JKT Tanzania yapongezwa kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu wa 2023/24

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu, ameipongeza Klabu ya JKT Tanzania kwa kurejea kucheza Ligu Kuu Soka Tanzania Bara msimu mwaka 2023/2024 baada ya kumaliza vinara katika ligi Championship msimu 2022/2023.

Yakubu ametoa pongezi hizo Mei 14, 2023 katika hafla ya kukabidhi kombe kwa mabingwa hao, mara baada ya kushuhudia mchezo maalum kati ya JKT Tanzania dhidi ya Transit Camp uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na JKT mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya magoli 2-2.

“Kwanza leo nimefurahi sana kuona mchezo mzuri, mkali, wa kuvutia ambao umeisha kwa sare ya 2-2 baina ya JKT na Transit Camp na ni mchezo lengo la mchezo huu ni kukabidhi kikombe kwa mabingwa wa ligi daraja la kwanza JKT. Tunawashukuru sana Jeshi kwa kujali michezo na nitoe wito kwa vyombo vingine vya ulinzi waungane na jeshi ili tuendelee kuinua sekta hii ya michezo nchini,”amesema Yakubu.

Aidha, Yakubu ameipongeza Bodi ya Ligi pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa juhudi wanazofanya kuipandisha thamani Ligi ya Tanzania, jambo ambalo limewavutia wachezaji wengi wa kigeni kuja kucheza soka la kulipwa nchini.

“Niwapongeze sana bodi ya ligi pamoja TFF kwa kijihada walizozifanya na kuipandisha thamani ligi yetu, na nimekuwa nikizungumza na baadhi ya viongozi wa vilabu hapa nchini, wanakiri kabisa ligi yetu inawavutia wachezaji wengi wa kigeni kuja kucheza soka la kulipwa hapa nchini,”amesema Yakubu.