Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nyanja zote za maendeleo, kisiasa, Uchumi, utamaduni na huduma za jamii yameipatia nchi heshima kubwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi wakati wa uzinduzi wa Sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema, kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano huo, Tanzania imeendelea kubaki kwenye historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote kutokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano viliyoasisiwa na viongozi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano huo.

“Tunaposherekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tuna wajibu wa nkujipongeza kwa mafanikio makubwa nchi yetu iliyoyafikia kwenye nyanja zote za maendeleo kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii amesifu Dk. Mwinyi.
Alieleza dhamira ya dhati kwa viongozi mbalimbali walioshika nyadhifa za uongozi kwa awamu tofauti kwa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza maono ya Waasisi wa Taifa hili kumefanikisha kudumisha na kuimarisha Muungano huo.

“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo umeongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu” amesifu Rais Dk. Mwinyi.

Akizungumzia changamoto za Muungano, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote za Muungano huo, ikiwemo kuunda Tume na Kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja za Muungano.

Amesema, miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.

Amesema tangu mwaka huo hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa, kati ya hoja hizo alieleza hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Aidha, hoja zilizobaki Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa zipo kwenye hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.

By Jamhuri