Kanuni mpya kusimamia ununuzi tiketi mtandao, zanukua.

Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema kuwa inaandaa Kanuni mahususi kwa ajili ya kusimamia ununuzi wa tiketi za abiria kwa njia ya mtandao ikiwa ni pamoja na kuweka masharti kwa watoa huduma wa mifumo ya Tiketi Mtandao.


Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habib Suluo ameyasema hayo leo jijini Dar Es Salaam katika Mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya habari ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya taasisi za Umma inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habib Suluo akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya habari


“Mabasi yote ya masafa marefu yameunganishwa na mfumo wa Tiketi Mtandao na kwa kiasi kikubwa mfumo huo umesaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli, lakini ili kuwa na usimamizi mzuri tunaanda Kanuni za kusimamia eneo hilo,” alisema CPA Suluo.


Pia, amesema kwamba mamlaka imeandaa mfumo tumizi wa LATRA unaopatikana ‘Play Store’ kwenye simu zote za Android ili kumwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini.

CPA Suluo ameongeza kwamba kwa sasa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaendelea kuboresha huduma za mfumo tumizi wa LATRA ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari.
Akizungumzia mapato ya LATRA, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2021/22, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.945 hadi Shilingi Bilioni 28.53 ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 2.58 sawa na ongezeko la 10%.


Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 28.53 hadi Shilingi Bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 5.64 sawa na ongezeko la 20%.


CPA Suluo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.95 hadi Shilingi Bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 8.22 sawa na ongezeko la 32%.

Kwa upande wa utoaji wa leseni kwa vyombo vya biashara CPA Suluo amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.