Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) na Jeshi la Polisi Tanzania (TPF) kupitia Shule ya Polisi-Moshi wamezindua rasmi ushirikiano wa kitaaluma, uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa wiki,katika Chuo Cha Polisi Moshi.

Akizindua rasmi ushirikiano huo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camilius Wambura, ametoa pongezi kwa taasisi hizi mbili na kusema siku hii imeandika historia kubwa kutokana na ushirikiano huo kuwa na tija kwa Jeshi la Polisi na watendaji wake kwa ujumla.

‘’Tarehe 30 Agosti 2022 Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alishauri Jeshi la Polisi kuboresha Mifumo yake ya utendaji kazi hasa katika kuzuia uhalifu wa mitandao, hivyo ushirikiano huu wa kitaaluma unaenda kutekeleza agizo hili’’ Amesema IGP Wambura.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka ameushukuru uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kuwa tayari kushirikiana na IAA hasa katika suala zima la taaluma.

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa program watakazoshirikiana na Jeshi la Polisi kwenye kutoa mafunzo ni pamoja na Shahada ya Sayansi katika Usalama wa Mitandao, Shahada ya Usalama wa Masomo ya Kimkakati, Shahada ya Uzamili ya Ulinzi wa Taarifa, na Shahada ya Uzamili ya Amani na Masomo ya Ulinzi.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi IAA, Dkt. Mwamini Tuli amesema Jeshi la Polisi limeonyesha nia madhubuti ya ushirikiano, hivyo kupitua elimu watakayoipata itasaidia kuboresha ulinzi na usalama,na kwa pamoja watahakikisha wanawaanda watumishi mahiri wenye weledi mkubwa.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na makamanda wa polisi, wafanyakazi wa IAA pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.