Watanzania hivi sasa wamo katika hekaheka ya kuwasikiliza wagombea urais, ubunge na udiwani wakinadi Ilani na sera za vyama vyao vya siasa na kuweka ahadi ya mambo watakayofanya pindi wapatapo ridhaa ya kuongoza nchi, kutoka kwa Watanzania.

Hekaheka hizo zinaendeshwa na kuonekana kwenye mikutano isiyo rasmi, ya faragha na ya hadhara huku wakijenga imani wagombea hao watapowachagua na kuwa viongozi wao, watawaletea maendeleo na kuwaondolea shida au matatizo waliyonayo sasa.

Dhana inayowakumba Watanzania katika pilikapika hizo ni mabadiliko. Mabadiliko yenye sura zaidi ya moja, kutokana na mitazamo mbalimbali ya makundi ya wazee, vijana, wataalamu, na viongozi wa siasa. Kila kundi lina jaribu kupiku kundi lingine na kutuweka akina tata kabwela katika mshangao!

Mathalani, wazee wanataka mwendelezo wa mabadiliko ya utamaduni wa Mwafrika ambao ndani yake imo elimu ya maisha na usalama wa nchi. Wataalamu na wasomi wanataka mabadiliko ya kiuchumi, unaotegemea rasilimali katika kuendeleza nchi yao.

Viongozi wa siasa wanataka mabadiliko ya kuondoa mfumo wa uongozi na utawala uliyopo ambao wanaamini ndiyo unaolea mafisadi na umaskini nchini. Vijana nao wanataka mabadiliko tu bila ya kufafanua ni mabadiliko ya aina gani, alimradi tu shida zao za kupata ajira na mlo mmoja kwa siku zinakufa.

Mitazamo hiyo ya makundi na kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayosema,”Watanzania wanataka mabadiliko” Zinakubaliana? Kwa maana makundi yametoa tafasiri thabiti ya kauli ya Mwalimu kwa Watanzania?

Hebu tuangalie pale Mwalimu Nyerere anaposema kuwa: “Watanzania wamechoka na rushwa. Nchi yetu ni maskini bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi maskini. Watu wameanza kuzungumzia udini, hatumpendi mtu kwa dini. Dini yake inatuhusu nini sisi. Watanzania wanaanza kuulizana makabila. Wanafikiri jambo la maana sana kujua kabila la mtu.”

Mwalimu Nyerere alitoa kauli hiyo mwaka 1995. Leo, imejenga umbo ambalo viongozi wa siasa wanajivuna na kudanda majukwaani wakizungumzia mabadiliko hata kama hawatoi tafsiri sahihi na kamilifu.

Lililo mbele yao ni mabadiliko tu huku wakiwaaminisha Watanzania hayo ndiyo  mabadiliko aliyoyasema Baba wa Taifa, Mwalimu  Nyerere! Jambo ambalo si kweli.

Kauli zinazotolewa hivi sasa kwenye mikutano ya kampeni zinajenga  umbo kwa miaka ijayo na Watanzania watatumia umbo la kauli hizo kuwachapa wagombea hawa endapo watapata uongozi na kutaka tena kuongoza. Ni busara kwa wagombea wa leo wanapotoa kauli zao, ndimi ziwe na saburi na kubakisha maneno ndani ya vifua vyao.

Nasema hivyo kwa sababu tayari baadhi ya wagombea na wapambe wao kwa miaka iliyopita walipokuwa viongozi waandamizi waliwahi kutoa kauli za kusifu utawala wa serikali na uwezo wa vyama vya siasa katika uongozi.

Kauli zile zimejenga umbo hivi sasa na viongozi hao sasa wanashindwa kutetea na kulinda kauli zao mbele ya umma wa watanzania.

Baadhi ya viongozi wakuu wa siasa nchini, miaka kadhaa iliyopita walitoa kauli za kuumbua na kuvunja heshima na utu wa mtu.

Waliosemwa kuonekana na kukubalika mbele ya umma hawana thamani. Leo, waliotoa kashfa na kuibua uchafu wa wenzao wanashindwa kutetea wala kulinda kauli zao kwa sababu ya umbo liliyopo.

Kauli zinazotolewa na baadhi ya wanachama wapenzi, au mashabiki kwenye vijiwe, mitaani na mikutanoni kuhusu chama fulani au mgombea fulani hafai zinajenga umbo baada ya kipindi cha kampeni na uchaguzi kupita. Watoa kauli wakati huo ujao hawataweza kufumbua vinywa vyao pale wataposhindwa

Baadhi ya viongozi wa dini hawana haya wala woga kusimama mbele ya hadhara iwe ndani ya nyumba za ibada au mikutanoni kutoa kauli zenye kuchochea chuki na dharau kwa watu. Kesho kauli hiyo itajenga umbo ambalo kwao na hata kwa waumini wao kubutwaa pale amani itapotoweka.

Ni busara Watanzania tukakumbuka kauli zilizowahi kutolewa na viongozi wetu waliojaa hekima, busara, upendo na adili katika miaka ya mwanzoni ya kupata uhuru wetu wa nchi. Kauli zao zilijikita  kwe.yeutu, haki, upendo na amani.

Kwa miaka mingi kauli zao zimejenga umbo lenye umoja, upendo na utulivu baina ya mtu na mtu mtoto kwa mkubwa, kijana kwa mzee, na wala haikuacha mwanaume kwa mwanamke.

Umbo hilo limekwenda mbali kwa kuthamini mlemavu na asiyemlemavu na kuweka pomoja waumini wa dini mbalimbali wakiwa ndugu na marafiki.

Leo wanapotokea viongozi na kauli zao za kutaka kuondoa sifa hizo za amani na kulielekeza taifa kwenye chuki na uhasama; vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ni dalili ya kuunda umbo la kuligawa taifa na kuliweka katika mapande mapande ya maeneo.

Watanzania na kila mzalendo kukataa kupokea kauli za chuki kwa nguvu zote zilizopo. Vyombo vya ulinzi na usalama kuacha ajizi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watoa kauli hizo. Vyombo vya habari kuacha ushabiki upendeleo katika kukumbatia kauli hatarishi. Hayo ndiyo yatakuwa mabadiliko.

Tukifanya hivyo tutaweza pasi na mashaka kuleta mabadiliko. Mabadiliko ya kukataa rushwa, kuondoa umaskini, kutoubeba udini na kuuzika ukabila. Kwa Tanzania iliyo huru inawezekana, tutimize wajibu wetu.

1503 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!