Jamii ikatae uzinifu, ikuze maadili

Kijana mmoja alimwendea Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akamwambia: “Ewe Mtume wa Allaah, nipe idhini ya kuzini.” Watu wakamzunguka na kuanza kumuonya. Vipi anamuomba Mtume wa Mwenyezi Mungu ruhusa ya kufanya maasi? Mtume akawaambia: Hebu mleteni karibu yangu. Yule kijana akamsogelea Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akakaa.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia zinaa kwa mama yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Vivyo hivyo na watu wengine hawaridhii kwa mama zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa binti yako?

Kijana akajibu: Hapana, Ewe Mjumbe wa Allaah.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa mabinti zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa dada yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa dada zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa shangazi yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa shangazi zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa ndugu wa kike wa mama yako (mama mdogo/mkubwa?)

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu hawaridhii kwa ndugu wa kike wa mama zao (mama mdogo/mkubwa).

Kisha Mtume akaweka mkono wake katika kifua cha kijana huyu na kumuombea dua: “Ewe Allaah msamehe madhambi yake, na uusafishe moyo wake, na ikinge tupu yake.”

Kijana akawa baada ya hapo hageuki kutizama chochote (miongoni mwa maasi).

Uzinifu ni uhusiano wa kingono (kitendo cha mwanamume na mwanamke kujamiiana) nje ya ndoa halali kwa mujibu wa mafundisho ya dini. Visawe vya neno hili uzinifu ni uzinzi, zinaa, uasherati, ukware na dondoo.

Uzinifu ni janga kubwa kwa jamii kwani linahusika katika mchakato wa kuitengeneza jamii kitabia na kisaikolojia na kuamua hatima ya jamii kuwa ya kistaarabu yenye kufanya yale yanayokubalika kidini au kuwa ya jamii ya kishetani inayoongozwa na matamanio ya kila mwanajamii na uhuru usio na mipaka. Uzinifu ni dhambi kubwa na una athari mbaya kwa mtu mmoja mmoja na jamii.

Uzinifu ni dhambi kubwa ambayo tumetakiwa kujiweka mbali nayo na kutoikaribia kwa kujiepusha na kila ambacho kitatufanya kuangukia katika janga hili kubwa. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 17 (Surat Al-Israa/Bani Israil) Aya ya 32 kuwa: «Wala msiikaribie zinaa kwani hiyo zinaa ni uchafu na ni mwenendo mbaya.»

Uzinifu ni miongoni mwa madhambi yanayoiathiri imani ya muumini kama anavyotunabahisha Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kuwa: “Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pindi anapokunywa pombe hali ya kuwa ni muumini, hapori mwenye kupora pindi anapopora, jambo linalofanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”

Mbali ya athari hii ya kupungua imani ya muumini, uzinifu una athari mbalimbali katika nyanja zote za maisha.

Mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu anayenasibika na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Ziko athari sita za zinaa, tatu ambazo zinapatikana humu duniani na tatu zitapatikana huko akhera. Zile zitakazoonekana duniani ni: (1) Kuondosha heshima ya mtu na kumdhalilisha; (2) Kumfanya mtu awe masikini; (3) Kufupisha umri wa maisha yake (yaani kufa haraka). Na zile zitakazopatikana akhera ni: (1) Adhabu za Allaah Mtukufu; (2) Hali ngumu kabisa katika utoaji wa hesabu; na (3) Kutumbukizwa katika Jahannam na kukaa humo milele.”

Naam, bila shaka uzinifu una madhara makubwa ya aina mbalimbali na jamii imeathirika kwa namna moja au nyingine na madhara haya yanayowapata watu wake na pia mzigo unaobebwa na jamii ukiwa ni matokeo ya madhara ya uzinifu.

Nani asiyeathirika na mzigo wa ulezi wa watoto waliopatikana kutokana na uzinifu wakakosa malezi stahiki kutoka kwa baba na mama na hatimaye ukawa ni mzigo wa familia?

Nani asiyeathirika na madhara yanayoipata jamii kutokana na watoto wasiojua hatima yao mitaani na hatimaye wakakua wakiwa sehemu ya wahalifu wanaoisumbua jamii?

Nani asiyejua madhara yanayoipata jamii kutokana watoto wanaobebeshwa mimba shuleni na kukatishwa safari yao ya kimalezi na kielimu na sababu kuu ikiwa ni uzinifu?

Nani asiyejua familia zilizoathirika kutokana madhara ya magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uzinifu ukiwemo Ukimwi?

Jambo pekee la kushangaza ni jamii kutofanya juhudi thabiti ya kuikataa dhambi ya uzinifu, bali wakati mwingine kuishabikia kwa namna mbalimbali huku ikijielekeza katika kukabiliana na yanayosababishwa na huo uzinifu.

Niliweke wazi hili kwa mifano michache ifuatayo: Jamii yetu imefikishwa mahali kuona uzinifu ni jambo la kawaida kiasi cha hata baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuushabikia kwa kuwatangaza wakware na taarifa za uzinifu wao kwa kiwango cha kuihamasisha jamii, hususan vijana kupambana katika kutengeneza historia zao za uzinifu.

Jamii inaonekana kuburudika na vishawishi vya uzinifu kiasi hakuna anayekemea uwepo wa vishawishi vya uzinifu katika jamii ukiondoa hatua zinazochukuliwa na vyombo vya kimamlaka kama vile Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Hata baadhi wanaharakati hawasumbuliwi na uzinifu, bali matokeo ya uzinifu kama mimba zisizotarajiwa hususan kwa wasichana walio shule za msingi na sekondari kiasi cha kusimamia kampeni ya kiitwacho “ngono salama” kwa kuwafundisha matumizi ya mipira ya kiume na ya kike na hata kuwahurumia kwa kuitaka serikali ilegeze msimamo ili wafanye uzinifu kwa uhuru kabisa; wapate mimba; wajifungue bila ya jamii kuwanyanyapaa na baada ya hapo warudi shuleni kuendelea na kumaliza masomo waliyokatisha!

Yaani, tatizo si uzinifu ambao ni dhambi kuu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu na Ukristo, bali tatizo ni mimba zisizotarajiwa na katika umri mdogo! Haya yanafanyika bila ya kuzingatia ukweli kuwa ikiwa sasa ambako mwanafunzi anayepata mimba akiwa shule ya msingi au sekondari anafukuzwa shule kama njia ya kuzuia uzinifu kwa wanafunzi (punishment)  bado tunasoma kupitia vyombo vya habari kuwapo kwa wilaya moja nchini Tanzania ambayo wanafunzi wasichana  zaidi ya 100 wamekatisha masomo mwaka huu wa 2019 kutokana na mimba; hali itakuwaje iwapo wanafunzi watahakikishiwa kuwa uzinifu na kupata mimba hakukatishi safari yao ya kimasomo?

Vipi mimba hizi zitakosekana wakati sababu kuu uzinifu jamii inaishabikia kwa njia mbalimbali na wazinifu ndio wanaopamba kurasa za magazeti yetu na mitandao ya kijamii wakati ambao baadhi ya wanaharakati na taasisi zinatumia fedha nyingi kuhamasisha ‘ngono salama’ kwa wanafunzi hawa hawa na kuandaa matamasha ya kuwagawia bure mipira ya kiume na ya kike na kuwapa elimu ya kuitumia?!

Nihitimishe makala hii kwa kumnasihi kila mmoja wetu na jamii kwa ujumla kuukataa uzinifu kwa kuyakataa na kuyapiga vita kijamii yale yote yanayochochea dhambi hiyo na kufanya juhudi za makusudi hata kwa kutunga sheria ndogo ndogo (by-laws) zinakazochochea na kuhamasisha ukuaji wa maadili mema katika jamii kwa mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa ujumla.

Tuhamasishane kama jamii na hususan jamii ya Kitanzania kuziba ufa wa mmomonyoko wa maadili katika kuta za taifa letu ili tusilazimike kujenga ukuta huku tukipambana na wanaotuzuia kuujenga miongoni mwa wanajamii wenzetu.

Shime, jamii ikatae uzinifu, ikuze maadili mema.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.