Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Kituo cha Upandikizaji Mimba cha Kairuki Hospital Green IVF (KHGIVF), kimeendesha mafunzo kwa madaktari wa hospitali mbalimbali kuhusu namna bora ya upandikizaji mimba.

Mafunzo hayo yametolewa leo kwenye kituo hicho, Bunju A Mianzini jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na madaktari zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kituo cha KHGIVF ambacho kilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi miaka miwili iliyopita kiko chini ya Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN).

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Clementina Kairuki,  Bunju A Mianzini, wakati wa mafunzo kwa madaktari mbalimbali kuhusu namna bora ya upandikizaji mimba.

Dk. Clementina alisema wanawake wengi wameshafanyiwa upandikizaji mimba kwenye kituo hicho na kufanikiwa kupata watoto lakini wengi walijifungulia kwenye hospitali mbalimabli na wengine nje ya nchi na wamekuwa wakifuatilia hali zao za afya.

Mkurugenzi wa hospitali ya Kairuki, Dk Asser Mchomvu akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku mbili Bunju A

“Tunawafuatilia na wanaendelea vizuri sana watoto na mama zao na watanzania hawana sababu ya kuhangaika kutumia gharama kubwa kwenye mataifa ya Ulaya kwasababu huduma hii sasa inapatikana hapahapa nchini na yenye mafanikio makubwa sana,” alisema

Alisema kituo hicho kimekuwa ikipokea wanawake wengi wengine wakitokea mikoani ambao hufanyiwa huduma hiyo kwa siku moja na kisha kurudi kuendelea na shughuli zao za kawaida kwenye maeneo yao.

Dk. Clementina alisema wakati wa uzinduzi wa kituo hicho mwaka 2021 waliahidi kwamba hakitakuwa cha kutoa tiba tu bali kitatumika kutoa mafunzo kuelimisha watanzania na kubadilisha uzoefu na wanataaluma wa tiba kuhusu namna bora ya kupandikiza mimba.

“Tumeanza leo kuwapa mafunzo madaktari wenzetu kutoka hospitali mbalimbali nchi nzima kuhusu upandikizaji mimba ili Tanzania isonge mbele kwenye tiba ya upandikizaji mimba,” alisema na kuongeza

“Tunataka kutoa mwelekeo sahihi kuhusu hii tiba ili kama kuna dhana potofu watu wajue ili tufikie wenzetu walipofikia kwenye tiba hii na tunatarajia angalau tufanye mafunzo kama haya kwa mwaka mara pili,” alisema.

Dk. George Tryphone ambaye ni Meneja wa Mabara ya Upandikizaji Mimba wa (KHGIVF), alisema tangu waanze upandikizaji mimba wamepata mafanikio kwani wanawake wengi wameshapata watoto huku wengine wakiendelea kulea mimba katika hatua mbalimbali.

Madaktari wakifanya moja ya mitihani waliyopewa kwenye mafunzo hayo

Alisema kuna baadhi ya wanawake ambao walipandikizwa mimba kwenye kituo hicho na kufanikiwa kujifungua watoto mapacha, watoto watatu kwa mpigo na wengine kujifungua mtoto mmoja mmoja.

Kuhusu mafunzo hayo, Dk. Tryphone alisema jamii bado haijawa na uelewa vizuri kuhusu upandikizaji mimba hivyo wameona ni muhimu kuanza kutoa elimu kwa umma wakiwemo watoa huduma ambao ni madaktari wa hospitali mbalimbali nchini.

“Tumeanza na madaktari tunawapa mafunzo madaktari ili wanaporudi kuwahudumia wanawake wenye changamoto ya kupata ujauzito wawahudumie vizuri katika misingi ile inayohusu msuala ya ugumba ili watatatue changamoto hiyo,” alisema

Alisema suala la kutopata watoto limekua tatizo kubwa nchini kiasi cha watu wengine kulazimika kwenda nchi za nje kupata suluhu ya changamoto hiyo na kulazimika kutumia gharama kubwa na muda mwingi.

Dk. Tryphone alisema kuanzishwa kwa KHGIVF ni ukombozi kwa watanzania wengi ambao walikuwa wakilazimika kusafiri na kutumia gharama kubwa kwani hivi sasa watapata huduma hiyo nchini tena kwa gharama ndogo kulinganisha na nje ya nchi.

“Hapa kwetu mwanamke anaweza kuja akafanyiwa upandikizaji akarudi kuendelea na kazi zake siku hiyo hiyo wakati akienda nje ya nchi shughuli zake zinasimama na  anatumia hela nyingi za kuishi kule, usafiri na gharama za matibabu unakuta anatumia gharama kubwa,” alisema

Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN), Kokushubira Kairuki akiteta jambo na mmoja wa madaktari waliohudhuria mafunzo hayo

Mkurugenzi wa Hospitali ya Kairuki, Dk. Asser Mchomvu alisema kuanzishwa kwa huduma za IVF kutasaidia kwa kiwango kikubwa kurejesha tabasamu kwa wanandoa  ambao walishakata tamaa ya kupata watoto.

Dk. Mchomvu alisema zamani watu walikuwa wakiamini kwamba masuala tatizo la uzazi ni ya wanawake pekee lakini siku hizi wanaume wameanza kupata uelewa na wengi wamekuwa wakiambatana na wake zao kwenda hospitalini kutafuta suluhisho la matatizo hayo.

“Kuingia kwa teknolojia hii kutasababisha tabasamu kwa wanandoa ambao walikosa mtoto kwa muda mrefu na tunashukuru kwamba tunatimiza maono ya hayati Profesa Hubert Kairuki aliyefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya afya na ndiye aliyeshauri serikali iruhusu kwatu binafsi waanzishe hospitali,” alisema Dk. Mchomvu

By Jamhuri