Mheshimiwa Rais, awali ya yote hongera kwa hotuba yako ya mwisho wa mwezi maana ilijaa lugha tamu ya kidiplomasia inayoonesha namna ulivyo muungwana na usiyependa ugomvi au migogoro na nchi majirani zetu.

Hotuba yako imeonesha ni namna gani una dhamira ya dhati ya kuona utulivu unashamiri kwenye nchi majirani zetu. Hotuba yako ilionesha ukomavu mkubwa wa dhamira ya kuona amani ambayo ni tunda la haki ikitamalaki kwenye nchi za wenzetu.

Katika kipindi chako dhamira yako ulishaionyesha kwa vitendo nchi jirani ya Kenya, ulifanya hivyo kwa Comoro na Madagascar, huku kote ulikotoa ushauri wako hukuwahi kutukanwa wala kubezwa bali ulipewa sifa na kuonekana shujaa na hata ulipoamua kutumia vikosi vya majeshi yetu hakuna aliyehoji dhamira yako ya kuitafuta amani.

Kwa majirani zetu wa Rwanda imekuwa tofauti, wao ushauri wako kwao imekuwa nongwa, wamekubeza, wamekutukana, wamekunanga na wamefikia hata hatua ya kukutishia kukupiga.

Binafsi ulipotoa kauli kule Kagera kuwa majeshi yetu yako imara na mipaka yetu iko salama huku ukitahadharisha atakayeleta chokochoko kukiona cha mtema kuni nilijua unajibu mapigo kwa Kagame, kumbe hukuwa na maana hiyo wala dhamira hiyo, niliogopa nikajua unataka twende tukamchape Kagame. Mungu ashukuriwe hekima ya kidiplomasia bado iko kifuani pako.

Hata hivyo, baada ya kusikiliza hotuba yako hiyo nataka kuwa mshauri wako kuhusiana na dharau, matusi na dhihaka zilizooneshwa na Wanyarwanda juu yako na kwetu Watanzania, najua una washauri wengi na wabobezi kwenye mambo mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, kijamii na hata kiimani, najua washauri wako wanafanya kazi yao vizuri usiku na mchana kwa weledi na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Busara imenituma kukushauri, mimi ni muungwana wa kijiwe cha kahawa nisiye kuwa na wadhifa wala hadhi ya kukuona ninapojisikia kufanya hivyo kwa muda wowote lakini najua nina uwezo wa kukufikia kwa njia ya maandishi ambayo kwangu ina nguvu kuliko kuja kubisha hodi kwenye nyumba tuliyokupangisha.

Naomba nianze kwa kunukuu maneno yako kwenye hotuba yako ya mwisho wa mwezi, umesema “Ushauri si shuruti, ushauri si amri, una hiyari ya kuukubali au kuukataa.” kwa heshima na taadhima naomba ushauri huu ninaokupa usiukatae kwa sababu eti si shuruti au amri.

 

Wewe nifanye mimi mjinga na upokee tu maana nataka kukuepusha na kikombe cha matusi na dharau kutoka kwa viongozi wa nchi nyingine ambao huenda baadaye ukajisikia kuwashauri kama ilivyotokea kwa Kagame na wao kuamua kufuata mkondo alioufuata Kagame.

Mheshimiwa Rais kipindi hiki achana kabisa na nia au dhamira ya kutoa ushauri kwa kiongozi yoyote mwenye nchi yenye mgogoro wa amani, natambua unajua kuwa amani ni tunda na zao la haki bali amani si tunda na zao la maombi kama baadhi ya viongozi wa chama chako wanavyopotosha. Lakini pia natambua kuwa haki ina mbegu ya upendo ndani yake.

Hivyo, kabla hujatenda upendo kwa mtu mwingine lazima ujipende kwanza mwenyewe na kabla ya kuonesha njia ya haki lazima wewe mwenyewe uitende haki na kuonekana kweli kuwa haki imetendeka.

Msingi wa mimi kukushauri usimshauri tena kiongozi mwingine wa nchi nyingine umelala kwenye mafundisho ya dini zetu tunazoziabudu, dini zote zinatabia moja kuu, zinafundisha upendo na kutendeana haki huku zote zikiamini kuwa haki ndio msingi wa upendo na amani.

Mafundisho ya dini yanatufundisha kuusema ukweli hata kama utaumiza vishikizo vya mioyo yetu, lakini pia mafundisho hayohayo yanatufundisha kuondoa kibanzi kwenye macho yetu kabla hatujafikiria kuondoa boriti kwenye macho ya wenzetu, huu ni misingi muhimu sana tuliowekewa kwenye mafundisho ya dini zetu na naamini ni udhaifu wa kutokufuata mafundisho haya ndiyo umesababisha Wanyarwanda kutudharau, kukudharau wewe na hata kukutukana kama nilivyokusikia ukilalamika.

Katika kipindi cha uongozi wako hasa ngwe hii ya mwisho kumekuwa na matukio mabaya sana na ya kuogofya ambayo pia naamini hata shetani ametushangaa kama Watanzania kuwa tabia hii imetoka wapi! Wapo Watanzania wenzetu waliopoteza maisha mikononi mwa polisi, kumetokea vifo vingi vyenye utata, kuna watu walitekwa, wameteswa  na kung’olewa meno na kucha bila hata ganzi, haya yote yametokea sauti za Watanzania zikapazwa lakini jitihada zako za dhahiri za kukomesha vitendo hivi hazijaonekana kwa dhati. Ndiyo maana nikasema nikushauri kwa dhati ya moyo wangu ili uhakikishe kwanza haki inatendeka nyumbani kwako kabla ya kwenda kushauri kwenye nyumba ya Kagame.

Japo kabla yako nilishahadithiwa kuwa yalipata kutokea mauaji ya Mwembe Chai na ya vurugu za uchaguzi wa Zanzibar ambazo zilisababisha wakimbizi kule Shimoni (Mombasa) nchini Kenya wakati wa mzee Mkapa lakini nimejikuta najiuliza maswali yafuatayo: Umethubutu vipi kwenda kumshauri Kagame apatane na waasi wakati wewe umeshindwa kutekeleza ombi la barua ya chama hasimu (Chadema) kwa chama chako kuhusu kuunda tume huru ya kimahakama itakayoongozwa na majaji kuchunguza vifo vyenye utata vilivyotokea kwenye mikutano ya chama hicho pamoja na vifo vingine vyenye utata?

Umethubutu vipi kwenda kumshauri Kagame wakati wewe ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi na jeshi lako la polisi kwenye moja ya ripoti linaonekana kuwa ni jeshi ambalo linakiuka haki za raia ikiwemo kubambikiza kesi na kutunga mashtaka ya uongo na kesi za ugaidi ambazo hazipo?

Umepata wapi uhalali wa kimaadili (moral authority) kutumia busara kumshauri Kagame aongee na wapinzani wake kisiasa wakati wewe umeshindwa japo kukaa na viongozi wa chadema kujadilina nao na kujua sababu za wao kukamatwa mara kwa mara na kwa kesi za mfululizo zisizo kuwa na kichwa wala miguu?

Nimejiuliza, umepata wapi mamlaka ya kimaadili kumshauri Kagame aongee na waasi wapinzani wakati wewe kupitia hotuba ya mwisho wa mwezi ulishalalamika kuwa Chadema wanafanya maandamano ili kuondoa serikali iliyoko madarakani kihalali kama ilivyotokea Misri na Libya huku ukiwa hujawahi kukaa na Chadema hao hao ukawauliza kama ni kweli walikuwa na mpango huo? Na mlifikia muafaka gani?

Bado najiuliza, umepata uhalali gani wa ki-maadili kumshauri Kagame aongee na wapinzani waasi wakati wewe umeshindwa japo kuwapa pole Chadema ambao ni wahanga waliolipuliwa mabomu kwenye mikutano yao kadhaa huku wewe ukikaa kimya?

Naendelea kujiuliza, umepata uhalali gani wa kimaadili kumshauri Kagame aongee na wapinzani waasi wakati Waziri Mkuu wako akitoa amri zenye utata? Mara anayeua albino naye auawe, mara “wapigwe tu maana sasa tumechoka”. Hivi ninyi mliochoka mnatoaje ushauri kwa wengine ambao hawajachoka?

Rais wangu, dawa pekee ya kuepuka matusi na kejeli na kutuepusha sisi na kikombe cha kejeli dhidi ya mataifa mengine achana na habari za kutoa ushauri kwa wengine, tukae chini tumalize matatizo yetu, tutoe boriti kwenye jicho letu ndiyo turuke kiguu na njia kwenda kuwashauri wengine.

Chukua ushauri wangu na kwa kuwa tuko kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani kabla ya kufungua kwa Sikukuu ya Eid nikutakie funga njema na Eid Mubarak Sheikh Jakaya Mrisho Kikwete.

“Tukosoane, turekebishane, tuwajibishane, ndipo tusameheane,” Regia Mtema.

0713 246  764/ 0784 246 764


1107 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!