DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Rafiki yangu Abdi Banda amerudi nchini kujiunga na Mtibwa Sugar. Sijui nini kimemtoa Afrika Kusini na kumrudisha nyumbani. Ninahisi kuna tatizo mahala. 

Muda ambao wachezaji wa mataifa mengine wanaikimbia ligi yetu kwenda ligi kubwa zaidi, ndio muda ambao mastaa wetu wa Kitanzania waliokuwa nje wanarudi kwa wingi. 

Nilitazamia kina Chama wapishane katika viwanja vya ndege na kina Nickson Kibabage, badala yake kina Kibabage wanapishana wenyewe kwa wenyewe pale Mbezi Mwisho, kituo kipya cha mabasi ya mikoani; Magufuli Bus Terminal.  

Kinachouma zaidi vijana wetu wengi waliorudi hawakujiunga na timu kama Azam FC, Simba wala Yanga, wamejiunga na timu za daraja la kati. Hii inaniumiza zaidi. 

Huko nyuma mara nyingi tuliona mchezaji wa Kitanzania akirudi nchini anakuwa bidhaa adimu kwa timu kubwa nchini. Kila timu inataka kumsajili, hivi sasa maisha yamebadilika.

Mastaa wetu wakirudi wanajikuta ni wachezaji wa timu za Namungo FC au Mbeya Kwanza. 

Vijiwe vya nyota hawa vimegeuka timu za kawaida. Hili suala linafikirisha. Tumekwama wapi kama taifa? Timu zetu kubwa zimo mikononi mwa wachezaji wageni?

Wazawa wachache ndio wana nguvu, uamuzi katika timu hizo, lakini wazawa wengi wanatazamwa kama wachezaji wanaosaidiwa kimaisha, si wao kuzisaidia timu.

Itazame Yanga ya msimu huu na ya msimu uliopita. Hakuna mchezaji wa Kitanzania aliyekuwa na nguvu mbele ya Mukoko Tomombe. 

Rudi kaitazame Azam. Mchezaji gani alikuwa juu ya Prince Dube? Dube alipoumia mwishoni mwa msimu na msimu wao ukaishia hapo! Hakukuwa na jambo jipya.

Watazame Simba. Angalau hawa wana namba kubwa ya wazawa wenye nguvu kushindanisha na wachezaji kutoka nje.

Shabalala, Kapombe, Manula, Bocco unaweza kusema ni majina makubwa mbele ya kina Chama na Miquessone walioondoka hadi hawa walioingia. Lakini bado haiondoi tatizo tulilonalo. Tunakwama wapi?

Kama ambavyo Wakongomani wameigeuza ligi yetu kijiwe chao, na sisi twendeni Congo tukapageuze kijiwe chetu. Lakini mastaa wengi wa Kitanzania wanaamini mastaa wa nje wanaotamba nchini wanakuzwa na kelele za ‘media’.