Ajenga zahanati ya kisasa, wananchi wafurahia

Na Ashrack Miraji, JamhuriMedia, Same

Wanakijiji wa Singa,kata ya Kibosho Mashariki mkoani Kilimanjaro wameonesha kufurahishwa kwa kujengewa zahanati na mdau wa maendeleo Joseph Mushi ambaye amechukua hatua ya kujenga zahanati ya kisasa kwa wanakijiji ili kusaidia kuoatikana kwa huduma za afya karibu.

Zahanati hii itakuwa na huduma bora za afya na itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi zaidi ya 4000 wa kijiji hicho. Kwa muda mrefu, wananchi wa kijiji hiki wamekabiliwa na tatizo la kukosa huduma za afya karibu na makazi yao.

Akizungumza na vyombo vya habari, mdau huyo amesema zahanati hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kijijini hapo kutokana na kwamba awali wakazi hao waliishi maisha ya wasiwasi kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya hasa nyakati za usiku.

“Kwa mapenzi yangu ya dhati nimeamua kujenga zahanati iwasaidie wananchi kijiji hiki na vijiji jirani vinavyoizunguka zahanati hii, tayari imekamilika asilimia zote tunatarajia kuifungua mwishoni mwa mwezi huu baada ya kukamilisha taratibu za kiserikali kupata vibali “alisema Mushi.

Ameongeza kuwa kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo, wanakijiji hao walikuwa wakienda kutibiwa Kibosho Hospital umbali wa zaidi ya kilomita tano lakini sasa wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Wakati huohuo baadhi ya wananchi waliofika kutembelea zahanati hiyo wamemshukuru mdau huyo kwamba zahanati iliyojengwa itaepusha vifo vilivyotokana na kuchelewa kupata huduma za afya.

“Kwa kweli zahanati hii itatusaidia sana,hivyo jukumu letu ni kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kizazi na kizazi kikute huduma hizi zikiendelea,” amesema David Masawe Mkazi wa Kijij hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji Cha Singa, Aloyce Chuwa amesema mdau huyo amekuwa msaada kwa wananchi kwamba awali wajawazito walipata shida ya kupata huduma, hali ambayo ilisababisha wengi wao kujifungulia njiani na wengine kupoteza watoto.

“Kutokana na huduma hii ambayo ameitoa katika kijiji chetu hatuna budi kumuunga mkono kwenye masuala ya maendeleo katika kijiji hiki maana amekuwa mtu wa watu niseme tu hii zahanati itakwenda kuwasaidia na vijiji vya jirani si tu kijiji cha Singa pekee” amesema Chuwa