Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

MKOA wa Mtwara umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayochangia kwa kiasi kubwa ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike hali inayohusishwa wa utekelezaji wa mila za jando na unyago.

Akizungumza leo mkoani Mtwara katika uzinduzi wa siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mtwara, mwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani humo, Baltazar Komba amesema wanaendelea kuandaa mipango na miradi yenye kutoa vipaumbele ili kuwajengea uwezo watendaji wa kimila wakiwemo makungwi na mangariba.

Uzinduzi huo umefanyika leo Novemba 25, 2023 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo kilele chake kitafanyika Disemba 10 wilayani Masasi mkoani humo.

Kampeni iliyoandaliwa na mashirika hayo chini ya mtandao wa Mtwangonet kwa kushirikiana na ofisi ya maendeleo ya jamii mkoani humo kupitia kauli mbiu inayosema, ‘Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia’

‘’Mtwara ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza mila ya jando na unyango kama sehemu ya mila na tamaduni zinazoitambulisha tamaduni za mikoa hii na mila hizi ni majukwaa muhimu ya tamaduni dhidi ya ujenzi wa vijana kuelekea katika utu uzima’’ameseme Komba

‘’Huko wanafunzwa mambo mengi sana ya kuwajenga katika kipindi hicho cha kuelekea ujana, mila ambazo zinatajwa mara kadhaa katika tafiti za kitaaluma, makongamano ya kitaaluma na hata maoni ya wadau mbalimbali wa maenedeleo kuwa na viashiria ya kuchangia mtoto wa kike na wa kiume kujiingiza kwenye mahusiano na ngono za mapema, mimba za mapema na ndoa za utotoni’’

By Jamhuri