Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Komedi Juma Homera amefika mlima Kawetele uliopolomoka alfajiri ya leo na kusababisha kufukiwa kwa nyumba 20, ng’ombe wanne na kuharibika kwa miundombinu ya Shule ya Mary’s katika Mtaa wa Gombe Kata ya Itezi Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Akizungumza baada kuwasili eneo la tukio RC Homera amekanusha uvumi unaozagaa mtandaoni ukidai kuna maafa katika tukio hilo ambapo amesema zaidi ya hivyo vilivyotajwa aya ya kwanza hakuna madhara mengine Wala Maafa kama inavyoripotiwa na Baadhi ya Watu.

Aidha Homera ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya tathimini juu ya waathirika hasa wale wasio na malazi ya kulala wahakikishe wanapatiwa sehemu hizo wakati huu ambao Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha hali inakuwa mawa katika Maeneo hayo.

Pia amekiagiza kitengo cha ardhi Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuacha kuwapimia wananchi viwanja eneo lenye changamoto hasa ya mkondo wa maji kwa kufanya kwao hivyo kutasababisha matatizo kama hayo ambayo yangeweza kuzuilika.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya kuamkia leo ambapo chanzo chake ni mvua zinazoendelea kunyesha mfululizo na matukio yanayofanana na haya yamekuwa yakitukia mikoa mbalimbali ikiwemo mikoa ya Arusha na Lindi.