Rais wangu, wako watu wanaosema, ‘dini zamani!’ Wengine wanasema zaidi ya hapo eti ‘hakuna Mungu!’ Haya ni matokeo ya kazi inayofanywa na baadhi ya viongozi wa dini wa kileo.

Huko tulikotoka viongozi wa dini walikuwa na uwezo mkubwa hata wa kutenda miujiza. Heshima yao katika jamii ilipita heshima waliopata viongozi wote wengine. Baadhi yao sasa wako, ‘mbwi’, wamenyweshwa sumu! Kama ilikuwa ni ibada iliyofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere na kuhutubiwa na baadhi ya viongozi wa dini imewatoa fahamu nao wanaonekana sasa si kitu tena, bali upatu uvumao! Walimsifia mchunga mbuzi kwa kuchunga mbuzi.

Kazi aifanyao Rais wangu ni nzuri kabisa. Kazi njema haihitaji mapambio. Wanapokusanyika timamu  kumsifia timamu, wanaunda shaka na haki ya kuuliza, hii maana yake ni nini hasa? Kazi ya kiongozi makini ni kuona mahitaji na kutafakari namna ya kuyakabili kwa ajili ya jamii anayoiongoza. Rais wangu ameliona hitaji la ndege walilonalo watu wake, amechukua fedha za wananchi akawanunulia ndege. Amefanya kazi aliyotakiwa kufanya kiongozi wa watu. Cha kusifia kikubwa hapa ni nini mpaka watu wazima wayakimbie madhabahu yao wakakongamane katika ukumbi uliopewa heshima ya juu ya jina la Mwenyeheri?

Baba Rais wangu, endelea na kazi njema unayoifanya. Usikubali kufanya kosa kubwa, ukamtanguliza Mungu mbele! Mungu hatangulizwi mbele. Mungu ni wa kumkiri na uwepo wake bila hiyana. Fungua kifua chako Mungu aingie na aishi ndani yako! Atakuongoza katika kutenda mema. Wengine wanamtanguliza Mungu mbele ili huku nyuma wateke, watese na hata watu kupotea!

Akiwa ndani ya moyo wako atakuongoza katika kuyatenda mema yampendezayo naye hataziruhusu tamaa za kimwili alizowaumba nazo wanadamu za kutaka yote yawe yao au yawe kwao kwa gharama za masikini, zitawale! Aliye na Mungu ndani yake mamlaka makubwa na mali nyingi hata zikiwa mikononi mwake, haviwezi kumfanya awe na kiburi. Atakubali kushauriwa na kukosolewa kwa sababu atajua kuwa hakuna aliye mkamilifu. Roho ya Mungu humuondolea mtu umimi na kujitukuza!

Katika mahubiri yake Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, hakuonyesha uelewa kuwa labda ni nyoka peke yake hapa duniani ndiye anayeuawa kutokana na jina lake tu. Lakini Dunia haikuwahi kumchukia Musolini kwa sababu ya jina lake. Wala katika kumbukumbu zote za ulimwengu huu, hakuna popote panapoonyesha kuwa Adolf Hitler alichukiwa kwa sababu ya jina lake! Hawa wanakumbukwa kwa sababu ya udikiteta wao. Kinachokumbukwa hapa ni udikteta majina yao hayajalishi. Sasa Mwadhama kwa maana yako ya udikiteta wafafanulie masikini wa nchi hii mfano wako ulikuwa na maana gani!

Baba Mwadhama, Rais wangu alipofika Kibaigwa umati mkubwa wa watu ulimzunguka. Wakamtolea kero zao ambazo zilikuwa nyingi sana. Baba akawauliza, “Mbunge wa hapa si mheshimiwa Ndugai?’’ Wakamjibu, “Ndiyooo’’. Baba akasema, “Basi Ndugai nitamtuma pia naye aje azungumze nanyi asikilize kero za hapa.’’ Ulitokea mvumo mkali kutoka kwa wananchi waliokuwa wamekusanyika pale. Mvumo ambao ulitoa ujumbe usio shaka hata kwa Baba Rais mwenyewe kuwa wananchi wale hawamtaki mbunge wao Job Ndugai hata kwa kumsikia tu! Watanzania nchi nzima nao wakajua hivyo kuwa Job Ndugai angalau kwa wananchi wa Kibaigwa, hatakiwi,  hafai.

Ndugai mwenyewe alisikia pasipo shaka kuwa wananchi anaodhani anawawakilisha bungeni, hawamtaki. Baba Mwadhama, kukata mzizi wa fitina Rais wangu akawauliza wananchi wale wa Ndugai, “Hamtaki nimtume Ndugai?’’ Mvumo wa kumkataa Job Ndugai ukazidi zaidi ya mwanzo. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenyewe akathibitisha pasi na shaka kuwa Job Ndugai, hatakiwi na wananchi. Akakubaliana nao kwa kusema, “Haya, sitamtuma Ndugai!’’

Kwa nchi za wenzetu ambako viongozi wake hawamtangulizi Mungu mbele, bali huishi naye ndani ya vifua vyao, kukataliwa na wananchi wako mbele ya mkuu wa nchi, angejiuzulu. Lakini kama ubunge wenyewe uliupata kwa kuwapiga washindani wako marungu ya kichwa utaanza kutafuta magongo mengine!

Hawa ni viongozi ambao wakishapita ili kuondoa mikosi katika nchi wanapaswa wasahauliwe moja kwa moja. Kulazimisha wakumbukwe kama anavyokumbukwa Nyerere, wengine wanaweza wakadhani huo ndiyo udikiteta. Mwalimu Nyerere alisema, ‘Tujisahihishe!’

Hakuna aliye mkubwa kuliko nchi. Tangu zamani nchi ina utaratibu wake wa kuweka majina ya viongozi wake wa kukumbukwa kwa mema yao. Tuna Chuo Kikuu cha Sokoine. Tuna Chuo Kikuu cha Mkwawa, tuna Daraja la Mkapa na vingi vya kuwafanya wananchi wamkumbuke Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kumbukumbu hizi hazikutolewa kirafiki na mtu mmoja. Kwa kuwa huyu mnafanya ibada pamoja, basi akumbukwe, hapana! Au utotoni zamani mliwahi kuiba pamoja, basi nyumba hii iitwe jina lake ‘Chakupewa’! Hapana baba! Hapana, hatufanyi hivyo! Huyo aliyekataliwa na wananchi mbele yako, tena hadharani, mwache ahangaike la yake! Tusilazimishe jina lake liingizwe katika watu wema wa kukumbukwa bila ridhaa ya wananchi. Tukifikia hapo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo analazimika kurudi katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere akawafafanulie Watanzania maana ya mfano wake. Huo ndiyo u-Hitler? Au huo ndiyo u-Musolini? Au huo ndiyo udikiteta?

Baba Rais wangu, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo alimfahamu vizuri sana marehemu Padri Boniface Songoro wa huko huko kwao Sumbawanga. Alikuwa mshauri wa kiroho. Alitoa mfano akasema, kama wewe baba umekaa sebuleni mtoto wako yuko jikoni; unataka kumtuma labda akuletee maji ya kunywa, ukimwita kwa jina lake, ‘fulani!’, badala ya kuitika ‘naam’ au ‘abe’ yeye akaitika kwa kusema, ‘hata, sikombi mboga’; jua mtoto huyo anakomba mboga!

Binti yetu Lady Jaydee aliimba kuwa siku hazigandi. Siku zinakuja! Siku ambazo mwanamwema Profesa Musa Assad atakuja kutukuzwa na jamii yetu! Kweli kweli nawaambieni, zitakuja siku ambazo kila litakapotajwa jina, ‘Ndugai’ kama kumbukumbu ya soko la Dodoma, jina la Musa Assad litajitokeza katika vifua vya masikini na wanyonge wa nchi hii! Kwanini kujitengenezea kumbukumbu ya visasi? Kwa jina la Musa Assad, katika hili, mafisadi wataugua katika vifua vyao siku zao zote za maisha yao! Nalo litadumu sambamba na jina la soko la Dodoma kama itakuwa ni lazima liwe, likiitokosha mioyo ya wananchi wema! Ah! Padri Boniface Songoro nawe katika hili utakumbukwa! Aliita kwa jina tu mwana yule akasema, ‘sizioni 1.5!’ Ikatokea sauti hata sijui ilikuwa ya nani badala ya kuitika ‘naam’ au ‘be’ ikaitika, ‘nani kaiba?’ Muda utakapoenea, utasema!

By Jamhuri