Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea

Kamati ya Mawaziri Wanane wa Kisekta inayoongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Jerry Silaa imeupongeza uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kufanikiwa kutatua migogoro 15 ya ardhi kwenye vijiji 38.

Slaa ametoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwa Mkoa wa Ruvuma iliyotolewa na Kamishina wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Said Juma Kijiji kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

“Kwa taarifa tulizonazo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imefanya kazi nzuri,Nawapongeza sana kwa kutatua migogoro 15 kwenye vijiji 38,hiki kilichofanyika ni upendo wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwamegea ardhi kutoka kwenye hifadhi na kuwapa wananchi waliovamia hifadhi, kwa taratibu za sheria mwananchi yeyote aliyevamia hifadhi alipaswa atoke kwenye hifadhi’’,alisema.

Amesema Kamati yake imefika mkoani Ruvuma kwa lengo la kutoa maazimio na maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwenye vijiji 975 vikiwemo vijiji kutoka Mkoa wa Ruvuma ambapo wananchi wanapata maelekezo ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambapo kazi ya kushughulikia migogoro ya ardhi imefanyika kwa mafanikio makubwa.

Amesema Rais Samia kwa huruma yake kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma amemega ardhi kutoka kwenye hifadhi ili wavamizi wa hifadhi waweze kumilikishwa na kufanya shughuli za kiuchumi.

Amewataka wananchi kuheshimu sheria za ardhi zilizopo ambapo amesema kuna vijiji vyenye matumizi bora ya ardhi ambavyo vimtenga maeneo ya malisho,makazi na kilimo ambapo amewaasa wananchi kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Waziri Slaa amemuagiza Kamishina wa Ardhi wa Mkoa na maafisa wote wa ardhi kwenye Halmashauri kuhakikisha wanasimamia sheria za ardhi ili kila mtu anatekeleza masharti ya matumizi ya ardhi na kuwaasa wananchi kuheshimu sheria ili kupunguza migogoro aya ardhi.

Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoani Ruvuma Said Juma Kijiji akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Kamati hiyo,amesema migogoro 15 ya ardhi iliyohusisha vijiji 38 mkoani Ruvuma imeshughulikiwa.

Hata hivyo amesema kati ya migogoro hiyo,migogoro 13 ilihusu uvamizi katika misitu ya hifadhi,mgogoro mmoja ulihusu fidia na mgogoro mmoja ulihusu uvamizi katika shamba la NAFCO.

Kuhusu mgogoro wa fidia eneo la uwekezaji(EPZA) Manispaa ya Songea,Kamishina huyo amesema wananchi 897 wamelipwa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 3.8.

Akizungumzia Shamba la NAFCO wilayani Namtumbo, Kamishina huyo amesema shamba la NAFCO lilikuwa na ukubwa wa hekta 5,763 ambapo wananchi wamemegewa na kupewa kiasi cha hekta 1,366.03 za ardhi.

Migogoro mingine ambayo imepatiwa ufumbuzi na Kamati ya Mawaziri wanane wa Kisekta ni uliokuwa mgogoro wa msitu wa Lihanje wilayani Songea na mgogoro wa eneo la ushoroba katika Kijiji cha Likusanguse wilayani Namtumbo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kikao hicho ameahidi kuendelea kusimamia sheria za ardhi ili kuzuia kuibuka kwa migogoro mipya ya ardhi hasa kuwadhibiti wafugaji holela ambao wamekuwa na tabia ya kuingia kwenye maeneo ya wakulima na kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Kamati ya Mawaziri wanane wa kisekta imemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Ruvuma kwa kumalizia kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo ya Lihanje wilayani Songea na Likusanguse wilayani Namtumbo.
Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya mawaziri wanane wa kisekta Mheshimiwa Jerry Slaa ambaye pia ni Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea

Kamati ya mawaziri wanane wa kisekta ilipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Ruvuma
Baadhi ya wadau wa wizara za kisekta wakiwa kwenye kikao na Kamati ya mawaziri wanane wa kisekta mjini Songea