Na Mwandishi Maalumu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanywa na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo walisema licha ya kupata huduma za matibabu pia wamefurahia kupata elimu ya lishe ambayo imewasaidia kufahamu namna bora ya kuchagua makundi ya vyakula. 

Mzee Abdalah Yasini mkazi wa Temeke alisema inawezekana kupatwa kwake kwa tatizo la mishipa ya damu kuziba kulisababishwa na kutokupata elimu ya lishe bora kwani angejua toka zamani namna ya kula chakula chenye mchanganyiko wa makundi yote ya vyakula kwa kiasi angeweza kuepuka tatizo la mishipa yake ya damu kuziba.

“Ninawaomba wataalamu wa lishe watafute namna ya kufikisha elimu ya lishe bora kwa jamii hata ikiwezekana katika vyombo vya habari kuwe na kipindi cha lishe kitatusaidia sana”, alisema Mzee Abdalah

Mzee Abdalah alisema kama jamii itazingatia lishe bora kwa kutumia makundi yote ya vyakula kwa kiasi kutasaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuwa na jamii yenye afya bora.  

Mama Yusta Joseph mkazi wa Kimbiji Dar es Salaam alisema elimu ya lishe aliyoipata inaenda kumbadilisha kwa kiasi kikubwa kwani kuna vitu amekuwa akivifanya ili kupunguza uzito kumbe alikuwa akifanya kimakosa.

“Elimu niliyoipata leo itaenda kunisaidia kwani nilikuwa najitahidi kupambana kupunguza uzito kwa kutumia njia ambayo si sahihi, nilikuwa sili milo ya asubuhi na mchana nakula usiku tu lakini nilivyofika hapa mtaalamu amenipa maelekezo kuwa ninapokula jioni na kwenda kulala sehemu kubwa ya chakula hutunzwa kama mafuta”, alisema Yusta

Yusta alisema mtaalamu wa lishe amemshauri kupunguza mlo wa jioni na namna ya kupata chakula bora kuanzi mlo wa asubuhi hadi jioni huku akimpa mbinu za kupunguza uzito wake bila ya kuleta athari nyingine za kiafya.

“Kwakweli elimu niliyoipata leo haitakuwa ya msaada kwangu tu bali ninaenda kuisaidia familia yangu kwasababu mimi ndio mama yao na mimi ndio mpishi hivyo ninaenda kuwasaidi pia katika kuboresha afya zao”, alisema Yusta

Mkuu wa Kitengo cha Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Maria Samlongo alisema wamekuwa wakitoa elimu ya lishe bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo pamoja na wananchi wanaohudumiwa katika kambi ambazo wamekuwa wakizifanya.

Maria alisema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu ya lishe bora inawafikia wananchi wengi zaidi.

“Bado elimu ya lishe haijaweza kuwafikia watu wote kutokana na uchache wa wataalamu wa lishe, kama JKCI tumetengeneza vipeperushi mbalimbali vinavyotoa elimu ya umuhimu wa lishe bora katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Maria 

Katika kambi hiyo jumla ya watu 364 walipatiwa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo ambapo kati yao watoto walikuwa 41 na watu wazima 323.

Watoto 11 walikutwa na matundu kwenye moyo, shida za valvu na mishipa ya damu huku watu wazima 161 sawa na asilimia 50 walikutwa na matatizo ya shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine ya moyo ikiwemo mishipa ya damu na matatizo ya valvu za moyo.

iani

Afisa Uuguzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Laetitia Kokutangaza akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani

Mfamasia kutoka kampuni ya Microlabs Laborex Zawadi Mbasa akimpatia dawa mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani

Daktari wa Hospitali ya JKCI Dar Group Masanja James akipa maelekezo mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

 Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Saadi Kamtoi na Loveness Mfanga wakiwafanyia utafiti wananchi waliofika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

By Jamhuri