Jamii ihimize utu, ipinge unyama

Makala hii inatudai kufasili maneno utu na unyama ambayo ni sehemu ya anuani. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili – TUKI (sasa, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili – TATAKI), mwaka 1981, utu ni hali ya kuwa na tabia zinazolingana na hadhi ya mtu. Kisawe cha neno utu ni ubinadamu. Na unyama ni matendo yasiyo ya kiutu (kiubinadamu), ukatili, udhalimu, uonevu na ujahili.

Uislamu umeupa utu nafasi ya kwanza na muhimu kabisa kwani mwenye utu ndiye awezaye kushika vema mafunzo ya dini na kuyatekeleza ipasavyo. Hata Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), kabla ya kupewa utume, alisifika kwa utu na jamii yake ikakiri kuwa yeye ni mkweli na mwaminifu.

Ukweli na uaminifu ni tabia zinazolingana na hadhi ya mtu ambaye Mwenyezi Mungu amemtukuza kwa kumpa akili na kumletea muongozo ili atofautiane na wale anaofanana nao kibailojia lakini hawana akili; wanyama.

Tunamuona Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anapotanguliza yanayohusiana na utu kabla ya kutaja msingi wa dini katika mazungumzo yake na mgeni aliyekwenda Makkah kumtafuta baada ya kupata habari ya utume wake. Mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Mgeni: Nani wewe? Mtume Muhammad: Mjumbe (Mtume) wa Mwenyeezi Mungu.

Mgeni: Nani aliyekutuma?

Mtume Muhammad: Allaah Mtukufu.

Mgeni: Kwa nini amekutuma?

Mtume Muhammad: Amenituma ili niuunge udugu, niwaokoe watu kutokana na umwagaji damu, nihakikishe usalama wa njia (barabara) na uvunjaji wa masanamu na kuabudiwa Mwenyezi Mungu Mmoja bila ya kumshirikisha na chochote.

Msingi wa kupewa kwake utume ni Itikadi ya Kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Itikadi ya Mungu Mmoja apaswaye kuabudiwa kwa haki – Tawhiid) kama tunavyosoma kwenye Qur’aan Tukufu Sura ya 18 (Surat Al-Kahf) aya ya 110 kuwa: “Sema: Mimi ni mwanadamu kama nyinyi. Nimeletewa Wahyi (ufunuo) kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja”.

Pamoja na ukweli huu, tunamuona Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipokuwa akimuelezea mgeni wake sababu ya yeye kupewa utume akitanguliza mambo matatu yanayohusiana na utu (ubinadamu) kabla ya kulieleza lile ambalo ndio msingi wa kupewa kwake utume. Mambo matatu Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) aliyotanguliza kuyataja ni:

(1) Kuunga udugu – Mafungamano ya kifamilia (Amani ya Jamii).

(2) Kuwaokoa watu kutokana na umwagaji wa damu – Thamani ya uhai wa mwanadamu (usalama wa uhai).

(3) Usalama wa njia – Usalama barabarani (usalama wa watu na mali zao).

Baada ya kuyataja mambo haya matatu ambayo ni mahitaji ya lazima kwa binadamu popote walipo, ndipo alipoutaja msingi mkuu wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu; kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, hana mshirika.

Mambo matatu haya ndiyo yanayompa mwanaadamu uhuru wa kuchagua wa uhakika, vinginevyo mwanadamu aweza kufanya jambo pasi na hiari bali kulazimishwa na mazingira yaliyopo walhali Uislamu umeweka wazi kuwa uchaguzi wa dini ni jambo la hiyari na si kulazimisha kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat al-Baqarah) aya ya 256 kuwa:

“Hapana kulazimisha katika dini.” Maelezo yaliyotangulia yanaonyesha wazi umuhimu wa wanajamii kuhimizana tabia zinazolingana na hadhi ya mtu.

Kwa maneno mengine, wanajamii kuhimizana mema na kukatazana mabaya. Jamii kusimama kidete kupinga tabia ambazo zinadhalilisha utu wa mwanadamu na kumuondolea utukufu wake wa kutofautishwa na wanyama anaofanana nao kibailojia.

Miongoni mwa tabia zinazodhihirisha unyama na hazistahili kufanywa na kiumbe aitwaye mwanadamu ni hizi zifuatazo:

Kuwaibia majeruhi badala ya kuwasaidia: Tabia nyingine inayodhalilisha utu wa mwanadamu na kudhihirisha unyama ni pale panapotokea ajali na watu wakashughulishwa na kujinufaisha kwa kuwaibia maiti na majeruhi badala ya kuwasaidia.

Unyama huu unadhihirisha dhuluma na ukatili wa hali ya juu. Ni dhuluma kwa kuwaibia marehemu na majeruhi na ukatili

wa hali ya juu kumuacha majeruhi anayehitaji msaada wa haraka, wakati mwingine majeruhi anayevuja damu, na badala ya kumsaidia ukashughulika na kuiba mali zao.

Kuvua nguo hadharani: Jamii yetu nchini Tanzania imefikia sasa kuzoea tabia ya wanawake wanaoamua kuvua nguo hadharani wakati wakicheza ngoma kwenye sherehe mbalimbali. Haya yanafanyika hadharani na mbele ya watoto wadogo wanaokomazwa na watu wenye rika la bibi zao, mama zao na dada zao.

Tabia hii maarufu kama “kumwaga radhi” inadhalilisha utu wa mwanadamu na ni unyama na dhuluma inayopanda mbegu mbaya kwa jamii na kuharibu tabia za watoto walio wepesi kuiga.

Ukifuatilia utabaini kuwa jamii imeufanya uovu huu ni jambo la kawaida kiasi cha watu wa rika mbalimbali kuvutiwa na unyama huu na kuwa sehemu ya watazamaji na washangiliaji.

Baya zaidi ni kuwa vitendo hivi vibaya vinasajiliwa kupitia vyombo vya kielektroniki na kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

Jambo la kushangaza ni kwa nini mamlaka husika hazichukui hatua kwa tabia hizi zinazodhalilisha utu wa mwanadamu wakati ushahidi umejaa kwenye mitandao? Wako wapi maofisa utamaduni waliokuwa wanatoa vibali vya shughuli kama hizi kwa msisitizo wa kufuata maadili?

Au tumemezwa na utandawazi na uhuru usio na mipaka kiasi sasa mwanamama kuvua nguo hadharani ni jambo la kawaida na jamii imelikubali?

Ni dhahiri kuendelea kwa unyama huu na jamii kukaa kimya bali wakapatikana watu wanaosambaza unyama huu kwenye

mitandao ya kijamii bila ya kujali yule atakayefikiwa na kuonyeshwa unyama huu.

Hebu fikiria kuwa mtoto wa mwanamama anayemwaga radhi atakuwa na hali gani atakapomuona mama yake ndiye anayemwaga radhi na picha zake kusambaa mitandaoni?

Vipi itakuwa hali ya mtoto mbele ya wenzake watakaofikiwa na vituko hivyo, iwe nyumbani au shuleni?

Hawa wanawake wanaofanya haya wametafakari athari mbaya ya kile wanachokifanya?

Hivyo taasisi zinazotetea haki za wanawake na hadhi yao hazioni kuwa matendo haya yanawadhalilisha wanawake hawa kabla ya kudhalilishwa na wengine?

Tunaamini mama ni shule muhimu katika makuzi ya mtoto tangu kuzaliwa kwake hadi kubalehe. Kama mama anayetarajiwa kuwa mwalimu mwenye kazi muhimu ya kumuandaa huyu mtoto kuwa mwanajamii bora ndiye huyo anayevua nguo hadharani huku akijidanganya kuwa hakuna anayemjua katika eneo hilo, walhali baadaye unyama huo utasambazwa mitandaoni, vipi ataaminiwa katika malezi mema ya watoto?

Hatuoni kuwa matendo haya na mengine yafanywayo kupitia ngoma hizi zinachangia kuharibu tabia za baadhi ya wasichana na kusababisha matendo machafu ya uzinzi na mimba kabla ya ndoa?

Jamii haina budi kuzinduka na kutekeleza wajibu wake wa kuamrisha mema na kukataza mabaya. Jamii ihimize tabia zinazolingana na hadhi ya mtu na ipinge tabia zinazodhalilisha utu wa mwanadamu. Jamii iweke “vidhibiti tabia” ili kutoruhusu mwanadamu katika kuyaridhisha matamanio yake afanye mabaya ambayo hata wanyama hawayafanyi.

Mmoja wa walimu wangu alipata kuniambia kuwa: “Mwenyeezi Mungu amewaumba malaika, akawapa akili bila ya matamanio, akawaumba wanyama akawapa matamanio bila ya akili, na akawaumba wanadamu akawapa vyote; akili na matamanio….Hivyo matamanio ya mwanadamu yakiishinda akili yake mwanadamu huyo atafanana na mnyama. Yaani, atakosa utu na ubinadamu na atafanya wanayoyafanya wanyama wasio na akili.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Uislamu, mwanadamu wa aina hiyo atakuwa katika hali mbaya zaidi kuliko wanyama kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 7 (Surat Al- ‘Aaraaf) aya ya 179 kuwa: “Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama howa (wanyama wanaofugwa), bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika”. Shime jamii ihimize utu na ipinge unyama.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa

Tanzania (Bakwata).