Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kuchakata data za hali ya hewa duniani Dkt.Hamza Kabelwa (Tanzania) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kamati hiyo, unaofanyika Arusha, Tanzania, tarehe 20-24 Machi 2023.

Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Kamati ya Kuchakata Data za Hali ya Hewa Duniani, lengo ikiwa ni kuhakikisha data za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na taasisi za hali ya hewa katika nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kwa manufaa ya sekta mbalimbali. Mkutano huo unaojumuisha wajumbe kutoka nchi kumi na mbili (12).

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa nchi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa, amesema “kwanza ni kutangaza utalii wa nchi yetu ambapo wageni hawa watakuwa mabalozi wa vivutio vya Tanzania katika nchi zao, aidha, kutokana na changamoto kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, upatikanaji data sahihi za hali ya hewa ni muhmu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania katika kusaidia kukabiliana na mabadiliko hayo ili kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”.

Mwenyekiti wa Kamati ya kuchakata data za hali ya hewa duniani Dkt.David Richardson (Uingereza) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamati hiyo, unaofanyika Arusha, Tanzania, tarehe 20-24 Machi 2023.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. David Richardson, alisema Kamati anayoisimamia itajikita katika kusaidia kujenga uwezo na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wote ili kulinda maisha ya watu na mali zao.

Kwa upande wake, Dkt. Anthony Rea, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu WMO alisema, majukumu ya kamati hiyo yanaenda sambamba na jitihada mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na WMO za kusaidia nchi katika kufanikisha upatikanaji wa data za uangazi za hali ya hewa ambazo zinazaa taarifa za hali ya hewa kwa matumizi ya nchi wanachama wa WMO.

Nchi zinazoshiriki mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuanzia tarehe 20 hadi 24 Machi, 2023 ni Australia, Brazil, Canada, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Korea ya Kusini, Japan, Afrika Kusini, Hispania, Uingereza na Marekani.

Wajumbe wa Kamati ya kuchakata data za hali ya hewa duniani wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa Kamati hiyo, unaofanyika Arusha, Tanzania, tarehe 20-24 Machi 2023
Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu kutoka Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt.Anthony Rea akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati hiyo, unaofanyika Arusha, Tanzania, tarehe 20-24 Machi 2023.

By Jamhuri