Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)imesaini Mkataba wa upembuzi yakinifu wa ununuzi wa meli za uvuvi wa bahari kuu na ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata samaki Kilwa na Fungurefu utakaogharimu jumla ya Dola za kimarekani milioni 77.4 ambao utachukua muda wa miaka sita kukamilika kwake kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2027/2028 .

Hayo yameelezwa jana Jijini hapa na Mratibu wa Programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi nchini Salimu Mwinjaka kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba huo na kueleza kuwa kati ya fedha hizo, mkopo toka IFAD ni Dola za Marekani milioni 58.8,fedha za Serikali ni Dola za Marekani 7.8,Sekta binafsi Dola za Marekani milioni 8.5 na fedha za wananchi Dola za Marekani milioni 2.4.

“Lengo kuu la Programu hii ni kuwa na uzalishaji endelevu wa kibiashara na wenye kuzingatia mazingira hususani uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo ikiwemo mahindi, alizeti, maharage na mimea jamii ya kunde, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ukizingatia uwezeshaji wanawake na ushiriki wa vijana,”amesema

Amefafanua kuwa programu hiyo inatarajiwa kunufaisha watu takribani 1,3000,000 ikiwemo Kaya za wakulima wadogo 200,000 ambao watakuwa wanapata mbegu bora za mahindi, alizeti na maharage .

Aidha wazalishaji wadogo na kati wa mbegu na Wafanyabiasha wa pembejeo za kilimo takribani 1,000 watapata mbegu bora na mafunzo , wavuvi wadogo na Wafanyabiasha wa samaki takribani 48,000 na wafugaji wa samaki na viumbe maji na mwani 21,000.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa Programu hiyo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kupitia Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hizo ikiwa ni pamoja na TAFICO , ZAFICO, Wakala wa mbegu-ASA, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI na Taasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu-TOSCI.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dot. Jim Yonazi ameleeza kuwa programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi ni mpango wa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo Serikali inakusudia kununua meli nane kwa ajili ya Uvuvi wa bahari kuu kwa kujumuisha meli nne kwa ajili ya TAFICO na nyingine nne kwa ajili ya ZAFICO.

“Upembuzi yakinifu wa awali tayari umekamilika na kubainisha kuwa meli hizo za Uvuvi zitaleta tija kwenye Uchumi, kuleta mchango kwenye sekta ya Uvuvi katika pato la taifa ikiwa ni pamoja na kuboresha lishe na kipato kwa mwananchi mmoja mmoja, ” amesisitiza.

Dkt.Yonazi amesema,”Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi ni ya kimkakati hivyo Sisi kama Serikali tutahakikisha tunasimamia kwa ukaribu zoezi zima ili kuleta ufanisi unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zozote zitakazo jitokeza ili kuleta tija,hivyo, mkifanya kazi hii kwa weledi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa mtakuwa mmeshiriki katika kutafsiri maono ya Viongozi wetu wakuu, “amesema.

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuzipongeza kampuni za DMG na TANSHEQ ambazo ziliingia ubia na kushinda zabuni hiyo
na kwamba Mkataba huu utatekelezwa kwa muda za siku zisizozidi 45 kwa gharama ya Shilingi milioni 348, huku akiweka mategemeo zaidi ya kazi hiyo kufanyika kwa weledi na kumaliza kwa wakati.

By Jamhuri