Na Aziza Nangwa, Jamhuri Media, Dar es Salaam

Wafanyabiashara wa spare za pikipiki nchini kupitia Chama cha Wauza Spare za Pikipiki Tanzania (CHAWASAPI), wameiomba serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kusimamia kikamilifu sheria zinazodhibiti ushiriki wa wageni katika biashara za rejareja, wakidai uwepo wa ushindani usio wa haki unaowaumiza wafanyabiashara wazawa.

Wito huo umetolewa leo Mei 19, 2026, katika mkutano wa wafanyabiashara zaidi ya 50 wa spare na pikipiki uliofanyika katika Hoteli ya Cate, iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hutuba yake Mwenyekiti wa CHAWASAPI, Renatus Sengo, amesema wafanyabiashara wazawa wameendelea kuathirika kutokana na wageni kujihusisha na biashara ambazo kisheria zinapaswa kufanywa na Watanzania.

Amesema licha ya kuwepo kwa maelekezo ya Rais kuhusu umuhimu wa kulinda wafanyabiashara wazawa pamoja na sheria zilizotungwa kusimamia biashara hizo, bado utekelezaji wake umekuwa hafifu.

“Sekta yetu imeendelea kuathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na wafanyabiashara wa kigeni kujihusisha na biashara za rejareja ambazo kisheria zinapaswa kufanywa na wazawa,” amesema Sengo.

Alidai hali hiyo imeendelea kudhoofisha mitaji ya wafanyabiashara wazawa, kupunguza ajira kwa wananchi na kuua ushindani wa haki katika biashara ya spare za pikipiki.

Amesema chama hicho hakipingi uwekezaji wa wageni nchini, bali kinataka sheria zilizopo zisimamiwe kwa usawa ili kulinda biashara za wazawa pamoja na ajira za Watanzania.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Mtei, amesema wafanyabiashara wengi walikuwa wakisafiri kwenda China kuagiza bidhaa moja kwa moja, lakini hali imebadilika kutokana na kushuka kwa mitaji yao.

Amesema kwa sasa wafanyabiashara wazawa wamekuwa wakinunua bidhaa
kutoka kwa wageni waliopo nchini, hali inayowapunguzia faida na uwezo
wa kukuza biashara zao ,wakati huko nyuma tulikuwa tuna uwezo wa kwenda China kuchukua bidhaa wenyewe, lakini sasa tumekuwa wateja wa wageni wanaotuuzia hapa hapa nchini,” amesema .

Kwa upande wake, mfanyabiashara Max Mlewa alisema biashara ya spare
inahusisha usalama wa maisha ya watu, hivyo ni muhimu sekta hiyo kusimamiwa kwa karibu.

Amesema licha ya kuwepo kwa sheria zinazolinda biashara za wazawa, bado wageni wanaendelea kufanya biashara hizo waziwazi huku mamlaka husika zikishindwa kuchukua hatua.

“Sheria ziko wazi kuwa biashara za wazawa zifanywe na wazawa wenyewe, lakini bado tunashindana na wageni katika maeneo yale yale,” amesema .

Menlick Daniel amesema amekuwa katika biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 20, lakini kwa sasa hali ya biashara imezorota kwa kiasi kikubwa.

Amesema hapo awali alikuwa na uwezo wa kuingiza makontena zaidi ya 10 ya bidhaa, lakini sasa uwezo huo umepungua kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara wa kigeni.

Daniel amedai wageni wamekuwa wakinufaika zaidi kutokana na kupata
mikopo yenye riba nafuu kutoka katika nchi zao tofauti na wafanyabiashara wazawa.

Kwa upande wake, Fransisco Msigwa amesema hata maeneo ya vijijini
ambayo yalikuwa soko kubwa la wafanyabiashara wazawa sasa yamevamiwa
na wageni, jambo linalozidi kupunguza mapato yao.

Amesema hali hiyo imeathiri hata juhudi za kuwainua vijana waliokuwa wakifundishwa biashara hiyo ili waweze kujitegemea baadaye.

Wafanyabiashara hao kwa pamoja wameiomba serikali kupitia Wizara ya
Viwanda na Biashara pamoja na mamlaka nyingine husika kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu ili kulinda biashara za wazawa na uchumi wa taifa.