Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza.
Taasisi ya Wanahabari ya usaidizi wa jamii za pembezoni(MAIPAC) kwa kushirikiana na Mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu(THRDC) , imezindua mafunzo kwa wanahabari wa mazingira wa Kanda ya Ziwa ili kuwajengea uwezo kuandika vyema habari hizo lakini pia wakitambua sheria mbalimbali za mazingira.
Mafunzo hayo yanayoshirikisha wanahabari 35 ni mfululizo wa mafunzo ambayo.yanaendelea kutolewa na taasisi hizo, kwa ufadhili wa shirika la Umoja wa mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO)awali waandishi wa kanda ya kaskazini walipatiwa mafunzo hayo.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Miradi wa THRDC Wakili Halima Sonda aliwataka wanahabari kuandika habari za kiuchunguzi kuhusiana na masuala ya mazingira ili kusaidia jamii.
Sonda jamii zimekuwa zikiathirika na uharibifu wa mazingira na wanahabari wanawajibu wa kusaidia jamii kukabiliana na athari za mazingira.
Mkurugenzi wa taasisi ya MAIPAC,Mussa Juma Siwayombe akitoa mafunzo kuhusu uandishi wa habari za mazingira,aliwataka wanahabari kujua vyanzo vya uharibifu wa mazingira na jinsi ya kuvizuia.
Alisema habari za mazingira zimejikita katika mambo kadhaa ikiwepo mabadiliko ya tabia nchi,uchafuzi wa mazingira,Ukame,uhifadhi na wanyamapori,Kilimo na mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari(JOWUTA) alisema kupitia mafunzo hayo, wanataka wanahabari kuandika habari za kina za kichunguzi ili kusaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira,kushawishi maboresho ya sheria na sera na kuokoa jamii ambazo zinaendelea kuathirika.
“MAIPAC na THRDC tutasaidia ili mtimize wajibu wenu na tunataka matokeo chanya katika mafunzo haya”alisema
Wakili Paul Kisabo akitia mada kuhusiana na sheria ambazo zinasimamia masuala ya mazingira aliwataka wanahabari kuzijua sheria hizo ili kufanya kazi vizuri.
Wakili Kisabo aliwahakikishia wanahabari wanaoandika habari za mazingira usaidizi wa kisheria kama wakikumbana na madhira mbalimbali ya kikazi.
Wakili Kisabo pia alielezea nafasi ya wanahabari katika kusaidia jamii,ikiwepo pia kutohofu kufikisha mashauri yao mahakamani katika kesi za maslahi ya umma.
Mwanahabari mkongwe, Edwin Soko akitoa mada katika mafunzo hayo, aliwataka wanahabari kutambua wanawajibu mkubwa kuwa wasemaji kwa wasio na sauti.
Mafunzo hayo yanashirikisha wanahabari 35 kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na baada ya mafunzo kwa kandanya mafunzo hayo yataendelea katika kanda nyingine.








