Na Mwandishi wa OMH, Dar es Salaam
Tanzania imeonesha nia ya kutumia uzoefu wa China katika mageuzi ya mashirika ya umma, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuongeza ufanisi, faida na uwajibikaji katika uwekezaji wa umma.
Nia hiyo ilibainishwa Jumatatu, Mei 18, 2026, wakati Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, pamoja na ujumbe wake, walipotembelea Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na menejimenti ikiongozwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, kuhusu uwekezaji, maendeleo ya miundombinu na uhamishaji wa teknolojia.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mchechu alisema Tanzania inalenga kujifunza kutoka China katika kusimamia na kuleta mageuzi ya mashirika ya umma kupitia mfumo wa Tume ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mali za Serikali ya China (SASAC), akibainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni taasisi ya kimkakati yenye dhamana ya kusimamia uwekezaji wa Serikali.
Alisema kutokana na jukumu hilo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaona umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za China, hususan katika maeneo ya uwekezaji, usimamizi wa mashirika ya umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tunapofanya mageuzi ya taasisi zetu, tunataka kujifunza kutoka kwa nchi ambazo zimefanikiwa kupitia njia hii. China ni mojawapo ya mifano bora duniani katika kufanya mageuzi kwenye mashirika ya umma,” alisema.
Bw. Mchechu alisema baadhi ya mashirika yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina tayari yana ushirikiano mzuri na taasisi mbalimbali za China, hali ambayo imeongeza umuhimu wa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Pande hizo mbili pia zilijadili umuhimu wa kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa mashirika ya umma, utekelezaji wa mageuzi ya taasisi pamoja na maendeleo ya miundombinu na uhamishaji wa teknolojia.
Bw. Mchechu alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa sasa inasimamia taasisi na kampuni 308 ambazo serikali ina uwekezaji, zikiwemo 252 ambazo Serikali ina hisa nyingi.
Alieleza kuwa uwekezaji huo umefanywa katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo usafiri wa anga, nishati, mafuta na gesi pamoja na madini.
Aidha, alisema serikali inaendelea na mageuzi ya kupunguza utegemezi wa ruzuku, kuongeza mchango wa gawio serikalini, kuimarisha uwajibikaji wa taasisi na kutoa uhuru zaidi wa kiutendaji kwa mashirika ya umma.
“Hata kama tunataka uchumi uongozwe na sekta binafsi, sekta ya umma isiyo na ufanisi itaendelea kuwa kikwazo kwa sekta binafsi kustawi,” alisisitiza.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Mchechu pia aligusia ushirikiano unaoendelea kati ya Tanzania na China katika miradi ya kimkakati ikiwemo usafiri wa majini, madini na uendeshaji wa bandari.
Pia aliishukuru China kwa kuendelea kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, akieleza kuwa watumishi sita walinufaika na mafunzo mwaka jana huku wengine watatu wakitarajiwa kupata mafunzo mwaka huu.
“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka na yana mchango mkubwa katika kujenga uwezo wa watumishi wetu,” alisema.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mingjian alisema China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa mageuzi ya kiuchumi na mabadiliko ya taasisi.
Alisema sera ya Mageuzi na Ufunguaji Uchumi ya China iliyoanza mwaka 1978 ilisaidia kuibadilisha nchi hiyo kiuchumi licha ya changamoto kubwa katika miaka ya awali ya utekelezaji.
“Tuko tayari kabisa kushirikiana na ndugu zetu wa Tanzania katika uzoefu huu wa kitaasisi,” alisema.
Aliongeza kuwa China itaendelea kuunga mkono ajenda ya Tanzania ya viwanda kupitia biashara, miundombinu, teknolojia na mafunzo ya watumishi.
Pia alibainisha kuwa serikali ya China itaendelea kutoa nafasi za mafunzo kwa watumishi wa umma wa Tanzania katika maeneo ya mabadiliko ya kidijitali, utawala na usimamizi wa uchumi.
Balozi mingjian alisema Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wenye kuaminiana, akitaja ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China mwaka 2022 kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili.
Kikao hicho pia kilijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika uongezaji thamani wa madini, ambapo Tanzania inalenga kuanzisha viwanda vya ndani vya kusafisha na kuchakata madini ya kimkakati.
Vilevile, pande hizo mbili zilijadili mustakabali wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ambayo mwaka huu inatimiza miaka 50 ya uendeshaji wa kibiashara.








