Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini ( CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), wamezindua mipango ya ushiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Wazalishaji Tanzania 2024, Tanzania International Manufacturers Expo (TIMEXPO2024).

Maonesho hayo yamepangwa kufanyika kuanzia Septemba 26 hadi 29 mwaka huu katika viwanja vya Sabasaba Dar es Salaam ikiwa ni mara ya pili tangu CTI na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuingia makubaliano ya kufanya maonesho hayo.

Leodegar Tenga ambaye ni Mkurugenzi wa (CTI), ameeleza matumaini yake kwa maonesho ya mwaka huu, akisisitiza lengo lake la kukuza ushirikiano kati ya wazalishaji wa ndani na wazalishaji wa kimataifa.

Akizungumzia kauli mbiu ya “Kujenga Daraja na kukutanisha wazalishaji wa ndani na Nje,” Tenga aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuinua uzalishaji wa ndani hadi kuwa na viwango vya kimataifa.

Fortunatus Mhambe ambaye ni Mkurgenzi wa Kukuza Biashara TANTRADE, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa (TANTRADE), alionesha umuhimu wa kuunganisha viwanda vya ndani na vya nje na kueleza jukumu la tukio hilo katika kurahisisha kubadilishana maarifa na maendeleo ya kiteknolojia, muhimu kwa kuweka viwanda vya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Pia Mhambe aliwahimiza wadau kushiriki kikamilifu, kwani zaidi ya makampuni 500 kutoka masoko ya ndani na kimataifa yanatarajiwa kushiriki kwa kuonyesha bidhaa na huduma zao.

Kwa upande wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) linatazama maonesho haya kama fursa muhimu kwa wajasiriamali na wabunifu wa ndani

Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Teknolojia na Viwanda ‘SIDO’ Mhandishi Kulumuna Benedicto alithibitisha nia ya SIDO kuwawezesha wazalishaji wa Kitanzania, hasa kwa kutoa njia za kujifunza na kufikia masoko ya nje.

Hata hivyo Ushiriki wa SIDO katika maendeleo ya teknolojia mbalimbali unathibitisha dhamira yao ya kukuza uzalishaji wa kitaifa na ukuaji wa kiuchumi.

Aidha Masoud Kipanya, Mkurugenzi wa Kaypee Motors, alisisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani na kutilia mkazo hoja ya Tanzania kubadilika kutoka kuwa wanunuzi wa bidhaa peke na kuanza kuwa wazalishaji zaidi, akiongeza kuwepo na ushirikiano na washirika wa kimataifa ili kuimarisha ujuzi wa viwanda, akisistiza zaidi katika umuhimu wa kutumia maarifa na rasilimali za nje kukuza viwanda vya ndani.

Huku Tanzania ikijiandaa kuandaa Maonyesho ya Kimataifa ya Wazalishaji 2024, hamu ni kubwa kwa mkusanyiko unaotarajiwa kusukuma ubunifu, ushirikiano na ukuaji katika tasnia ya viwanda nchini. Kwa wingi wa washiriki, mijadala yenye mafanikio, na fursa za mtandao, tukio hilo limepangwa kuonyesha uwezo wa Tanzania kama kitovu cha ubora wa kimataifa katika uzalishaji wa viwandani.

By Jamhuri