Kinywa cha Haji kinahitaji timu bora kiwanjani

NA MWANDISHI WETU 

Nchi ‘ilisimama’ kwa muda. Mitandao ya kijamii ilikuwa busy. Kila sehemu ni Haji Manara. Haji Manara. Haji Manara. Haji Manara. 

YES! Manara amehamia Yanga na wiki iliyopita jioni moja hivi alitambulishwa katika hoteli moja ya kifahali katikati ya jiji. Hii ni kama ndoto.

Mtu aliyewaweka Yanga roho juu na kuwanyima amani ya moyo muda mrefu, leo yuko upande wao. Hii ndiyo biashara ya soka.

Tumtarajie Haji wa namna gani na Yanga? Hili ndilo swali wanalojiuliza wengi. Uzuri Haji mwenyewe ameshasema alichokifanya Simba, ndicho atachofanya na Yanga. Pia akasisitiza huku atakuwa zaidi. 

Nyuma ya kinywa cha Haji pale Simba, kiwanjani Simba walikuwa na timu bora sana. Kazi yake ikawa nyepesi kama kukipaka siagi kipande cha mkate na kukipeleka kinywani.

Kina Chama, Mkude, Manula, waliirahisisha kazi yake kwa kiwango kikubwa. Mara nyingi alichokuwa anakisema katika Press ndicho kilichokuwa kinakwenda kutokea kiwanjani.

Mastaa wa Yanga watamrahisishia kazi? Ni swali gumu. Kuwa na Haji kisha ukawa na timu ya hovyo kiwanjani ni kazi bure.

Jikumbushe Haji aliyekuwa Simba kabla ya fedha za MO kuingia, huku Yanga wakiwa na Jerry Muro na fedha za Yusuph Manji. 

Haji kabla ya fedha za MO alikuwa mlalamikaji kila siku. Kuna siku alibeba hadi Tv kuja nayo kwenye Press kutuonyesha jinsi Simba wanavyominywa na waamuzi. Haji wa fedha za MO ni kiburi, halalamiki hovyo, jeuri na kinywa chake kimejaa kero. 

Lakini Yanga wamesajili mastaa wa maana msimu huu. Kama mastaa wale watatoa kitu kiwanjani, kinywa cha Haji hakitashikika.

Lakini kama mastaa wale watashindwa kutoa kitu kinywa chake kitapoteza mvuto. Ni kama kinywa cha Nugaz kilivyopoteza mvuto masikioni mwa wengi hivi sasa.

Nugaz alianza na mikogo kwa lugha tamu ya Kitanga. Alituvutia wengi. Lakini kiwanjani timu ikaanza kumuangusha pole pole. Baadaye akaja kuonekana wa kawaida. 

Alichokuwa anakizungumza Nugaz ni tofauti na tulichokuwa tunakwenda kukiona kiwanjani. Timu ilimuangusha sana. Mwisho kabisa, hakuna aliyekuwa anatega sikio lake kutaka kumsikiliza anazungumza kitu gani.

Manara peke yake hawezi kuwafikisha nchi ya ahadi Yanga. Ni lazima kuwepo na namba kubwa ya watu. Ni kama ambavyo Simba wamefanikiwa. Kila la heri Manara.