Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita

Machi 18, 2024, shauri la rushwa na uhujumu uchumi Na. 7060/2024, lilifunguliwa mbele ya Atupye Benson Fungo ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbogwe dhidi ya Ambakisye Amani Mfwango ambaye ni mwalimu mkuu na Beatrice David Musiba ambaye ni Mwalimu wa kawaida
wote wa Shule ya Msingi Bukandwe.

Walimu hao walifikishwa mahakamani na Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mbogwe, ikiongozwa na Wakili wa Jamhuri Chali Kadeghe.

Washitakiwa wamefikishwa Mahakamani kwa mashtaka ya ubadhirifu wa mali za umma; kugushi nyaraka za vikao vya kamati ya shule ya Msingi Kanegere sambamba na kugushi hati ya malipo yenye thamani ya shilingi 1,500,000 kwa manufaa yao binafsi, jambo ambalo ni kinyume na vifungu vya 333, 335(d)&(i) na 337 vyote vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyorejewa Mwaka 2022.

Makosa haya pia ni kinyume na Vifungu vya 28(1) na 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2011, ikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza, vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 toleo la Mwaka 2022.

Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na shauri limehahirishwa hadi l Machi 28, 2024 litakapo kuja mahakamani hapo kwa ajili ya upande wa Jamhuri kusoma hoja za awali.

Washitakiwa walishindwa kutimiza mashariti ya dhamana na hivyo kubaki ndani ya mahabusu mpaka watakapo timiza mashariti hayo.

By Jamhuri