Kwanza nianze kwa kuwapongeza viongozi wote ambao mmekuwa mkishiriki katika dakika hizi za lala salama za uchaguzi mkuu ujao ambao utatuletea serikali mpya siku chache zijazo, nasema siku chache zijazo kwa maana ya Oktoba.

Katika mvutano huu kuna kila aina ya michezo michafu ambayo  inafanyika na wagombea wengi ili kuweza kushinda kushika madaraka ya dola ya nchi, washike dola ili wawe na mtaji wa kuweza kuwaeleza watanzania kuwa tulikuwa tukitarajia kufanya mambo ya maendeleo hata kama katika kampeni hatukuyaweka wazi, lakini cha msingi tayari wapo madarakani.

Tumeshuhudia vitimbwi vingi vya kisiasa na hata vile ambavyo havina sifa ya siasa ikiwa ni pamoja na matusi kwa maana ya kutamka na kuonyesha kwa vitendo, watu wamedhihakiana kwa masuala binafsi ya mtu ikiwamo kuombeana vifo, kutukanana kwa mambo ya kawaida kwa mahitaji ya binadamu na hata kusemeana mawazo ya zamani ya aliyokuwa nayo.

Katika kampeni kuna namna nyingi za ujanja wa kupata wanachama  na mashabiki, upo ujanja wa kuwarubuni wanachama wa vyama vingine kurudisha kadi za vyama vyao na kujiunga na chama chao, upo ujanja wakuwaleta watu maarufu ili kunogesha kampeni na kuwafanya wakubalike katika mikutano yao.

Lakini ninalopenda kulizungumzia leo ni hili la kusanyakusanya watu kwa ahadi ya fedha na usafiri ili wawezekufurika katika mikutano ya kampeni na kuwashawishi watu wengine kukubaliana na mgombea bila kuangalia sera za chama husika zinasema nini.

Hivi sasakuna kauli ambazo zinakinzana na watu wengi kwamba vyama vingi ambavyo vipo katika mchakato huu vina tabia ya kubeba washabiki wao mahali walipo na kuwapeleka katika mikutano mingine na kufanya idadi ya wasikilizaji kuwa wengi siku hadi siku, hii ina maanisha nini katika matokeo ya mwisho, inamaanisha watu kupiga kura kwa idadi ya watu walioshiriki katika mikutano.

Lengo kubwa la kuandika waraka huu ni kuitakia mema nchi yangu, hawa washabiki ambao wengi wao naamini siyo wanachama na wanaodiriki kusikiliza sera bali ni bendera fuata upepo kwa maana ya ushabiki tayari wameshajiwekea malengo ya ushindi, chochote kitakachotangazwa kwa kumtaja mshindi inaweza ikawa mwanzo wakutokubaliana na kile ambacho kimo katika imani yao.

Nina uzoefu wa kutosha katika suala la kuaminishwa, matatizo ya kuaminishwa yana athari kubwa kwa jamii ambayo ina mlengo wa kushoto kwa maana ya kwamba lolote liwalo na liwe, nchi yetu imekumbwa na ombwe kubwa la vijana ambao bila kuumauuma maneno naweza kutamka bayana kwamba hawana kazi na wana matarajio mengi makubwa.

Kundi hili ndio mtaji mkubwa wa wanasiasa ambao wanajua kabisa kwamba ndio wanaweza kuwaingiza katika madaraka, iwe kwa kura au iwe kwa maandamano, wanasiasa wamejua umuhimu wa ombwe hili na jinsi ya kulitumia, wanasiasa wametumia ujanja wa kisiasa kuweza kuwanunua kwa gharama nafuu wapiga kura hawa ambao kwa bahati mbaya wameshindwa kubaini kuwa baada ya kutangaza matokeo inaweza kuwa mwanzo wa vurugu za kisiasa. 

Kwa umri wangu na kwa uzoefu wa amani tuliyonayo nachelea kusema nina hofu kubwa na kundi hili la wanasiasa ambao kazi yao ni kucheza na mtaji wa vijana katika kuhakikisha wanayapata madaraka ambayo wanayatafuta usiku na mchana na kwa gharama yoyote iwe kuwasafirisha kushiriki kuleta hamasa katika mikutano yao au kujaza umati wa mikutano na kutoa utafiti wao kuwa tayari wameshika dola.

Ningelipenda sana wanasiasa wote wanadi sera zao na kuacha kufanya mbinu chafu za kuingia madarakani kwa kutumia mtaji wa wapiga kura na vijana ambao wengi tayari wameshakata tamaa ya maisha kutokana na kutojishughulisha na kazi wakiamini serikali ndio yenye wajibu wa kuwatafutia riziki yao ya kila siku, haya ndiyo madhara ya kufuta elimu ya kujitegemea na kuimarisha elimu ya kutegemea.Mwisho najua kuwa lazima mmoja ashinde, vyombo ambavyo vinasimamia zoezi hili vinatakiwa kutoa angalizo kwa wahusika ikiwa ni pamoja na wale ambao wanafanya utafiti usiokidhi mahitaji ya wasikilizaji na kuutangaza kama ni halali, kwa uzoefu wangu pia hakuna utafiti wa kipindi kifupi ambao utakupa usahihi wa majibu ya kweli na fasaha.

Naipenda sana nchi yangu lakini huu mtindo wa bebabeba ambao unafanywa na vyama vya siasa kujaza wasikilizaji naona kama ni mwanzo wa kuleta uvunjifu wa amani. Haya ni maoni yangu ila asiyesikia la mkuu na asubiri kuvunjika guu.

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1488 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!