Ndugu Rais, tunasoma katika Biblia Takatifu kuwa wanafunzi wake Bwana Yesu walimwambia, “Mwalimu utufundishe kusali kama Yohani Mbatizaji alivyowafundisha wafuasi wake”. Yesu akawajibu akawaambia, “Mnaposali salini hivi; Baba yetu uliye Mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike, utakalolifanyike duniani kama Mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi lakini utuopoe na yule mwovu’’. Imepita zaidi ya miaka elfu mbili, lakini sala imebaki ileile!

Tangu kuasisiwa kwa nchi yetu tumejaliwa kuwa na marais watano. Watatu kati yao ni walimu. Enzi zetu tuliumiza vichwa kutaka kujua ipi taaluma iliyobora zaidi. Ilijulikana kuwa taaluma zote ni muhimu, lakini kati ya udaktari na ualimu ni ipi iliyo bora zaidi? Ikakubalika kuwa kwa sababu daktari hawezi kuwa daktari mpaka kwanza afundishwe na mwalimu, basi ni kuku ndiye alianza kwa sababu yai lisingeweza kujitotoa lenyewe. Mwalimu ni muhimu.

Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitukuza sana taaluma yake ya ualimu. Alienda nayo sambamba na urais wake siku zote za uongozi wake. Aliutumia muda wake mrefu wa urais wake akifundisha ndani na nje ya nchi yetu. Hakutuachia muda wa kukaa bila kuwa na jambo la kutafakari. Wanasema kichwa cha mvivu wa kufiri ndiyo karakana ya shetani.

Rais Ali Hassan Mwinyi naye alifundisha wakati wa urais wake ingawa ni vigumu kutaja ni somo gani. Wengine wanasema bila Nyerere kumkataza Mwinyi polisi wake wasiwapige wapinzani mabomu, eti leo Agustino Mrema angekuwa kipofu. Leo tunaye Rais wetu ambaye kwa kuwa ni mwalimu, tunamwomba atufundishe kutafakari.

Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianza na somo la ‘Uhuru na Umoja’. Lilipoeleweka akaja na somo la ‘Uhuru na Kazi’. Baadaye akaja na ‘Uhuru na Maendeleo’. Julius Kambarage Nyerere akiwa mwalimu na akiwa Rais hakuwahi kusikika akilalamika popote hata kilipokuja kipindi kigumu pale ndege ya Air Tanzania ilipotekwa.

Watekaji walidai Rais Julius Kambarage Nyerere ajiuzulu. Nyerere hakulalamika kwa wananchi, eti aonewe huruma. Alijua kuwa Watanzania hawawezi wote kuwa na akili sawa. Vimbulu hawakosekani. Badala ya kulalamika kwa wananchi kuwa kuna watu wanatuonea wivu, alisimama imara kama jemadari akasema, kama mbwai na iwe mbwai, hapa hajiuzulu mtu. Ndege ilikuwa katika uwanja wa ndege kule London. Wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hatukusikia kelele za mavuvuzela kuandamana kwenda kudai ndege kwenye ubalozi wa Uingereza hapa nchini. Hakika Nyerere hakuruhusu uvuvuzela wa aina hiyo.

Hatimaye ndege ilirudishwa ikiwa salama na abiria wote ambao wengi wao walikuwa ni Watanzania kwa sababu ndege ilitekwa ikiwa katika safari zake za ndani. Kurejea kwa ndege hakukuzua shamrashamra zozote ingawaje haijaeleweka mpaka leo ilikuwaje rubani Deo, mateka (aliyetekwa) alituzwa kama shujaa. Waswahili walikuwa hawana nguo za kubadilisha wakashonewa kaunda suti wote. Nyerere hakuwa mtu wa kufanyiwa mzaha!

Watanzania wote wenye uelewa walikuwa wanajua kuwa ndege ile ni yao iliyotokana na kodi zao kwa mgao wa Bunge mbele ya wawakilishi wao. Hii iliyozuiwa sasa ununuzi wake umewatatiza wananchi. Hakuna mahali wanapopajua panapoonyesha kuwa wawakilishi wao kama Bunge waliidhinisha fedha zitumike kuinunua. Elewa kuwa ndani ya nyumba fedha inayotumika kununua shati la baba siyo ya familia. Bunge yaani familia halikai kugawa fedha kwa ajili ya kununua shati la baba. Fedha iliyotumika kununulia ndege ilitokana na kikao gani cha Bunge? Hawa waliofurahia hawaelewi, tusiwalaumu. Waliona ndege imenunuliwa kama shati la baba. Lakini walimsikia CAG anasema katika ukaguzi wake fedha nyingi kiasi cha Sh trilioni 1.5 hakuona zilipotumika. Je, ndiyo hizo zilizonunua shati la baba?

Kama kati yao ni baadhi ya wazazi wa watoto 342 waliorundikwa chini katika chumba kimoja Shule ya Msingi Msowelo iliyopo mkoani Morogoro katika wilaya ya Kilosa, kama kuna kiongozi aliwashangaa hawa kufurahia ndege kuzuiwa alishangaza sana. Nina hakika Mwalimu Elizabeti Mbilinyi anayewafundisha watoto hao, hakuwa tofauti.

Mama Anita Chavike na mama wenzake wa Kijiji cha Pangamlima, Kata ya Makole wilayani Muheza mkoani Tanga wanaodai kujifungua watoto njiani usiku kutokana na umbali wa kufuata huduma ya afya, habari za ndege kuzuiwa zingewasikitishaje?

Wazazi wa watoto wa madarasa tofauti wanaosomea katika chumba kimoja huku wakiwa wamegeuziana migongo na kufundishwa na walimu tofauti kwa wakati mmoja timamu anapaswa kushangaa akiwaona hawafurahii.

Kwa mifano hii michache ndiyo inayotufanya tuliheshimu sana wazo la Katibu Mkuu wetu wa Chama Cha Mapinduzi, baba Bashiru Ally kuwa viongozi waende kwa wananchi. Wakawaeleze mpaka waelewe nini maana ya miradi hii mikubwa ikiwamo na hizi ndege, zina faida gani kwao? Kwa sababu hawaelewi maana yake, wanapodhani kuwa miradi hii ndiyo sababu ya maisha yao kuwa magumu hawakosei. Wanaokosea ni viongozi wao ambao badala ya kuwaelimisha mpaka waelewe, wao wanabaki wanawashangaa!

Wanawema tunapoongea tuweke makini kwa kuwa tunasikiwa na wananchi wengi. Siyo busara kudhani kuwa ujumbe tuutumao unawafikia wale tu tusiowapenda au tunaowadhania hawatupendi. Tukituma ujumbe usiompendeza Mungu unawafikia hata waumini wenye hofu ya uwepo wake. Jumla ya wanachama wa chama chako cha siasa, ukichanganya na jumla ya wanachama wote wa vyama vingine vya siasa, idadi yao haifiki hata nusu ya Watanzania. Hivyo kiongozi bora ni yule asiyeabudu chama chake cha siasa hadharani.

Timamu wenye vyama na wasio na vyama wanaelewa kuwa nchi yao Tanzania ni moja. Nao ni wana wa familia moja. Kinachowaunganisha ni upendo wa kweli kati yao. Sawa tuwapelekee maji huko hata ya kutosha kuwa kabahari kadogo, lakini kama pasipo upendo wa Mungu Baba, tujue tunafanya ubatili mtupu.

Mtume Petro alisema, “Hata nikitoa mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo mimi si kitu’’. Inapotokea mwanajamii mwenzetu kaumizwa vibaya na watu wabaya kwa kukatwakatwa na mapanga, anapougulia hospitalini hayuko nyumbani kwake, usiwaambie watu wema kuwa kaitelekeza familia yake. Watu wa Mungu watatutoa sisi katika vifua vyao! Tumejibomoa huku tukimkusanyia huruma nyingi mgonjwa kutoka kwa wananchi.

197 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!