Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua uhalali wa vyama vingi vya siasa. Inasema, Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa

Kumekuwapo matukio ya Jeshi la Polisi kuzuia vyama vya siasa kuendesha siasa, kiasi cha baadhi ya watu kusema heri vifutwe. Tusichoheshimu ni kuwa unaweza kufuta vyama vya siasa lakini hauwezi kufuta fikra na misimamo ya upinzani (ukinzani) vichwani na nyoyoni mwa watu. Upinzani kwa wale wanaoamini uwepo wa Mungu, ni suala la asili. Haufutiki kamwe. 

Mtawala wa kwanza kumpata mpinzani ni Mungu. Shetani ametajwa kuwa ndiye mpinzani mkuu wa Mungu. Lakini Mungu alivyo wa huruma, amemwacha shetani aendelee kuwa hai. 

Hakuna wakati Mungu amediriki kumtoa uhai. Amemwacha pengine amsaidie kuona utii wa wanadamu kwake (Mungu) unakuwaje. Akimwondoa shetani yawezekana mambo yasiwe motomoto kama yalivyo sasa. 

Kinyume cha uvumilivu wa Mungu kwa mpinzani wake – shetani, wanadamu wamekosa uvumilivu. Kila leo zinatafutwa mbinu za kuua upinzani. Hata hivyo, tofauti moja tu ni kuwa hakuna siku chama cha shetani kitampiku Mungu, lakini chama kingine kuing’oa CCM ni ahadi ya agano. Itatimia tu. Ndiyo maana tunasisitiza suala la CCM na dola kuweka mazingira ya haki na usawa ili kuepuka visasi huko mbele ya safari.

Rais John Magufuli akiposhika madaraka mwaka 2015 alipiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa. Akaruhusu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiendelee kufaidi pepo. Hoja yake ikawa kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu, vyama vya siasa vitoe nafasi kwa chama kilichoshinda ili kitekeleze kwa ufanisi yale kilichowaahidi wananchi hata wakakipa ushindi.

Awali, alitoa ruhusa kwa wabunge kuendesha siasa katika majimbo yao. Wasivuke mipaka ya majimbo yao. Waliothubutu kuvuka walikiona cha moto. Baadaye ikawa kwamba wanasiasa wa hivyo vyama hawatakiwi kuendesha siasa, iwe nje au ndani ya majimbo yao. Huu ulikuwa ubabe uliovuka mipaka ya kikatiba.

Ni katika kipindi hicho tuliona wimbi la wapinzani kuhamia CCM. Ni mtu dhaifu tu wa kufikiri anayeamini kuwa uhamaji ule ulikuwa wa kuunga mkono juhudi. Ukweli ni kuwa waliokosa kupumua kisiasa na kimaisha, waliona heri warejee CCM kupata fursa za kiuchumi na kimadaraka. 

Wapo walioomba, lakini wapo pia waliorubuniwa. Huko tuendako kuna siku watu jasiri wataandika juu ya ‘kuunga mkono juhudi’ kama miongoni mwa rushwa mbaya kuwahi kutokea nchini.

Kabla na baada ya hapo tukashuhudia watu ambao kimsingi ni wapinga CCM wakipewa nafasi kubwa kubwa ndani ya chama na hatimaye kuendesha uchaguzi wa kiimla uliohakikisha wapinzani wanakabwa koo na kuambulia majimbo manane  tu kati ya majimbo 264 nchini kote. 

Matokeo ya dhuluma hii ya kufifisha mawazo tunayaona kwenye uamuzi mbaya wa baadhi ya mambo bungeni. Tozo za miamala ya simu ni ‘case study’ nzuri ya aina ya Bunge lenye uhaba wa mawazo makini.

Baada ya Rais Magufuli kuondoka, matarajio ya wanasiasa wa vyama tofauti na CCM yakawa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan angewapa fursa ya kuendesha siasa kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Walidhani watapumua. Walioota ndoto hizo walijidanganya. Mambo yameendelea kuwa magumu kwa upande wa upinzani.

Mimi ni mwanachama hai wa CCM. Mapenzi yangu kwa CCM hayahojiwi, maana yanajulikana kwa miongo minne. Hata hivyo, kwangu Tanzania ni zaidi ya chama chochote cha siasa. Nayasema haya kwa sababu mbadala wa CCM kama si kesho, basi keshokutwa utapatikana; lakini mbadala wa Tanzania haupo. Tuna sababu zote kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye watu wanaosikilizana.

Kuna mambo yanayohitaji baadhi ya Watanzania vichaa wasimame wayaseme wazi kwa lengo jema kabisa la kuhakikisha Tanzania yetu inaendelea kuwa salama. Kushangilia mateso wanayopata watu wa vyama vya upinzani si chanjo ya kutuepusha na kisasi kijacho. Polisi wasikubali kutumika kujenga nchi ya watu wanaochukiana.

Kwa siku za karibuni wafuasi, wanachama na viongozi wa vyama vya siasa wamezuiwa kushiriki mikutano ya hadhara na hata ya ndani. Jeshi la Polisi likitambua wazi kuwa halina mamlaka ya kuzuia mikutano inayofuata taratibu za kisheria, lakini limekuwa la kibabe. Miongoni mwa sababu zinazotumiwa na polisi muda wote ni kuwa ‘taarifa za intelejensia’ zinaonyesha kuwapo kwa hatari. Baada ya hekaya hizo kuzoeleka, sasa ugonjwa wa UVIKO-19 ndio umekuwa ngao ya kuzuia mikutano hiyo.

Kichwa kisichohoji mambo ni kichwa mfu. Mtu mwenye akili timamu anapoona chama ‘A’ kinazuiwa wanachama wake 50 kukutana kwa sababu ya UVIKO-19, na wakati huo huo akaona chama ‘B’ kinaruhusiwa wanachama wake 500 kukutana katika mazingira na hali ya hewa ile ile, lazima atahoji. 

Atahoji kwa nini huyu azuiwe, lakini yule aruhusiwe? Kichwa kisichoweza kuhoji jambo kama hili kina walakini. Haupaswi kuwa mfuasi wa chama cha upinzani kung’amua au kuhoji kuhusu huu upendeleo. 

Hata mwana CCM wa kweli na mcha Mungu, aliyefundishwa na kuikiri amri kuu (UPENDO) atahoji. Kuona hali hii na kukaa kimya tafsiri yake ni kuwa unabariki uonevu huo.

Polisi kuwazuia wapinzani kufanya siasa ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini hili si jambo la kuwatazama polisi pekee. 

Watu wanajiuliza, polisi wanatoa wapi nguvu za kuvunja haki za msingi za watu kukusanyika kwa kuheshimu misingi ya kisheria? Nani anawatuma kuvunja haki hiyo? Je, ni amri kutoka kwa wakuu wao? Je, ni amri kutoka kwa Rais? Kama si amri ya Rais, kwa nini hakemei uonevui huu? Kukaa kwake kimya kunatenganishwa vipi na haya yanayoendelea?

Kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka 2012, Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, alisema: “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli.” Waliomsikiliza akiyasema haya wapo, lakini kama ilivyo ada, waliyasikia na kuyaacha hapo hapo japo yataishi daima.

Tunapotosha kudhani kuna muda wa siasa na muda usio wa siasa. Siasa ni maisha ya kila siku. Ni maisha ya kila mtu kwa sababu taathira yake inamgusa kila mtu katika nchi. Nitajieni, nani haguswi na uamuzi mbaya au mzuri wa siasa na wanasiasa kila siku? 

Kama siasa ni kitu kinachotuhusu kila siku, iweje itengewe msimu wa miezi mitatu kila baada ya miaka mitano? Bahati mbaya waliozuiwa siasa hawaendi kudai haki hii mahakamani! Katiba ya nchi imesema Tanzania ni nchi yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Haikusema Tanzania ni nchi yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa vya msimu.

Tunao viongozi wakuu wastaafu wa kutosha. Haya mambo wanayaona kila leo kwenye vyombo vya habari. Wanayaona huko wanakoishi. Licha ya kuyaona na kuyasikia, wamechagua kukaa kimya kana kwamba kinachofanywa na dola ni cha maana. 

Wanajua wazi kinachoendelea ni ubaguzi. Athari za ubaguzi wanazijua vizuri sana. Mataifa mengi yaliyoingia kwenye migogoro, ubaguzi ni miongoni mwa vichocheo. Ukimya huu unatokana na nini? Woga? Wazee ni glisi. 

Kunapotokea mambo ya kuigawa jamii wazee wanao wajibu wa kuonya. Wazee si lazima wasimame majukwaani. Wana sehemu zao za kukutana. Huko huketi wenyewe na kujadili mambo kwa manufaa ya nchi. Humwita aliyeshika usukani na kumpa mawazo yao ambayo ni mawazo ya jamii.

Naomba nitoe hadhari: Hii double standard inayofanywa ya kuwabana wapinzani na kuwaachia CCM watambe kisiasa ina athari kwa umoja wetu kama nchi. Inajenga ubaguzi. Inajenga chuki. Inawapa mwanya watu waliojawa upepo vifuani kutafuta njia ya kuonyesha hisia zao. Hizo njia mara zote si nzuri.

Njia ya watu kuondokana na yanayowakwaza vifuani ni kuwapa nafasi ya kusema alimradi waseme kwa kulenga kwenye misingi ya kisheria. Wapewe nafasi ya kupumua. Waachwe wakutane maana ni haki yao. Mwangalie mtu aliyefiwa – huwezi kumnyamazisha kibabe. Anapolia, mpe nafasi alie awezavyo – baada ya muda atatulia.

Angalieni chuki iliyojengeka leo katika jamii yetu. Watu kwa sababu wanaamini polisi wanatumiwa na CCM, leo wakifikwa na mabaya watu wanashangilia! 

Polisi wanauawa halafu watu wanashangilia? Sisi kama nchi hatugutuki? Nani katutia upofu na ukiziwi? Mbona zamani zile msiba wa nchi ulikuwa ni wa watu wengi katika nchi? Leo nini kinatufanya tushangilie kwa sababu fulani kafa? Tusitafute mchawi. Turejee kwenye misingi ya mambo yaliyotufanya tukajiona na kuishi kama watoto wa tumbo moja.

Nimesema, na ninaomba nieleweke. Hata Mwalimu Nyerere zama zile za miaka ya 1950 alikuwa mpinzani. Ambao hawakutarajia siku moja watawala watakuwa wapinzani wa serikali, walijidanganya. Walikosa maono. Mtawala wa leo akiweka uwanja sawa wa ushindani wa kisiasa anakuwa amejiwekea akiba ya baadaye ya kutendewa haki. Tusiende mbali. Tuzirejee picha za video tuone jeuri, matusi na kejeli za Edgar Lungu miezi miwili iliyopita. Tumtazame HH wa leo. Watawala wetu na polisi hamuoni ya mwaka 2030, maana yako mbali, na hili la leo tu la Lungu na HH nalo hamlioni?

Haya yanayofanywa na polisi hayamsaidii Rais Samia na serikali. Hayaisaidii CCM. Tunaweza kujidanganya na kushangilia kuona wapinzani wanazimwa kwa maguvu ya dola. 

Tunaweza kutoa taarifa za kuwapongeza polisi kwa kusimamia ‘amani na utulivu’  hata kama ni kwa uonevu. Tunaweza kutafuta maneno ya kila aina alimradi tu kuhalalisha ubabe huu, lakini lililo wazi ni kuwa hakuna kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko tu. Heri yao walioamua kuyasema haya, maana wanaipenda Tanzania.

428 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!