Kifo cha mwanamuziki nguli wa Kimarekeni Tina Turner chawaliza wengi

Mwanamziki nguli wa Kimarekani, Tina Turner aliyeutumbuiza ulimwengu kwa miongo mingi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83.nyumbani kwake Zurich Switzerland.

Turner ambaye alifahamika kama Malkia wa muziki wa Rock and Roll, alifariki jana nyumbani kwake karibu na mji wa Zurich nchini Uswisi baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliopata mafanikio makubwa sana wa muda wote. Miongoni mwa nyimbo zake zilizovuma ni “What’s Love Got to Do with It” na “Simply The Best.”

Salamu za rambirambi zinaendelea kutumwa kutoka kote ulimwenguni kutoka kwa wasanii, mashabiki na hata viongozi wa nchi akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden aliyesema kuwa Turner alikuwa na kipaji kilichobadilisha milele muziki wa Marekani.

“Juu ya kuwa na kipaji adimu kilicholeta mabadiliko ya kudumu katika muziki wa Marekani, Tina alikuwa ni mtu imara, aliyeshinda vikwazo chungu nzima, na manyanyaso, na kujenga fani itakayodumu kwa vizazi vingi na kuacha urithi ambao ni wake binafsi,” limesema tangazo la Rais Biden kuhusiana na kifo cha Tina Turner.

Tina Turner alijulikana kwa aina ya utumbuizaji wa sauti yenye nguvu jukwaani

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amemuelezea Tina Turner kama ”mtu aliyekuwa na nguvu isiyoweza kusimamishwa, aliyesema ukweli katika nyimbo zake, iwe katika machungu, katika ushindi na katika msiba.”

Salamu za rambirambi pia zimetolewa na nyota wa muziki wa miongoko tofauti duniani, kuanzia Mick Jagger, Mariah Carey hadi Beyoncé, wakimtaja kama malkia wa muziki wa Rock and Roll, na mtu aliyeacha alama isiyochuja katika fani ya muziki kwa ujumla.

Tina Turner alifahamika sana kwa aina ya utumbuizaji wake majukwaani, sauti yenye nguvu na mavazi ya kumeta.

Alizaliwa katika hospitali moja jimboni Tennessee ambako ubaguzi wa rangi ulikuwa umekita mizizi, jina lake la utotoni likiwa Anna Mae Bullock.

Nyota yake ilianza kung’ara akiwa muimbaji katika bendi ya Ike Turner, ambaye baadaye alimuoa, lakini ndoa yao ya miaka 20 ilikuwa na pandashuka zilizomuacha Tina Turner akiwa amevunjia kimwili, kiroho na kifedha.

Akiwa katika umri wa miaka 40 alianza kuyajenga maisha na muziki wake, na wakati nyota za watu wa rika lake zilipokuwa zikianza kufifia, yake ilizidi kung’ara, na aliendelea kuongoza kwenye chati za muziki kwa miaka mingi.

”Tunaweza vipi kusema buriani kwa mwanamke aliyeyakubali mauamivu yake na mifadhaiko, na kuvitumia kama nyenzo ya kuubadilisha ulimwengu?,” ni maneno ya Angela Bassett, mchezaji maarufu wa filamu nchini Marekani, aliyemuigiza Tina Turner katika filamu ya mwaka 1993 juu ya maisha yake iliyoitwa ”What’s love got to do with it.”

Mwanamuziki huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi kadhaa ikiwemo kufeli kwa Figo, ugonjwa na kiharusi (Stroke)
Alipata umaarufu katika miaka ya 1960 na nyimbo zake zikiwemo Proud Mary na River Deep, Mountain High.

Marehemu ameacha watoto wanne.