JAMHURI mmemtendea haki Dilunga

Sehemu ya wafanyakazi wa Kampuni ya JAMHURI Media Limited wakiomboleza wakati wa ibada ya kumuaga Godfrey Dilunga.

Safari ya mwisho hapa duniani ya aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la JAMHURI, Godfrey Dilunga, imehitimishwa wiki iliyopita baada ya mwili wake kuhifadhiwa katika makaburi ya Bigwa, mkoani Morogoro.

Dilunga alifariki dunia alfajiri ya Septemba 17, 2019, baada ya kusumbuliwa kwa maradhi ya tumbo. Kifo cha mhariri huyo kimeacha simanzi kubwa miongoni mwa wanahabari wenzake, wadau wa habari, viongozi wa serikali na familia yake kwa ujumla.

Dilunga alilazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Septemba 9, 2019 akitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa rufaa kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo. Madaktari na wauguzi wamejitahidi kadiri ya uwezo wao kumtibu Dilunga, ila Mungu mwingi wa rehema, ambaye alimtoa ameamua kumtwaa kutoka dunia hii.

Licha ya kusoma maandiko yake kupitia magazeti ambayo amewahi kufanyia kazi na katika maandiko kwenye mitandao ya kijamii, Dilunga alikuwa mwanachama mwenzangu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), hivyo ninatambua uwezo wake mkubwa wa kuiona habari kubwa na kuichambua kwa kina, kwa kuipa vionjo vyote vinavyohitajika katika habari.

Kimsingi, Dilunga alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya habari, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba ameondoka duniani mapema ilhali bado mchango wake unahitajika zaidi kuielimisha, kuiasa, kuikosoa na kuiburudisha jamii kupitia kalamu yake.

Familia ya wanahabari, wadau wa habari, wanasiasa na watu wengine mbalimbali wamehuzunishwa kwa kuondokewa mpendwa wao Dilunga. Umati mkubwa uliofurika katika kumuaga viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam siku ya Alhamisi iliyopita na Ijumaa nyumbani kwao pale Bigwa, Morogoro ni ushahidi tosha kwamba mwanahabari huyu alikuwa mwema kwao.

Kundi kubwa la wanahabari, majirani zake na wanasiasa akiwamo Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, walisafiri kwenda Morogoro kumzika Dilunga. Hakika huu ni upendo ambao unapaswa kuendelea kuonyeshwa kwa familia yake ili kumuenzi.

Kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji wa JAMHURI Media Limited, Deodatus Balile, alivyosema kuwa kwa muda mfupi aliofanya kazi Gazeti la JAMHURI, Dilunga amekuwa msaada na ametoa mchango mkubwa katika kuboresha maudhui ya gazeti hili la uchunguzi.

Hakika Dilunga ameacha pengo kubwa. Hata hivyo, jambo la msingi ni kuuenzi mchango wake kwenye taaluma ya habari aliyoipenda sana. Wanataaluma tuliobaki ni vema kufanya kazi kwa bidii ili kuitendea haki jamii ya Tanzania kama ambavyo aliasa Padri Godfrey Maghali, ambaye aliongoza misa ya mazishi Bigwa.

Hata hivyo, mbali na kuhuzunika kwa kuondokewa mpedwa wetu Dilunga, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Kampuni ya JAMHURI Media Limited kupitia kwa uongozi wake katika kumhudumia Dilunga, wakati akiugua na baada ya mauti kumkuta, kwa kuhakikisha inashughulikia msiba mpaka kuuhifadhi mwili wa mfanyakazi wake huyo katika kaburi lake.

Licha ya kuwa ni takwa la kisheria kwa mwajiri kuwakatia bima ya afya watumishi wake, bado kuna kampuni nyingi za binafsi hazina utaratibu wa kuwakatia bima ya afya au bima ya majanga wafanyakazi wao.

Lakini kwa upande wake, JAMHURI Media Limited imewakatia bima ya afya na bima ya majanga wafanyakazi wake, kuanzia viongozi wa juu mpaka wa chini. Hili ni jambo la kupongezwa na kuigwa.

Kimsingi bima ya afya inapunguza gharama za matibabu. Hivyo, ni vema sasa kampuni nyingine zikaiga mfano wa JAMHURI Media Limited kwa kuwakatia bima ya afya wafanyakazi wenu. Hii itasaidia kuwapunguzia gharama za matibabu na kampuni haitaingia mfukoni kuchota kiasi kikubwa cha fedha kushughulikia matibabu ya mfanyakazi wake.

Nchini kuna kampuni nyingi za binafsi zinaendeshwa kibabaishaji, licha ya kuwalipa mishahara kiduchu, pia hazitaki kuwakatia bima ya afya wafanyakazi wao, pindi inapotokea mtumishi wake akaugua, inakuwa kimbembe, uongozi unamtelekeza mgonjwa kwa kutomsaidia fedha za matibabu na inapotokea akafariki dunia, kampuni inajiweka kando, haijihusishi na msiba wa mfanyakazi wake.

Kimsingi jambo hili la ovyo linaumiza sana familia za wafanyakazi ambao hupatwa na magonjwa ama kufariki dunia bila kupata msaada wa ofisi ambako mhusika alikuwa akifanya kazi. Hivyo, chonde chonde kampuni ambazo hazina utaratibu wa kuwajali watumishi, viongozi wake wawe na utu kwa kuwatendea haki wafanyakazi wao kama ambavyo JAMHURI Media Limited imemtendea vema Dilunga.

Natambua zipo baadhi ya kampuni ambazo zina utaratibu mzuri kama wa JAMHURI, lakini bado zipo nyingi zenye matatizo. Viongozi wake hawana ubinadamu hata kidogo, wanachojali wao ni kufanyiwa kazi kwa ujira mdogo.

Licha ya Dilunga kufanya kazi kwa kipindi cha takriban miezi sita, waajiri wake walimkatia bima ya afya na bima ya majanga. Hivyo, alipata tiba kwa kutumia bima yake ya afya, jambo ambalo naamini litakuwa limesaidia kupunguza gharama za matibabu.

Aidha, uongozi wa kampuni chini ya Balile, Manyerere Jackton na Mkinga Mkinga umeona kuna umuhimu wa kumuenzi Dilunga kwa vitendo zaidi kwa kuahidi hadharani kampuni itamsomesha mtoto wa kwanza wa Dilunga mpaka ngazi ya chuo kikuu ambacho gharama zake zinahimilika. Kimsingi huu ni mchango mkubwa katika kumuenzi aliyekuwa mfanyakazi wake.

Mbali na kuahidi kumsomesha mtoto huyo, kampuni hiyo imekusudia kufungua akaunti ili fedha za michango zilizopatikana ziwe kianzio cha kusaidia kuwasomesha watoto wengine wawili wa Dilunga chini ya usimamizi wa familia. Hakika huu ni mchango mkubwa kwa familia ya Dilunga.

Hakika, JAMHURI Media Limited mmemtendea vema na ubinadamu aliyekuwa mtumishi wenu Dilunga, ambaye amewahi kufanya kazi pia katika Gazeti la Mtanzania na Raia Mwema, gazeti ambalo amelitumikia kwa miaka mingi.

Mwandishi wa makala hii ni mdau wa tasnia ya habari anapatikana kupitia namba 0712 727244