Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana amepokea malalamiko mbalimbali yakiwemo ya mauaji yanayotokea katika maeneo ya hifadhi wilayani Serengeti mkoani Mara ambapo ametumia nafasi hiyo kukemea na kusisitiza hakuna mwenye haki ya kukatisha uhai wa mwingine kwa namna yoyote.

Akizungumza jana mbele ya wanachama wa CCM wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa kikao cha ndani cha CCM, Kiana alielezea iko haja ya viongozi kuendelea kuwaelimisha wananchi kuheshimu mipaka iliyopo.

“Mkuu wa wilaya ya Serengeti amelifafanua vizuri sana na huwezi kuulaumu upande mmoja peke yake, lakini tunawajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu kuheshimu mipaka lakini jambo moja la msingi hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mtu. Hata katika Katiba haki ya kwanza ni kuishi,” alisema.

Alifafanua kuwa serikali hairuhusu kundoewa maisha ya mwananchi yeyote na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wake ni kufuata sheria na sio kuua.

Hata hivyo, alisema katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo tayari serikali imeunda kamati ndogo ambayo itafika mkoani Mara kufanya tathimini na hatimaye kutatua changamoto hiyo.

Kinana aliamua kuelezea hayo baada ya baadhi ya wana CCM akiwemo Diwani wa Kata ya Machochwe Joseph Magete kueleza kuwa kumekuwepo na matukio ya kutatanisha pembezoni mwa hifadhi hiyo kwa watu kupotea, hivyo alimuomba Makamu Mwenyekiti kuangalia suala hilo kwa nini linatokea pembezoni mwa hifadhi.

Kuhusu kero ya mpaka kati ya wilaya ya Serengeti na Bunda Kinana alisema kabla ya kufika katika kikao hicho alipata nafasi ya kuzungumza na Kamati ya Siasa ya Wilaya na ameelezwa changamoto hiyo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 50.

“Nikajiuliza kwa nini liwepo wakati watu wa Bunda na Serengeti ni ndugu na kwa kuwa wazee wapo watatuongoza katika hili. Pia nitakwenda kushauriana na viongozi wa Mkoa wa Mara pamoja na viongozi wa kitaifa. Kwa mtazamo wangu hili jambo ni la kijamii si la kiserikali,” alisema.

Aliafafanua kuwa, kabla ya kutenganishwa Wilaya ya Bunda na Serengeti ilikuwa moja na kwamba katika kugawa unaweza kugawa watu, lakini huwezi kuwagawa ndugu.

“Katika hili wazee wakae watushauri na tatizo hili itabidi tuanze kutafuta namna nzuri ya kutatua kwani inaonekana njia tunayotumia sio nzuri maana haiwezekani kwa muda wote huu ishikandikane. Hivyo wilaya na mkoa wakae waone jinsi gani ya kutatua tatizo hili,” alisema.

Akizungumzia malalamiko ya barabara inayounganisha kipande cha Sanzati, Nata hadi Arusha yenye urefu wa kilometa 40, Kinana alisema amepokea kero hiyo na tayari amezungumza na Waziri wa Ujenzi Inocent Bashungwa na wamekubaliana hadi mwakani iwe imekamilika.

“Baada ya Bunge kumalizika Waziri wa Ujenzi atakuja hapa kwa ajili ya kusimamia barabara hii. Haiwezekani jambo hili tuwe tunajadili kila mwaka na kuahidi halafu isitekelezwe, hivyo nitasimamia kuhakikisha barabara inakamilika.

“Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri na ninyi ni mashahidi, shule zinajengwa, vituo vya afya, barabara na huduma nyingine kama miradi ya maji inaendelea hivyo hata barabara ambazo zimeahidiwa zitajengwa,”amesema Kinana.

Hata hivyo, alitumia nafasi hiyo kuelezea uharibifu wa miundombinu ya barabara ulitokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza kuwa serikali italazimika kutafuta fedha nyingi kukarabati miundombinu.

Akizungumza kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025, Kinana alitoa rai kwa viongozi na wana CCM kutobeba au kupandikiza wagombea.

Aliwakumbusha wana CCM wakiwemo wa Mkoa wa Mara kutenda haki katika uchaguzi huku akisisitiza kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila mtu na kukemea rushwa katika uchaguzi.

By Jamhuri