Katibu Mkuu TALGWU awapongeza wanachama kusimamia mipango miji

Na Zephania Kapaya, JamhuriMedia, Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), amewapongeza wanachama kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia ipasavyo suala la mipango miji, changamoto za ukuaji wa miji pamoja na kuchangia maendeleo endelevu katika Nchi yetu.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika Maadhimisho ya Siku ya Miji Duniani inayofanyika Oktoba 31 kila mwaka, Rashid M. Mtima amesema chama kinapenda kutoa ujumbe kwa Waajiri katika Serikali za Mitaa Nchini Mameya na Wakurugenzi kwamba haki za wafanyakazi ni haki ya Binadamu.

“Ieleweke kwamba haki za wafanyakazi ni sehemu muhimu ya ukuaji endelevu na jumuishi wa miji hapa nchini na mafanikio yote katika ukuaji wa miji yanachangiwa na utendaji kazi bora wa Wafanyakazi waliopo katika sekta hiyo” amesema Mtima.

Mtima ameongeza kuwa waajiri wana jukumu kubwa la kuhakikisha eneo la kazi linakuwa salama na bila manung’uniko kwa kulipa kipaumbele suala zima la haki ya wafanyakazi ili dhana ya ukuaji wa miji ipate kutimia kwa maendeleo ya Nchi na kuendelea kulijenga Taifa letu Tanzania.

Hata hivyo Mtima amesema siku ya Miji Duniani ( World Cities Day), ilianzishwa kimataifa kwa kuzingatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2014.

“Siku hii hutumika kama fursa ya kukuza nia ya jumuiya ya kimataifa katika ukuaji wa Miji Duniani, kusukuma mbele ushirikiano kati ya Nchi katika kushughulikia changamoto za ukuaji wa Miji na kuchangia maendeleo endelevu ya Miji Duniani kote” amesema Mtima.

Eidha amefafanua kuwa TALGWU ni chama kinachotetea haki na maslai ya Wafanyakazi ambao ndio watekelezaji wakuu wa jukumu la kila siku katika Miji hapa Nchini tunaungana na shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vinavyotoa huduma kwa Umma (PSI), kwa kuazimisha siku hii muhimu yenye kauli mbiu inayosema haki za wafanyakazi ni haki za Binadamu.