Na Mwamvua Mwinyi, Jamhurimedia, Mkuranga

Tatizo la hali ya lishe kwa kundi la vijana balehe bado ni changamoto katika Mkoa wa Pwani ,licha ya mkoa huo kuwa wa kwanza kitaifa katika suala la lishe.

Aidha tafiti za malaria na lishe nchini zinaonyesha vijana balehe katika mkoa huo, upungufu wa damu ni asilimia 51.9 ,ukondefu asilimia 24, uzito uliozidi asilimia 4.6 hali ambayo ni changamoto kimkoa.

Akizindua kampeni ya lishe kwa vijana balehe yenye kauli mbiu ,Lishe Bora Kwa Vijana Balehe, Chachu ya mafanikio yao, wakati wa siku ya lishe Kitaifa iliyofanyika viwanja vya shule ya msingi Kiguza, Mkuranga Mkoani Pwani, kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowelle ameeleza, Serikali na wadau wa lishe wameendelea kuboresha na kuimarisha suala la lishe.

Ameeleza ,hali hiyo inashabihiana na tafiti za kitaifa za maralia na masuala ya lishe ,utafiti ambao umefanyika mwaka 2019.

Ilieleza, kundi la vijana balehe linakabiliwa na changamoto nyingi katika hatua ya ukuaji wao ikiwemo upungufu wa damu,madini na upungufu wa vitamini.

“Matokeo ya tafiti yanaonyesha kuwa asilimia 5.1 wenye unene uliozidi kundi la miaka 5-9 ndio liliongoza kwa asilimia 6.6, asilimia 11.2 wana ukosefu, asilimia 34.2 walikuwa na upungufu wa wekundu wa damu ambapo kundi la wanafunzi 15-19 liliongoza, huku asilimia 42 wana kiwango cha chini cha tabia bwete” amesema.

Taarifa hiyo ya Ummy ilieleza, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa lishe, wanaweka msukumo katika kusimamia kuandaa sera,miongozo na mikakati ya afya.

Pia kuandaa mpango jumuishi wa Kitaifa wa lishe namba II kwa mwaka 2012-2022, 2025-2026 pamoja na agenda ya kitaifa ya kuhakikisha hatua na kuwekeza kwa afya na ustawi wa vijana wa mwaka 2021-2022 na 2024-2025 ambapo lishe kwa vijana balehe imepewa kipaombele.

Vilevile iliongeza kuwa ,mpango wa kutekeleza mkataba wa lishe nchini ,msukumo ukiwa kwenye wanafunzi kula chakula shuleni na kulima bustani za mbogamboga .

Awali akitoa taarifa ya lishe mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ,Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanal Joseph Kolombo alisema, lishe kwa vijana balehe hali bado ni changamoto .

Amefafanua kwamba ,ni matumaini ya mkoa kuwa maadhimisho hayo yanakuwa ni chachu kuhakikisha suala la lishe kwa vijana linapewa kipaombele na kuleta matokeo chanya .

“Mkoa wetu umekuwa wa kwanza Kitaifa katika suala la lishe kijumla” tuna imani tutafanya vizuri na hili ,kwa kuendelea kulitilia mkazo “ameeleza Kolombo.

Mwanafunzi Sauda Misana na Esther George kutoka klabu ya lishe ,Shule ya Msingi Kiguza walieleza dhamira yao ya kuanzisha bustani ya mbogamboga ili kuimarisha afya zao .

“Itakuwa ni lishe kati ya vyakula tunavyokula ,ni lishe bora, pia ni sehemu ya elimu ya ujasiriamali kwani tunaweza kujiongezea kipato wakati wa mavuno” walisema.

Mwisho

By Jamhuri