Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

MKAZI wa kijiji cha Katale Buzirayombo Wilayani Chato mkoani Geita,Hassan Ramadhan (29) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mapenzi na mwanaye ya kike mwenye umri wa miaka 12 kinyume cha sheria za nchi.

Uamuzi huo umetolewa leo Januari 19, 2024 mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Chato, na hakimu mkazi wa mahakama hiyo,Erick Kagimbo baada ya kukamilika kwa ushahidi uliotolewa na pande zote mbili katika kesi namba 579 ya mwaka 2023.

Awali mwendesha mashitaka wa Polisi,Mauzi Lyawatwa,ameiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alituhumiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2020 hadi 2023 alipokamatwa baada ya mhanga wa tukio hilo kutoa taarifa za kufanyiwa ukatili huo kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho.

Baada ya taarifa kufikishwa Jeshi la Polisi mtuhumiwa alikamatwa Agosti 27 mwaka 2023 kabla ya kufikishwa mahakamani Agosti 31 mwaka 2023 kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema kwa nyakati na maeneo tofauti mshitakiwa alikuwa akimuingilia kimwili mtoto wake wa kuzaa kwa madai anamuondolea mkosi alionao kutokana na mtoto huyo kuota meno ya juu baada ya kuzaliwa na kwamba asingeweza kuolewa na mwanaume yoyote.

Pasipo kujua nia ovu ya mzazi wake,mtoto aliendelea kutunza siri na kushindwa kumweleza mama yake wa kufikia(mama wa kambo) akihofia kupigwa na kufukuzwa nyumbani na baba yake huyo.

Hata hivyo kitendo hicho kiliendelea kumsononesha mtoto huyo na kulazimika kumweleza shangazi yake,pamoja na bibi yake ambao hawakuchukua hatua za haraka mpaka pale alipolazimika kwenda kwa mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye aliambatana na mtoto huyo kwenda kituo cha polisi kuripoti unyama huo.

Mwendesha mashitaka huyo amesema kitendo cha kufanya mapenzi na ndugu wa damu ni kinyume na kifungu cha 158(1) Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Aidha kutokana na maelezo hayo pamoja na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambao uliwasilisha mashahidi sita akiwemo mtoto(mhanga wa tukio), mama wa kambo(mke wa mshitakiwa) shangazi, mwenyekiti wa kijiji,polisi aliyechukua maelezo ya awali pamoja na mhudumu wa afya aliyefanya uchunguzi wa kitabibu, umetosha kuithibitishia ukweli mahakama hiyo kwa lengo la kutenda haki kwa pande zote mbili.

Mbali na mshitakiwa kupatikana na hatia ya kutenda kosa hilo, mahakama hiyo imempa nafasi ya kuomba huruma ili kupunguziwa kifungo ambapo ameomba kupunguziwa adhabu kwa madai ni mgonjwa na anafamilia kubwa inayomtegemea kuihudumia.

Hata hivyo Mheshimiwa hakimu mkazi wa mahakama hiyo, akitoa hukumu amesema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa kwa pande zote mbili na aina ya kosa analoshitakiwa nalo, sheria inafunga mikono kuamua vinginevyo badala yake atakwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa wafu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.

Kadhalika amesema mshitakiwa anayo nafasi ya kukata rufaa ndani siku 45 iwapo atakuwa hajaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo, na mshitakiwa amechukuliwa kwenda gerezani kuanza kutumikia kifungo chake.