Unakuta umefungua shauri la ndoa, inaweza kuwa maombi ya talaka, mgawanyo wa mali, malezi ya watoto au vyote. Wakati huo ambapo kesi haijaanza, au imeanza lakini haijaisha, unahisi au umeona mali za ndoa ambazo pengine zinatakiwa kugawanywa zikiwa katika hatari ya kuuzwa, kugawiwa, kuharibiwa au kubadilishwa umiliki.

Unaona kabisa shauri likija kwisha patakuwa hamna kitu au kitakuwepo kidogo. Unapaswa kufanya nini kisheria katika mazingira kama haya ili kuokoa mali hizi ili usije kukosa haki yako kesi ikiisha? Hiki ndicho kitakachozungumzwa leo.

Kitu unachotakiwa kufanya  kimeelezwa katika Kifungu cha 138(1) cha Sheria ya Ndoa. Kifungu hiki kinasema pale ambapo mtu ataona kuna hatari ya mali kuuzwa, kuharibiwa  au kupotezwa kwa namna yoyote ile basi atakuwa na haki ya kuomba mahakama itoe zuio la muda kumzuia mtu yeyote kuuza, kubadili umiliki, kuharibu, kutoa zawadi au kufanya kitu kingine chochote kitakachoathiri mali hizo.

Kitu hiki pia kimeelezwa mara nyingi na Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Rufaa katika kesi mbalimbali, mojawapo ikiwa ni hii ya ELIZABETH GIKENE dhidi ya JOHN ZAKHARIA GIKENE, shauri la ndoa namba 5/2004.

Kwa hiyo unachoweza kukifanya ni kwanza, kama shauri liko Mahakama ya Wilaya, Mahakaya ya Hakimu Mkazi, au Mahakama Kuu na una wakili anayekuwakilisha, basi mwambie kuhusu wasiwasi wako wa dalili za kupotezwa kwa mali lakini pia muombe mfanye utaratibu wa kuweka zuio. Bila shaka mtakubaliana kuhusu hilo.

Pili, kama shauri liko katika mahakama nilizotaja hapo juu lakini hauna wakili anayekuwakilisha basi ni muhimu kumtafuta wakili yeyote umweleze wasiwasi wako na umuombe akuandalie maombi ya zuio hili ili uzuie mali wakati shauri la msingi likisubiriwa kwisha. Mtaelewana kuhusu hili na mtafanya kama mlivyoelewana.

Ni muhimu ukampata wakili wa kukuandikia maombi haya hata kama utayawasilisha mahakamani wewe mwenyewe, kwa sababu ni shida kwa mtu ambaye hana utaalamu kuandaa maombi haya.

Kama kesi iko Mahakama ya Mwanzo hapa hauna haja ya wakili wala kuandaliwa maombi rasmi bali utamueleza hakimu anayesikiliza shauri lako kwa mdomo kuhusu  wasiwasi wako wa mali kuharibiwa na utamuomba atoe zuio la muda mali zisiguswe mpaka shauri la msingi litakapomalizika.

Itasaidia zaidi iwapo utaweza kunukuu kifungu cha sheria nilichokitaja hapa juu pamoja na hiyo kesi mahususi niliyoweka ambavyo kwa pamoja vinaruhusu maombi haya ya zuio. Kama utashindwa basi mwambie tu bila kumtajia kifungu, atatoa msaada.

Mara nyingi tatizo hili la kuharibiwa mali wakati shauri likiendelea limekuwa likiwakumba zaidi kina mama. Anapofungua shauri kuomba talaka au mgawanyo wa mali,  basi mwanaume huanza kuuza baadhi ya mali au kuzibadilisha umiliki ili wakati shauri linakwisha mali ziwe zimekwisha ili mwanamke asiambulie kitu, au kwa lengo kuwa ikifikia ushahidi kila mali itakayotajwa na mwanamke kuwa ni ya ndoa akatae kuwa si yake au ilishauzwa.

Hata wanaume nao hukumbwa na tatizo hili, lakini zaidi ni wanawake. Basi hili lisikupe taabu tena kwa kuwa dawa yake ndiyo hii. Na kwa taarifa mali ikizuiwa na mahakama isiuzwe na mtu akaendelea na uuzaji au kuiharibu, basi adhabu yake ni kifungo miezi sita jela kwa kuidharau mahakama, lakini pia yule aliyenunua anakuwa amepoteza hela yake kwa kuwa amenunua mali ambayo imezuiwa na mahakama na hivyo biashara hiyo itakuwa batili.  Basi tuchukue hatua.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri