Na Cresensia Kapinga,Songea.

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Dkt. Philis Nyimbi amewataka wazazi na walezi nchini kusimamia maadili mema ya malezi kwa watoto wao kwa kuwa hivi karibuni kumekuwepo kwa vitendo vilivyokithiri vya mmomonyoko wa maadili jambo ambalo linaweza kulitia doa nchi.

Hayo ameyasema jana kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Bombambili vilivyopo Kata ya Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakati wa hitimisho wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya UWT Taifa iliyoanza Julai 24 mwaka huu ikiongozwa na mwenyekiti wa UWT Taifa, Mery Chatanda ambapo katika ziara hiyo wametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.

Dkt.Nyimbi amesema kuwa sasa hivi kumekuwepo na mmomonyoko mkubwa wa kimaadili kwa vijana wa sasa jambo ambalo lina changiwa na wazazi hivyo ameitaka jamii kutokata tamaa kwenye kusimamia maadili ili nidhamu iweze kuimarika vyuoni,mashuleni na majumbani.

“Sasa hivi muna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili, niwaombe vijana wangu mnaonisikiliza leo hapa kuwa mabalozi wazuri kwa wenzenu,tuache kutembea nusu uchi kwa wasichana, wanaume kuvaa mlegezeo, tuwaambie hiki mnachokifanya sio sawa,wanataka kutuharibia kizazi ambacho sio chetu, hawa ndio watakuwa mawaziri wetu, wakuu wa mikoa, ndio wakuu wa Wilaya wa baadae” alisema Dkt. Nyimbi.

Katibu mkuu huyo wa UWT Taifa Dkt. Nyimbi ameitaka jamii nchini kuhakikisha inakemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani kuishi bila vitendo vya ukatili wa kijinsia inawezekana na lazima vitendo hivyo vitoweke katika jamii ya kitanzania na si vinginevyo.

Hata hivyo amesema katika ziara hiyo wamefurahishwa namna miradi ya maendeleo ilivyotekelezwa kwa viwango ikiwemo miundo mbinu ya elimu, maji, barabara pamoja na Afya na amempongeza mama Samia Hassan Suluhu rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo ili wananchi waendelee kunufaika.

Kwa upande wao wazee waasisi wamemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema ya kuboresha miundo mbinu lakini wamemuomba awasaidie kuwalipa pesheni zao kwa wakati wapo wanaopoteza maisha kwa kukosa mahitaji muhimu kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu, lakini pia falsafa ya wazee kwanza imekuwa ni changamoto kwao pindi wanapoenda kutibiwa wanaambiwa dawa hakuna wakanunue .

By Jamhuri