WAZIRI  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho amesema Serikali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) itaendelea kuimarisha mafunzo kwa vijana pamoja na kuendeleza kilimo cha kimkakati ili kujenga uzalendo, kujitegemea na kuchangia usalama wa chakula nchini.

Dkt. Nyansaho aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, vijana 34,000 wa kundi la lazima walipatiwa mafunzo kupitia Operesheni Nishati Safi, ambapo wavulana walikuwa 25,469 na wasichana 8,531.

Aidha, alisema vijana 12,000 wa kundi la kujitolea walipata mafunzo kupitia Operesheni Miaka 60 ya Muungano katika mwaka wa fedha 2024/2025, huku vijana wengine 12,000 wakiendelea na mafunzo chini ya Operesheni Nishati Safi.

Dkt. Nyansaho alisema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kambi za JKT ili kuhakikisha wahitimu wote wa Kidato cha Sita wanapata nafasi ya kujiunga na mafunzo hayo.

Alieleza kuwa hadi sasa kambi za JKT zina uwezo wa kuchukua vijana zaidi ya 60,000, huku Serikali ikipanga kuongeza uwezo huo hadi vijana 140,000 ifikapo mwaka 2031.

“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ya kijeshi, stadi za kazi na uzalendo ili waweze kujitegemea na kushiriki katika ulinzi na maendeleo ya Taifa,” alisema Dkt. Nyansaho.

Kuhusu kilimo cha kimkakati, alisema JKT inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Mageuzi ya Kilimo wa mwaka 2019/2020 hadi 2027/2028 wenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza gharama za chakula kwa vijana wanaopata mafunzo kambini.

Alisema kupitia mpango huo, JKT imeendelea na ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Chita ambapo ekari 2,500 kati ya ekari 12,000 tayari zimejengewa miundombinu ya umwagiliaji.

Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, alisema JKT ilizalisha tani 1,962.2 za mpunga, tani 5,864 za mahindi, tani 6.52 za maharage pamoja na tani 48 za alizeti.