Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kibaha

MKUU wa Wilaya ya Kibaha,Sara Msafiri, ameeleza wanatarajia kufanya matamasha na kutoa elimu ya umuhimu wa Zoezi la Sensa kupitia nyumba za ibada ili kuongeza wigo wa elimu ya sensa ndani ya jamii.

Vilevile, ameiasa jamii yenye watoto wenye ulemavu mbalimbali kuwatoa watoto wao kushiriki kuhesabiwa siku ya sensa pasipo kuwaficha ili kupata idadi kamili ya watu wenye makundi maalum ,baadae wapate kujulikana idadi Yao kamili na kupangiwa mipango ya kimaendeleo Kama ilivyo kwa wasio na ulemavu.

Sara alibainisha Mjini Kibaha ,kwamba watatumia pia viongozi wa dini na maeneo ya ibada ili japo dakika mbili zitumike kuwapa uelewa na kujua umuhimu wa zoezi hilo kwa waumini.

Aidha amesema mgawanyo wa rasilimali hauko sawa kutokana na kutokuwa na takwimu sahihi ya watu,hivyo zoezi hilo likifanikiwa kwa asilimia 100 litaleta tija kiwilaya,mkoa na Kitaifa .

Pamoja na hayo ,akiwa Mlandizi Sara alizungumza na viongozi wa madereva pikipiki (bodaboda, )viongozi wa soko na wausafirishaji wa daladala katika kikao chake cha kujadili namna ya kuhamasisha kushiriki sensa.

Amesema ili mgawanyo uende sawa na kila mmoja apate huduma stahiki ni vema wananchi washiriki kuhesabiwa ifikapo Agost 23 Serikali iweze kupeleka huduma inayoendana na idadi ya watu.

“Wilaya ya Kibaha ilikuwepo katika sensa ya majaribio ,itakuwa haipendezi tukashindwa kusimamia kikamilifu Zoezi la sensa linalokuja “ameeleza.

“Rais amewekeza kwenye anuani za makazi na sensa ya watu wananchi tutoe ushirikiano kwa maharani wa sensa, nimewaita nyie ili mnisaidie kuhamasisha na wataalamu wataendelea kutoa elimu kila mahali kuhusiana na umuhimu wa hili jambo” amefafanua Sara.

Hata hivyo,Sara amewataka wafugaji kuondokana na dhana ya kwamba mifugo ikihesabiwa inakufa badala yake waruhusu kuhesabiwa wao na mifugo yao ili dawa za mifugo ziweze kutolewa za kutosheleza idadi iliyopo.

Mkuu huyo wa Wilaya,amemuelekeza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Kibaha kuitisha kikao na wanawake ili waweze kupatiwa elimu ya sensa kwani wao ni watu wenye ushawishi kwenye jamii.

Kwa upande wake ,Mkufunzi wa sensa wa Halmashauri hiyo Gele Msangi ameataka wananchi kuzingatia kutoa taarifa sahihi kwa maharani wa sensa.

By Jamhuri