni ya CWT kinyume cha sheria.

Viongozi hao wanatajwa kujimilikisha Kampuni ya Teachers Development Company Limited (TDCL), mali ya chama, huku taarifa za usajili wa Brela zikionyesha kampuni hiyo imesajiliwa kama kampuni binafsi.

Madai mengine kutoka kwa Hellen Mbezi aliyepata kuwa Katibu wa Bodi ya Wadhaini ni pamoja na Benki ya Mwalimu kudaiwa kufunguliwa kwa mtaji wa Sh bilioni 15 wakati sheria ya kusajili benki kwa mujibu wa sheria za kibenki ni Sh bilioni 4.

Wakati Hellen akisema hayo, kwa upande wake Mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Wadhamini wa CWT, Clement Mswanyama, amedai kuwa Hellen Mbezi ndiye pekee anayeona tatizo kwenye chama hicho chenye wanachama zaidi ya 100,000.

“Hizo tuhuma kwamba Kampuni ya TDCL inamilikiwa na watu binafsi hazipo. Kinachoonekana katika maandishi yale ni majina ya waanzilishi, yaani ‘promoters’, lilikuwamo hadi jina la Margaret Sitta,” anaeleza Mswanyama na kuongeza kwamba kwa sasa yamefanyika “maboresho” yanaoonyesha kampuni hiyo inamilikiwa na CWT kwa asilimia 100.

“Hisa za Kampuni ya TDCL zinamilikiwa kwa asilimia 99 na wadhamini kwa niaba ya wanachama wote. Asilimia moja inayobaki inamilikiwa na Katibu Mkuu kwa niaba ya CWT,” anaeleza Mswanyama. Huu ni uongo.

Hellen Mbezi anasema uongozi wa juu wa CWT umekuwa ukilenga kuwahujumu baadhi ya watendaji wanaohoji kuhusu uadilifu ndani ya chama hicho.

“Mwaka 2011 nikiwa nimehudhuria baraza langu la kwanza la chama nilibaini hujuma ya kimadaraka katika chama. Niliona karatasi ambayo inapendekeza wakurugenzi wa Benki ya Mwalimu, Teachers Development Company Limited (TDCL), wajumbe waliokuwa wamependekezwa katika karatasi hiyo walikuwa ni Naibu Katibu Mkuu, alikuwa mzee Tido Lweyichi na Makamu wa Rais wa CWT kwa kipindi hicho aliyeitwa Mary Chitanda.

“Baada ya kuona karatasi hiyo sikutaka kuongelea nje ya kikao hicho, nilinyoosha mkono nikaomba kuzungumza. Nilihoji kwamba huo ni uteuzi wa kamati ya utendaji? Lakini wenye mali hawatambui. Nikahoji kama chama kinaruhusiwa kufanya biashara ilhali maudhui ya chama hicho si kujihusisha na biashara bali ni kuwekeza kwenye maeneo ya elimu pekee. Chama hakiruhusiwi kufanya biashara, lakini nilihoji kitendo hicho cha kuteua wakurugenzi katika kampuni hiyo hakijafuata sheria,” anasema Mbezi.

Anaeleza kuwa viongozi hao walileta hoja hiyo wakijua kwamba walimu ni watu wa kawaida ambao hawawezi kutambua kwa umahiri masuala ya mienendo ya biashara.

Hellen anadai baada ya kuhoji masuala hayo, baadhi ya viongozi wa CWT na wadhamini wenzake kutoka Bodi ya Wadhamini ya chama hicho walianza kumchukia, wakatengeneza mipango ya kumng’oa kwenye uongozi.

“Huyo Mwenyekiti wangu (Mswanyama) nikizungumzia hili suala atakuwa analijua vizuri, kwamba tangu mwaka 2011 walikuwa kwenye mikakati ya kuwaondoa wadhamini kwenye chama, na walianza kwa kuomba ushauri wa kisheria.

“Sababu ya kuwaondoa ni baada ya kuhoji nafasi ya wadhamini na mali za chama hasa Kampuni ya TDCL na mchakato wa Benki ya Mwalimu,” amesema Hellen na kuongeza: “Chama chetu kina wanasheria, wanasheria hao ndio waliokwenda kuomba ‘legal opinion’ (ushauri wa kisheria) kwa kampuni moja ya kisheria.

“Walikwenda kuomba mwongozo wa kisheria kwamba Chama cha Walimu ni ‘Board Cooperate’ lakini pia kina wadhamni ambao nao ni ‘Board Cooperate’, lengo lao walijua walimu si wapekuzi. Hivyo walijua katika mabaraza yao wadhamini wataondolewa moja kwa moja,” anasema Hellen Mbezi.

Kwa mujibu wa maelezo yake ya ziada, Hellen Mbezi, anasema mwaka 2012 katika kikao kilichofanyikia Morogoro alishinikiza kuhusu mali za CWT, lakini ikaibuka hoja ya kuwaondoa wadhamini kwa sababu sheria iko kimya juu yao.

“Wadhamini wenzangu kwa kipindi hicho walikuwa ‘hawajaharibiwa’ kwa ushawishi wowote mbaya. Walikuwepo wadhamini wenzangu kama Faustine Salalala na Fortunata Kadega. Wote katika kikao kile tulikubaliana kulipinga hilo na baadhi ya wajumbe wenye hekima wakatuunga mkono na hoja hiyo ikabaki kuwa kimya,” anasema.

Anafafanua kuwa baadaye alimwandikia barua mwanasheria wa serikali akiomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu wadhamni kutotakiwa katika chama hicho.

“Mimi na wenzangu tulimwandikia barua Msajili wa Vyama vya Kijamii kueleza malalamiko yetu, hali iliyomfanya msajili huyo kuwaita ofisini kwake wadhamini na uongozi wa CWT na kuhoji kama sheria imekuwa kimya kuhusu wadhamini ndiyo sababu ya kuwaondoa?” anasema.

Anaendelea kueleza: “Katika maazimio aliyoandika Msajili wa Vyama nakumba katika aya ya pili aliandika uwepo wa wadhamini, kwamba waachwe wafanye kazi zao na wasiingiliwe na kwamba sheria hiyo haikatazi wadhamini, na akawaongoza kwenda kwa mwanasheria wa serikali ili atoe ushauri zaidi.

“Mimi nimewahi kushiriki kwenye vikao vya kibenki katika Benki ya CRDB, kule nilijifunza namna ya kuiendesha benki, kwa hiyo nilipoona mchakato unavyoendeshwa katika chama chetu nilihoji nikitaka kujua hatima ya Benki ya Mwalimu na namna walimu watakavyofaidika na benki hiyo kwa sababu nilikuwa sioni ‘MEMAT’ za mali nyingi za CWT zikiwemo MEMAT ya benki wala MEMAT ya jengo la Mwalimu,” anasema Mbezi kwa wakati huo akiwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini.

Anaeleza kuwa ili kunusuru mali za chama ilibidi kuwashitaki  mahakamani Katibu Mkuu na Rais wa chama hicho, kwa sababu wao ndio wanaoongoza chama na kwamba hoja zake zilikuwa nane na zote zilikubaliwa.

“Moja ya hoja zangu ilikuwa ni kampuni kuendeshwa na wanachama, MEMAT za chama kutoonekana pamoja na MEMAT hizo kugawiwa kwa wanachama na zuio la kutoondoa wadhamini,” anasema Mbezi.

Anaeleza kuwa, hoja zake nyingi viongozi wa CWT walizikubali huku akieleza kuwa wadhamini walikubali kutoondolewa ila watabaki kama vielelezo tu, na hawatakuwa na mahala pa kuwasilisha hoja zao hata wakisafiri kwenda popote kuangalia mali za chama hawatakuwa na mahala pa kuweka hadidu za rejea zao.

Kwa mujibu wa Hellen Mbezi, baada ya kuona hali hiyo, aliomba Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA) waingilie kati suala hilo, na kwamba walifanya vikao viwili na mwanasheria wa RITA ambaye aligusia kuhusu sheria ya wadhamini kukaa kimya wakati katiba inawatambua wadhamini hao.

“Kwa kipindi chote hicho tunachohangaika tulikuwa tunahangaika na sheria isiyotambua wadhamini katika chama chetu cha walimu, na hilo ndilo tatizo la vyama vya wafanyakazi nchini,” anaeleza Mbezi.

Anasema pamoja na Benki Kuu kuelekeza Benki ya Mwalimu kufanyiwa marekebisho kwa kuboreshwa mifumo ya kiuongozi ya benki hiyo, uongozi wa CWT haujafanya mabadiliko katika benki hiyo.

“Wakati michakato ya kuhuisha hisa nilikuwa siwaelewi kwa sababu nilikuwa nimeshatengwa, sikuwa nashiriki, lakini kimsingi baada ya mchakato huo muundo wa benki ungebadilika, lakini hali haikuwa hivyo, kama kuna mabadiliko basi tungeshuhudia wanachama nao wangekuwa na ukurugenzi katika kampuni hiyo.

“Hapa ambacho kingeangaliwa ni kundi la wanachama wenye hisa nyingi ni wangapi na kundi la wanachama wenye hisa kidogo wako wangapi, na je, wanapatikanaje? Pamoja na misuguano hiyo, bado benki hii haijabadilika ili ifanane na umiliki wa walimu, wakurugenzi mpaka leo bado naona ni walewale hali ambayo inaongeza utata,” amesema.

Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) imesambaratika katika usimamizi wa mali za chama hicho. Bodi hiyo ya wadhamini ndiyo yenye jukumu kwa mujibu wa Katiba ya CWT kusimamia mali za chama hicho ambacho walimu nchini hukatwa asilimia mbili kwenye mishahara yao, kwa hiyo kwa mwezi chama hicho hukusanya takriban Sh bilioni 3.6. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Clement Mswanyama, hapikiki chungu kimoja na Katibu wa Bodi, Hellen Mbezi na katika mvutano huo juhudi zimefanyika kuhakikisha Mbezi anawekwa kando kwenye orodha ya wadhamini kutokana na misimamo yake ya kuhakikisha mali za chama hicho zinabaki katika ulinzi imara wa Bodi ya Wadhamini.

Mbali na mivutano ya viongozi hao, kumekuwa na tuhuma kuwa mali za chama hicho haziko salama. Brela kupitia mawasiliano yake kwenda CWT, kwa barua Kumb. Na. MIT/RC/45719/06 ya Januari 18, 2018 Kampuni ya TDCL haikuwa imewasilisha hesabu zake (annual returns) Brela kwa mujibu wa sheria katika miaka sita tofauti, yaani hesabu za mwaka 2011, 2012, 2014, 2015, 2016 na 2017 za kampuni hiyo ambayo hadi wakati huo, wanahisa wake walikuwa watu binafsi ambao ni Justinian Rwehumbiza (akiwa anamiliki hisa 50), Juma Abdallah (hisa moja), Margaret Sitta (hisa 10) na Yahaya Msulwa (hisa 10). Hapa wanahisa wameongezeka Mama Sitta na Msulwa.

Utata zaidi kuhusu usalama wa mali hizo ulithibitishwa tena na aliyewahi kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa CWT, Simon Keha, ambaye kwa mujibu wa uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI, Machi 28, 2018 aliandika barua kwenda Brela yenye kichwa cha habari: “Maombi ya nyaraka za umiliki wa makampuni yaliyo chini ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT)”, inaonyesha kuwapo kwa kasoro katika utunzaji wa nyaraka za chama hicho kwenye ofisi za watendaji na Baraza la Wadhamini.

Barua hiyo inaeleza: “Naomba kuwasilisha ombi la kupewa nyaraka za umiliki wa makampuni yanayomilikiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Makampuni hayo ni; Teachers Development Company Limited (TDCL) na Mwalimu Commercial Bank (MCB PLC).

“Lengo la kuomba nyaraka hizo ni kwa ajili ya kutaka kutekeleza yatokanayo na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyowasilishwa Jumanne tarehe 27, Machi, 2018.”

Gazeti hili limekuwa likiandika habari za uchunguzi kuhusu CWT kwa muda sasa na miongoni mwa yaliyowahi kuripotiwa na gazeti hili ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za chama hicho. Pia walimu wanataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kufanya marekebisho ya Katiba ya CWT kama ilivyoelekezwa na Mkutano Mkuu mwaka 2017 kuwa mwaka 2019 uitishwe mkutano mkuu wa CWT.

By Jamhuri