Kilio cha elimu kwa watoto wa maskini

Desemba 20, 1956 Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais wa TANU, alihutubia Umoja wa Mataifa (Baraza la Udhamini) kwa mara ya pili. Alihutubia Umoja huo kwa mara ya kwanza Machi 7, 1955 akiwa mwalimu wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Francis, Pugu, nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam.

Mwalimu Nyerere hakuwa Mtanganyika wa kwanza kuhutubia Umoja wa Mataifa. Mtanganyika wa kwanza kuhutubia Umoja huo ni Japhet Kirilo aliyehutubia Julai 21, 1952. Alitumwa na chama chja Rais wa Meru (Meru Citizens Union) kwenda kudai warudishiwe ardhi waliyonyang’anywa na Serikali ya Mwingereza nchini Tanganyika. Madai hayo hayakufanikiwa.

 

Kwa upande wake, Mwalimu Nyerere alipohutubia Umoja wa Mataifa Desemba 20,1956 alidai mambo mengi ikiwa ni pamoja na elimu bora kwa watoto wa maskini.

 

Akitoa kilio cha elimu bora kwa watoto wa maskini, Mwalimu Nyerere alisema “Nchini Tanganyika elimu inatolewa kibaguzi. Watoto wote wa Kizungu na wa Kiasia wanakwenda shule ambapo ni asilimia 40 tu ya watoto wa Kiafrika wanaokwenda shule.”

 

Hicho kilikuwa kilio cha Mwalimu Nyerere kwa ajili ya elimu ya watoto wa maskini Tanganyika, alichotoa Umoja wa Mataifa mwaka 1956.

 

Mwalimu Nyerere angekwena leo Umoja wa Mataifa angeweza kutoa kilio kinachofanana na hicho kuhusu elimu ya watoto wa maskini. Angeweza kusema, “Nchini Tanzania elimu inatolewa kibaguzi. Kuna shule za watoto wa matajiri (shule za watu binafsi) zinazotoa elimu bora na shule za watoto wa maskini (shule za umma) zinatoa elimu duni.”

 

Shule za watoto wa maskini zinapewa elimu duni kabisa. Ukitaka sababu hatutachelewa kupata jibu. Sababu moja kubwa ni kwamba watoto wa mawaziri, wabunge na maofisa wa serikali wanasomeshwa shule za watu binafsi. Kwa hivyo hakuna anayejali watoto wa maskini wanapewa elimu ya namna gani.

 

Chukua, kwa mfano, suala la vitabu vibovu vya shule lilipofika bungeni ni mbunge mmoja tu aliyelivalia njuga, naye si mwingine bali ni James Mbatia. Ingekuwa suala hilo linahusu shule za watu binafsi wanakosoma watoto wa wabunge, bila shaka wabunge karibu wote wangeungana na Mbatia kudai vitabu bora kwa watoto wao.

 

Tukizungumzia vitabu vya shule izingatiwe kwamba Waziri wa Elimu alitamka bungeni kwamba vitabu vya fedha ya rada vingeanza kusambazwa shuleni tangu Septemba, mwaka huu, kumbe alikuwa analidanganya Bunge, maana tayari vitabu hivyo ambavyo havikufanyiwa masahihisho yoyote vimeshasambazwa katika Mkoa wa Dar es Salaam tangu Aprili!

 

Ukiuliza kulikuwa na haraka gani kuchapishwa vitabu hivyo upya na kusambazwa sasa wakati vingeweza kusahihishwa, kuchapishwa upya, na kusambazwa Novemba na Desemba tayari kwa mwaka mpya wa shule 2014 hutakosa jibu. Sababu ni kwamba wakubwa wa wizarani walitaka kuhakikisha wanapata asilimia 10 yao haraka kutoka kwa wachapishaji vitabu husika.

 

Katika mazingira hayo watoto wa maskini wataendelea kupewa elimu duni kutokana na kitendo cha wizara kuamua vitabu hivyo vibovu vichapishwe upya kwa fedha za rada bila kufanyiwa marekebisho.

 

Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulugo, anakubali kwamba vitabu hivyo vina makosa madogo lakini eti hayataleta madhara.  Kitabu cha kiada lazima kiwe na mambo sahihi kwa asilimia 100. Kuruhusu, kwa mfano, wanafunzi wafundishwe kuwa Tanzania ni muungano wa Tanganyika na Zimbwabwe ni kosa kubwa sana tena la aibu!

 

Kwa kuruhusu vitabu vibovu viingie shuleni Waziri wa Elimu amehujumu elimu ya watoto wa maskini. Ukimtaka ajiuzulu atakwambia kuwa ana baraka za Rais zinazomruhusu aendelee kuwa Waziri wa Elimu. Haiaminiki kwamba Rais anaweza kumpa baraka mtu anayeshika nafasi ya kwanza kwa kuvuruga elimu katika historia ya Tanzania! Angalia watoto wa maskini wanavyoendelea kuhujumiwa katika mitihani!

 

Muhtasari wa masomo ya darasa la saba ni mmoja kwa shule zote za msingi za umma na za watu binafsi. Tofauti ni lugha ya kufundishia na ya kufanyia mitihani – Kiswahili katika shule za uuma na Kiingereza shule za watu binafsi. Yanapotangazwa matokeo ya mitihani shule za watu binafsi zinafunika shule za umma.

 

Chukua, kwa mfano, mtihani wa darasa la saba wa ‘mock’ wa wilaya uliofanyika Kinondoni, Dar es Salaam, mwaka huu, nafasi ya kwanza mpaka ya 28 zilishikwa na shule za watu binafsi. Shule ya umma ya kwanza ilishika nafasi ya 29. Kwa kifupi shule za watoto wa maskini (za umma) zimeendelea kufanya vibaya katika mitihani.

 

Unapofanyika mtihani wa taifa wa darasa la saba ni wanafunzi wa shule za watu binafsi wanaoendelea kushika nafasi ya kwanza, kwa kuwa katika uteuzi wa wanafunzi wanaojiunga na shule za sekondari za umma wanafunzi wa shule za umma huchanganywa na wale wa shule za watu binafsi. Matokeo yake shule za sekondari za umma hujazwa na watoto wa matajiri na wa wakubwa kutoka shule za watu binafsi.  Katika mazingira hayo baada ya mtihani wa taifa wa darasa la saba watoto wengi wa maskini hurudi nyumbani kushinda vijiweni.

 

Hali hii inatokana na ukweli kwamba watoto wa maskini hawafundishwi vizuri katika shule za umma. Ukweli ni kwamba walimu wa shule za umma wamekata tamaa kutokana na kutotimiziwa madai yao. Kwa hivyo wanafanya mambo mawili.

 

Kwanza, wengi (na kwa kweli karibu wote) hawaandai mazoezi na mitihani inayoendana na silabasi. Badala yake wanaagiza nje ya shule mazoezi na mitihani isiyoendana na silabasi, huku walimu wa shule za watu binafsi wakitunga wenyewe mitihani na mazoezi yanayoendana na silabasi.

 

Pili, walimu wengi wanaishi kwa fedha ya tuisheni (masomo ya ziada) ambapo wazazi wa watoto hawa maskini wanalazimika kulipia kila siku wakiamini kwamba kwa njia hiyo watoto wao watapata elimu bora. Ukweli ni kwamba tuisheni hizi haziwasaidii watoto wa maskini kufanya vizuri katika masomo yao.

 

Tazama, watoto wa maskini wanatakiwa wawahi shuleni saa 12.00 asubuhi na wanaruhusiwa kurudi nyumbani saa 12.00 jioni, lakini bado shule za watu binafsi ambazo nyingi huanza masomo saa 2.00 asubuhi na kumaliza saa 8.00 mchana zinaendelea kufanya vizuri zaidi.

 

Kinachotakiwa sasa ni Serikali kuwalipa vizuri walimu wa shule za umma ili kuwapunguzia wazazi maskini mzigo wa kutafuta fedha ya tuisheni kila siku, na wakati huohuo kuhakikisha kwamba walimu wenyewe wanatunga mazoezi na mitihani badala ya hii inayoendelea kuingizwa shuleni kibiashara.

 

Hicho ndicho kilio changu cha elimu bora kwa watoto wa maskini.