Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ongezeko la dawa asili zinazodaiwa kuondoa changamoto za kike sehemu za siri, ikiwamo kupunguza majimaji, kulegea na kuongeza joto imebainika hazijasajiliwa, pia ni hatari kwa afya.

Baadhi ya dawa hizo ni vipipi, mbano na zingine mtumiaji anatumia kunywa kwenye kinywaji kama chai au kupaka sehemu za siri.

Wataalamu wa afya wanadai athari za matumizi ya dawa hizo ni kusababisha kupata magonjwa ya maambukizi sehemu za siri za kike (PID), fangasi, moyo na saratani ya shingo ya kizazi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwapo kwa wimbi kubwa la uuzaji holela wa dawa ya asili ya kuongeza ute kwa wanawake, kurekebisha maji ukeni na kubana kwa ulio legea jijini Dar es Salaam na kuongeza hamu ya tendo.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Mratibu wa Tiba Asilia kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Dar es Salam, Alana Ndomba, amesema wana jumla ya watalaamu wa tiba asilia na mbadala zaidi ya 600 na dawa za vipipi, mbano na nyingine za kupaka kwenye sehemu za siri hazimo katika orodha ya dawa zilizosajiliwa kisheria.

Amesema kama kitu hakikuthibitishwa ni hatari kwa matumizi na mtumiaji hajui madhara yatakayotokea mbeleni kiafya.

Amesema kwa sasa anafuatilia na watu wakipatwa na tatizo la kiafya kwenye maeneo yao ya siri wakafuate ushauri wa madaktari au kutumia dawa asilia na mbadala zilizopitishwa na serikali ili kuepuka wasipate madhara.

Kuhusu changamoto za uuzaji wa dawa holela na wataalamu kufanya kazi bila vibali alikiri kuwapo kwa kadhia hiyo kutokana na mazingira ya mkoa.

Kutokana na Dar es Salaam kuwa ni kitovu cha biashara, watu wasio waaminifu kwenye eneo la tiba asilia na mbadala wamekuwa wakiingia na kufanya kazi bila vibali lakini wanapambana nao kwa kuwapeleka mbele ya vyombo vya sheria na kuwalipisha faini.

“Unajua sheria ya tiba asilia iko wazi, mtu akikutwa na makosa atahukumiwa kifungo au faini ya Sh 200,000 au vyote viwili, inategemea amefanya kosa gani lakini huwa tunapendelea kwenye utoaji wa elimu,” amesema.

Kuhusu suala la wageni, amesema liko katika ngazi ya wizara na wao ndio wanajua wamesajili wangapi na wana taratibu zao za kisheria.

Amedai wamekuwa wakifanya ukaguzi kila robo mwaka na wakati mwingine kwa dharura pale wanapoona kuna uhitaji wa kufanya hivyo kutokana na watu wengi kukimbilia kufanya kazi bila vibali.

Kuhusu suala la uuzaji wa dawa holela hadi kwenye baadhi ya supamaketi zenye lugha isiyotambulika na wananchi ni kosa kisheria.

“Pia tunapokea wataalamu ambao ni waganga wa tiba asilia na mbadala kutoka mikoa mingine. Kuna utaratibu wa kisheria tunatoa vibali lakini watu wa nje nitapewa taarifa. Lakini kama unataka data za wageni tuliowakamata kwa kadhia ya kukiuka kwa haraka haraka sina idadi kamili ila wapo, nipe muda hadi nifuatilie baraza.

“Kwa sasa dawa zilizosajiliwa zipo na kama kuna ambazo hazijasajiliwa au zenye changamoto lazima tuzitoe kwenye soko. Tuna ukaguzi wa robo mwaka na kuna ukaguzi wa mara kwa mara. Mkakati wangu kwa mkoa hii tiba mbadala ni sahihi kwa watu wote wenye kuhitaji, kwa sababu ni hiari na ipo kisheria kama mkoa tumeanza huduma hiyo  Temeke,” amesema.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ben Kimaro, amesema dawa asilia wanazotumia wanawake katika kurekebisha changamoto za maumbile ya kike si salama kwa sababu athari watakazozipata ni kubwa.

Amesema kwa asili sehemu za siri za mwanamke zimeumbwa katika mlingano sahihi wa ‘alikali na asidi’ na kazi yake kubwa ni kuhakikisha sehemu za siri zinakuwa salama na ikitokea mtu anatumia dawa isiyo sahihi wanakwenda kubadilisha kitu kinachoitwa PH.

“Sasa ukitumia vitu sehemu za siri vinavyoweza kuharibu uwiano huo wa asidi na alikali unajiweka kwenye hatari ya uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa kama fangasi na saratani ya mlango wa kizazi,” amesema.

Ameshauri mwanamke yeyote mwenye changamoto katika maumbile yake aende kwa daktari kupata vipimo sahihi ili asichelewe kupata tiba na ushauri wa wataalamu.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Tiba Asilia na Mbadala kutoka Kituo cha Mbochi Herbal Life, Thobias Beda, amesema vipipi inayosemekana vinatibu changamoto za kike si vya kweli lakini ni watu wajanja tu wanawadanganya wanawake.

“Nasema si tiba kwa sababu ile dawa mimi naijua kwa ushahidi, kazi yake ni moja tu kuongeza joto, kwa hiyo wanaotumia wasifikirie watapona changamoto za kukosa ute, majimaji na kulegea, nashauri waende kuwaona wataalamu wa afya wajue shida, si kukimbilia vipipi.

“Kwa sasa wameibuka wanasambaza kienyeji bila kuangalia viwango na usalama wa package, kiafya si njema, kwa hili naishauri serikali kufuatilia kama hivyo vipipi na zingine vimekidhi viwango vinavyohitajika na je, wanajua vinaletwa nchini kwa kutumia kampuni gani ili visilete madhara? Kwa sababu mtandaoni utavikuta kibao vinauzwa holela kama njugu,” amesema.

Johari Habibu amesema alikuwa na tatizo la kukosa ute aliposikia habari za vipipi mtandaoni alikwenda kufuatilia na kununua kwa ajili ya kutumia ili awe vizuri kutoka na maelezo aliyosikia.

Johari amesema alitumia dawa ile ya vipipi hadi akamaliza lakini hakupona changamoto yake ya kukosa ute, ila kilichokuwapo alikuwa akipata hali ya kufanya tendo na alikuwa anapata maumivu bila mafanikio hadi alipokwenda hospitalini akapatiwa dawa.

Msemaji wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Gaudensia Simwanza, amesema dawa za vipipi na Reguratte Borother hazipo katika orodha ya usajili wa dawa, kwa sababu wao wanashughulika na dawa zenye fomula.

Please follow and like us:
Pin Share