Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mfanyabiashara kinara wa mtandao wa kuuza dawa za kulevya aina ya Cocaine nchini amekamatwa na jumla ya gramu 692.336 za dawa hizo zinazohusisha watuhumiwa wengine wanne katika oparesheni maalumu zinazoendelea nchini.

Hayo yameelezwa leo Januari 25 , 2024, jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema Mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Mtanzania alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu tangu mwaka 2000 na alikamatwa katika eneo la Boko Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam pamoja na washirika wake watatu ambapo kati yao wawili waliokamatwa Jijini Dar es salaam na mmoja alikamatwa katika cha Shamwengo Wilaya Mbeya mkoani Mbeya.

Kamshina huyo Jenerali amesema mfanyabiashara huyo kwa wiki ana uwezo wa kusafirisha watu 10 (punda) kwaajili ya kupeleka dawa za kulevya maeneo mbalimbali dunia wanawake wanaongoza kwa kubebeshwa dawa hizo.

“Mfanyabiashara huyu wa mtandao wa Cocaine ambaye alikuwa anatafutwa mda mrefu kabla ofisi ya DCEA haijafunguliwa ni miaka 23 anatafutwa hivyo alikamatwa katika eneo la Boko Wilaya ya Kinondoni pamoja na washirika wake watatu,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema huwa wanazimeza zikiwa katika mfumo wa pipi ambapo kwa mara moja mtu hubega kuanzia grams 300 hadi 1,200 na wengine hadi gramu 2,000 kwa wakati mmoja

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa dawa ya kulevya aina ya cocaine ambayo huzalishwa kwa wingi katika Bara la Amerika Kusini husafirishwa kwa njia ya anga na wabebaji (punda).

“Mfanyabiashara aliyekamatwa ana mtandao mkubwa wa wabebaji(punda) kutoka nchi mbalimbali ambao huwatumia kusambaza dawa hizo kwa njia ya kumeza hivyo ya makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa na unaovuka mipaka,” amesema.

Aidha Kamshina Jenerali huyo pia ametangaza oparesheni kali ya dawa za kulevya 2024 ambayo itafanyika nchi kavu na baharini.

Vilevile amesema oparesheni hizo nchi kavu zitahusisha mashamba ya dawa za kulevya kwenye mipaka na maeneo ya mjini kwa upande wa bahari zitahusisha fukwe na katikati ya bahari ni oparesheni za wazi.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Lyimo aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wote wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya Ili kuhakikisha kuwa nchi inaendeleza kuwa salama .

Mwisho

By Jamhuri