Home Makala kumkumbuka Mwalimu Nyerere

kumkumbuka Mwalimu Nyerere

by Jamhuri

Oktoba 14, 2019 itatimia miaka 20 tangu Mwalimu Julius Nyerere alipofariki dunia. Tangu afariki imekuwa desturi kwamba, kunapokaribia kumbukizi ya kifo chake, tunashuhudia ongezeko la matukio yaliyojaa kumbukumbu za maisha yake.

Vyombo vya habari hurudia hotuba na nukuu zake au huchapisha makala za ziada na kuandaa vipindi maalumu kumzungumzia yeye na maisha yake ya utumishi kwa umma. Siku ikipita tunarudia kwenye gurudumu la maisha na kusubiri maadhimisho yajayo.

Tunamtaja sana Mwalimu Nyerere kwa sababu yeye ni sehemu muhimu ya historia ya nchi hii. Ni suala la historia tu, si chaguo la mtu yoyote.

Lakini tunamtaja pia kwa sababu baadhi yetu tunaamini alikuwa mwalimu wa kweli; aliyeongoza taifa akijenga misingi imara ya umoja na mshikamano wa kitaifa, aliyepinga ubaguzi wa aina zote, na aliyejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhimiza uongozi wenye uadilifu na unaoheshimu utu na haki za binadamu.

Wengine watakumbuka mengine, lakini itoshe kusema kuwa tunayo mengi kama taifa ambayo tunaweza kujifunza kutokana na uongozi na maisha yake. Kama bado tunaendelea kumnukuu ni kielelezo cha kukubali kuwa anaendelea kuwa mwalimu.

Hata kwa wale wasiomkubali Mwalimu Nyerere kama kiongozi anayeweza kutufundisha lolote, umuhimu wake kihistoria unabaki pale pale. Hao wanaweza wakafafanua ni masuala gani ambayo hatupaswi kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere, au ya kuyaepuka ndani ya uongozi.

Kwa mabaya au mazuri, suala lolote ambalo linatupa fundisho kwenye historia na ambalo tunataka liwe la manufaa kwa kizazi chetu na kijacho litatufaa tu iwapo tutazingatia moja ya nguzo za msingi kabisa za elimu. Tunajifunza kitu vyema kwa kuliondoa lile somo darasani na kulifanya sehemu ya maisha yetu.

Ni rahisi sana ikifika Oktoba 14 kumnukuu Mwalimu Nyerere akirudia ahadi za mwanachama wa TANU akisema ‘rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa.’

Inawezekana baadhi yetu tukikabiliwa na polisi anayedai rushwa kwa kosa dogo la usalama barabarani tukagoma kutoa hiyo rushwa na kukubali malipo makubwa zaidi ya faini.

Lakini ni suala gumu zaidi kwamba tudaiwe rushwa na daktari ambaye huduma yake, baada ya kumpa rushwa, itaokoa maisha ya jamaa yetu, lakini badala ya kutoa rushwa tung’ang’anie kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa msimamo wake wa kupinga na kupiga vita rushwa.

Lakini yule atakayekuwa na ujasiri wa kufanya hivyo atakuwa na msimamo ambao umekuwa sehemu ya maisha yake, msimamo ambao hautamkwi tu kwenye maadhimisho, lakini unashikiliwa kwa mwaka mzima, mwaka hadi mwaka.

Ni sawa kabisa kusema kuwa Mwalimu Nyerere au rais mwingine yeyote ambaye yuko madarakani hawezi kudaiwa rushwa ambayo anadaiwa raia asiye na cheo chochote. Lakini kukubali ukweli huu ni kukubali unyonge. Itakuwa sawa na kusema kuwa kwa sababu jemedari hayuko mstari wa mbele na hakabiliani na risasi kama ambavyo anakabiliana nayo askari wa kawaida, basi mapambano hayapaswi kuendelezwa, au hayana msingi wowote.

Kwenye mapambano dhidi ya maovu kila mtu ana nafasi yake, hata kama baadhi wanakabiliana kwa karibu zaidi na adui.

Lakini siyo kweli kuwa viongozi hawakabiliani na mazingira ambayo yanafanana na kudaiwa rushwa. Katika miaka ya 1960 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipokubali kufunguliwa kwa ubalozi mdogo wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki, serikali ya iliyokuwa Ujerumani Magharibi ilitishia kusitisha misaada kwa serikali ya Tanzania iwapo ofisi ile ndogo ya ubalozi isingefungwa.

Serikali ya Tanzania iligoma kuifunga ile ofisi ikisisitiza uhuru wa kujiamulia masuala yake na kukataa kuwekewa masharti ya kupokea misaada. Baada ya kuweka msimamo huo uhusiano wa kidiplomasia uliendelezwa baina ya Tanzania na nchi zote hizo mbili.

Nimetumia mfano mdogo tu wa rushwa kujenga hoja juu ya umuhimu wa kuenzi suala la msingi mwaka mzima badala ya kwa siku moja tu. Lakini ya kuenzi yapo mengi. Aidha, hoja hii haimhusu Mwalimu Nyerere peke yake, bali mtu yeyote – kiongozi au asiye kiongozi – ambaye tunaamini anaweza kuturithisha misingi imara inayolinda haki na usawa ndani ya jamii.

Elimu haikomi baada ya kupata matokeo ya mtihani. Matokeo ya mtihani ni mwanzo tu wa kutumia ile elimu kukabiliana na jitihada za kuboresha maisha yetu kwa kutumia elimu tuliyonayo.

Ni kwa msingi huo huo naleta hoja kuwa maadhimisho yanapaswa kuvuka hatua ile tuliyozoea halafu kusubiri mwaka mzima ili tukumbushane tena masuala ambayo yana manufaa kwetu.

Jinsi gani jamii inaamua kufanya maadhimisho, si suala la sayansi. Ni suala la desturi. Linaweza kubadilika kutegemea na desturi za wakati uliopo.

Ni Rais John Magufuli ambaye amebadilisha kidogo desturi za kuadhimisha sikukuu na akaamua kuwa badala ya kwenda Uwanja wa Taifa na kushuhudia gwaride rasmi, basi tutumie baadhi ya sikukuu kufanya usafi.

Haihitaji tamko la rais kubadilisha mitazamo yetu, si la Rais Nyerere wala la marais wote waliomfuata. Tunahitaji tu kupima yale yenye manufaa na kuyatumia kama mwongozo wa kubadilisha maisha yetu na kuimarisha jamii.

Maoni: barua.muhunda@gmail.com

You may also like