Na Isri Mohamed, JamhuriMedia

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinatarajia kushuka dimbani kuvaana na timu ya taifa ya Morocco kesho Januari 17, 2024 huko nchini Ivory Coast katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika { Afcon} majira ya saa mbili usiku.

Kwa mujibu wa ripoti ya Afisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo ni kwamba wachezaji wote waliosafiri na timu wakiongozwa na Nahodha, Mbwana Samatta wako timamu kiafya na kiakili na wanatarajia kufanya mazoezi ya mwisho leo usiku.

Licha ya timu ya Morocco kusheheni nyota wanaocheza kwenye vilabu vikubwa duniani kama, Sofyan Amrabat wa Manchester United, Achraf Hakimi wa PSG na wengine  wengi,  lakini falsafa ya mpira ni dakika 90 na lolote linaweza kutokea kama wachezaji wetu watajituma kwa kumwaga jasho kwa uchungu wa bendera ya nchi.

Serikali kwa upande wao wamefanya kila jitihada za kuhakikisha inawapa nguvu wachezaji wetu ili wafanye vizuri katika michuano hiyo ambayo kwa miaka mingi tumekuwa tukitolewa hatua za awali, ndio maana hamasa iliyofanyika mwaka huu ikiongozwa na waziri mkuu Kassim Majaliwa ni kubwa sana na wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Bilioni mbili zitakazoelekezwa kwa vijana ili kuwapa motisha.

Kilichobaki kwetu sisi watanzania ni kuiombea timu yetu na kuachana na dhana ya kuwa Stars ni kichwa cha mwendawazimu, zama zimebadilika tikijitoa kuisapoti timu yetu kama wanavyofanya mataifa mengine basi lazima tutafanya vizuri.

Dua tunayotakiwa kuomba ni Mungu aibariki Tanzania sio Afrika maana michuano hii inajumuisha timu zote za taifa zilizopo bara la Afrika, tusijichanganye kwenye dua.

Kila la Kheri Taifa Stars, huu ni wakati wetu wa kukataa unyonge, uwezo wa kuwatoa Morocco tunao, nyuma yenu kuna Watanzania zaidi ya Milioni 60 wanaowasapoti na kuwaombea ushindi.

By Jamhuri