Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Tanga

Mafunzo ya Usalama barabarani yanayotolewa na Amend Tanzania kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini kwa madereva bodaboda jijini Tanga sasa yanatarajiwa kutolewa katika wilaya zote za Mkoa wa Tanga ,lengo likiwa kuwafikia madereva wengi zaidi wa bodaboda.

Hayo yamesemwa na Ofisa Miradi wa Taasisi ya Amend Tanzania Ramadhan Nyanza wakati akizungumza katika kipindi cha redio maarifa jijini Tanga alipokuwa akizungumzia mafunzo yanayoendelea kutolewa na Taasisi hiyo kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi.

Amesema kuwa mafunzo hayo yanayotolewa na Amend yameanza katika Jiji la Tanga lakini mkakati uliopo ni kwenda katika Wilaya zote za mkoa huo ili kuhakikisha wengi wanafikiwa na hatimaye kumaliza changamoto za ajili barabarani ambazo nyingi zinazababishwa na madereva kutofuata sheria na alama za usalama barabarani.

“Mafunzo yanatolewa bure kwa madereva bodaboda,kwa hiyo tunatoa rai kwa wajitokeze kwa wingi ili wapate mafunzo yatakayowawezesha kuwa salama wawapo barabarani.

“Mafunzo haya yanatolewa tukifahamu wao ni madereva lakini kuwa dereva bila kutii sheria za usalama barabarani inamaana unakuwa mtu ambaye unaendesha chombo cha moto kwa kudhamiria kusababisha ajali,”amesema Nyanza.

Aidha amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa madereva bodaboda katika Wilaya zote Mkoa wa Tanga na lengo la kwenda katika Wilaya zote ni kuifikia jamii.Hivyo wanaomba bodaboda wajitokeze kwa wingi katika mafunzo hayo.

Ameongeza katika mradi huo mbali ya mafunzo yanayotolewa wanatarajia kufanya uboreshaji wa miundombinu salama katika Shule ya Msingi Azimio na Makorora ikiwa ni muendelezo wa miradi wanayoifanya ndani ya Jiji la Tanga ,lengo likiwa kuendelea kuwalinda wanafunzi wanapokuja na kuondoka shuleni.

Pia amesema wanaandaa kanuni za maadili ambazo wanashirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba watayajumuisha rasmi katika elimu ya usalama barabarani na kanuni hizo zitakuwa zinalenga kusaidia kupunguza ajali lakini kuwalinda aabiria

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani William Mwamasika amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa madereva bodaboda wa Mkoa huo na wanaushukuru Ubalozi wa Uswisi pamoja na Amend Tanzania kwa kuona umuhimu wa madereva bodaboda kupatiwa mafunzo hayo.

“Jeshi la Polisi Kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Tanga tunawashukuru Ubalozi wa Uswisi nchini kwa udhamini wa mafunzo haya na kuona kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye utoaji elimu ya usalama barabarani hasa katika kundi hili ambalo linaonekana kuwa hatarini zaidi.”

Pamoja na shukrani hizo, mkakati uliopo kwa sasa ni kuhakikisha mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda yanayotolewa katika Wilaya zote za Mkoa wa Tanga kwani kwa sasa yanafanyika katika Jiji la Tanga na tayari madereva bodaboda zaidi ya 200 wamefikiwa na lengo ni kuwafikia madereva 500.

Hivyo katika kufanikisha kampeni hiyo Kamanda Mwamasika amesema watakaa kikoa cha pamoja kuona ni maeneo yapi yafikiwe ili kuhakikisha vijana hao wa kundi la bodaboda wanapata mafunzo yatakayowawezesha kujilinda wao wenyewe na kulinda abiria wao lakini waachwe kuwa visababishi vya ajali barabarani.