· Wengi washangazwa, wasema ni mchapakazi hodari anayejua kazi yake

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, ¹Zanzibar

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Simai Mohamed Said, ametangaza kujiuzulu kwa kile alichokisema, mazingira tatanishi ya kazi na yasiyo rafiki.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Simai ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Tunguu kwa tiketi ya CCM, alisema amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Dk. Mwinyi kutokana na mazingira magumu kwake kwenye kutekeleza majukumu yake.

Ingawa hakutaja sababu za kujiuzulu, lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema ni kuchukizwa na kuchoshwa kwake na kuingiliwa mara kwa mara kwenye majukumu yake ya kila siku na watu waliokaribu na Ofisi ya Rais Zanzibar.

Imeelezwa kuwa sababu nyingine ni kuchukizwa na uamuzi wa Bodi ya Vileo Zanzibar kuzinyanga’anya leseni kampuni tatu za kusambaza vileo na kuzipa kampuni zingine za nje ya Zanzibar kuagiza vileo ambazo hazina uwezo hali ambayo imesababisha upungufu mkubwa wa vileo visiwani humo.

“Ndugu wananchi napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia barua mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar ya kujiuzulu nafasi yangu kama Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale kuanzia leo (jana)’’ alisema Simai na kuongeza‘’Nimefikia uamuzi huu ambao hapa kwetu si rahisi katika utamaduni wetu.

Alisema kutokana na imani yake kwamba jukumu namba moja la wasaidizi wa Rais wakiwemo Mawaziri ni kumsaidia kutekeleza Ilani ya chama na inapotokea mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa wananchi, ni vyema kutafuta jawabu kwa haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea na ikibidi kukaa pembeni.

Alisema kuwa siyo vyema sekta ya utalii ikachezewa kwani ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa pamoja kutoa ajira kwa vijana wengi wa Zanzibar.

Simai alimshukuru Rais Mwinyi kwa kumuamini katika nafasi mbali mbali za uwaziri kwenye serikali yake tangu alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita.

‘’Namshukuru sana Rais Dk Hussein Mwinyi kwa kuniamini kwa kuniteua kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali na hatimaye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale. Nitaendelea kuwa mtiifu kwa serikali pamoja na chama changu, Chama cha Mapinduzi,’’ alisema.

Kujiuzulu kwa waziri huyo wa Utalii wa Zanzibar kunakuja wakati ambapo kuna taarifa za mpasuko katika serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

Chama cha ACT Wazalendo kimekuwa kikilalamika kuwa kuna kukiukwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Dr Hussein Mwinyi na Marehemu Maalim Seif Sharrif Hamad ya kuundwa kwa serikali hiyo.

Mmoja wa wakazi wa Unguja, Salum Hamza Sultani alisema ameshangazwa sana na hatua ya Waziri huyo kijuuzulu kwani ni miongoni mwa mawaziri wachapakazi na ambao hawana kashfa yoyote ya ufisadi.

“Binafsi nimepata mshtuko kusikia amejiuzulu kwasababu Simai ni kijana mwadilifu sana na mchapakazi hodari na ambaye hana makuu, ni Waziri anayetambua majukumu yake sasa sijui kimetokea nini,” alisema

Mkazi mwingine wa Unguja, Issa Omari Usi, alipongeza hatua ya Waziri huyo kujiuzulu akisema kuwa inaonyesha ukomavu wake wa kisiasa na inaonyesha kwamba kwake kuwa Waziri ni kutoa huduma kwa wananchi na siyo kazi ya kujikimu kimaisha.