Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ngorongoro

Kaya 77 zenye watu 463 na mifugo 1,408 waliohama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera wameagwa leo katika ofisi za mamlaka ya hifadhi hiyo.

Ofisa Uhifadhi Mkuu, Flora Assey ambaye ni meneja mradi wa kuhamisha wananchi wanaohama kwa hiari Ngorongoro amesema kufikia wiki hii jumla ya kaya 1,195 zenye watu 7,195 na mifugo 33,064 zimeshahama ndani ya hifadhi.

Amesema kati ya kaya 77 zilizohama ndani ya hifadhi wiki hii, kaya 75 zimeenda kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni na kaya mbili zimehamia kijiji cha Makao Meatu mkoani Simiyu.

Naibu Kamishna wa Hifadhi Huduma za Shirika la NCAA, Salum Mjema amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha zoezi la utoaji elimu, uandikishaji na uthaminishaji  kwa kuongeza timu ya uandikishaji ambapo ndani ya mwezi mmoja taratibu zote ikiwepo malipo zinakuwa zimekamilika na wananchi kuhamishwa bila kusiburi mda mrefu.

Mjema ameongeza kuwa ujenzi wa nyumba za makazi 2,500 Msomera unaendelea kwa kasi ambapo nyumba 903 zimeshakamilika, nyumba 97 zipo katika hatua za umaliziaji, nyumba 1500 zipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi huku maandalizi ya ujenzi wa nyumba zingine 2500 yakiendelea vijiji vya Kitwai, Wilani, Simanjiro na Saunyi Wilaya ya Kilindi.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo ametoa wito kwa jamii kupuuza baadhi ya watu wanaopotosha kuwa baadhi ya wananchi wanaohamishwa ndani ya hifadhi sio wakazi wa Ngorongoro na kusisitiza kuwa serikali iko macho katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Diwani wa kata ya Olbalbal ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro na katibu wa baraza la wafugaji Ngorongoro amesema ameamua kuhama baada ya kuona dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma bora za kijamii nje ya hifadhi

Please follow and like us:
Pin Share