Home Gazeti Letu Kipilimba katika mgogoro wa ardhi

Kipilimba katika mgogoro wa ardhi

by Jamhuri

Balozi Dk. Modestus Kipilimba yumo kwenye mgogoro wa ardhi na baadhi ya wakazi wa Msakuzi, Mbezi Luis, Dar es Salaam wanaodai amewapoka maeneo yao kwa kutumia nafasi aliyokuwa nayo.

Miongoni mwa wanaolalamika ni Rudolf Temba, ambaye amesema amedhulumiwa ekari 2.5 zilizomo ndani ya shamba namba 910 lililopo Mbezi Luis.

“Amechukua ekari hizo pamoja na nyumba ikiwa ndani yake. Amezungusha ukuta wakati kuna nyumba yangu na wapangaji, matofali na mali zangu nyingine,” anasema Temba.

Temba anasema Dk. Kipilimba amechukua eneo hilo kwa nguvu, na kwamba yeye na wananchi wengine wamekosa msaada kutokana na nafasi kubwa alizokuwa nazo serikalini.

“Tumepata nguvu baada ya Rais Magufuli kumwondoa, lakini kabla ya hapo tulishindwa na hata tuliogopa. Tulilalamika kwenye ngazi mbalimbali, tulishafika hata kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, lakini hakuna kilichofanyika. Kila tulipogusa na kueleza tunayepambana naye kila mmoja aliyetusikia aligeuka,” anasema.

Kwa upande wake, Dk. Kipilimba amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwa anamiliki ardhi katika eneo hilo.

Anasema eneo linalosemwa ni mali yake halali na ana hati zote zinazomhalalishia umiliki kisheria.

Naye, Rose Mkopi, ambaye ni mjane wa mzee Mkopi aliyekuwa mmiliki wa eneo hilo kabla ya kuliuza kwa kina Temba na wenzake, amesema hataki kuingia kwenye mazungumzo ya kina kuhusu mgogoro huu. “Nashindwa kujibu hilo suala kwa sababu kuna vitu vinataka ushahidi. Hii issue (jambo) ni nene, siwezi kulijibu kienyeji,” anasema.

Historia inaonyesha kuwa mwaka 1996 Dk. Kipilimba na mtu aliyeitwa Katawanya, waliuziwa ekari saba katika eneo hilo. Wakagawana kila mmoja ekari 3.5.

Miaka kadhaa baadaye, Katawanya alifariki dunia na eneo hilo likawa chini ya dada yake – Mama Katawanya. Mwaka 2016 Dk. Kipilimba na kijana wa marehemu Katawanya – Gerald Katawanya, walifika nyumbani kwa Temba wakiwa na watendaji wa Serikali ya Mtaa katika eneo hilo.

“Walifika wakiwa na mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Mama Janet Biseko. Walifika kwangu wakitaka kujua kama ninamtambua Dk. Modestus Kipilimba. Nikasema ninavyo vielelezo vya umiliki wa ardhi ya mtu anayeitwa Dk. Kipilimba nilivyoachiwa na marehemu mzee Duncan Mkopi.

“Basi, Dk. Kipilimba akajitambulisha kuwa ndiye yeye mwenye ardhi hiyo. Kwa kuwa mimi ndiye niliyekuwa nalijua vizuri eneo hili, wakanitaka niwapitishe waone mipaka ya eneo la Dk. Kipilimba. Nikawatembeza na tukakuta kuna watu wamejenga ndani ya eneo lake.

“Walipoulizwa wakasema wameuziwa na Mama Mkopi, na lile la Katawanya likawa limeuzwa na dada yake aliyekuwa ameachiwa. Eneo lililouzwa la Dk. Kipilimba aliyefanya hivyo ni Mama Mkopi na kwa kweli kukawa na mgogoro kati ya wawili hao. Hoja ikawa kwamba ameuzaje eneo bila kumshirikisha? Mimi nikawa shahidi kwa sababu naijua mipaka. Ikaamuliwa Mama Mkopi na waliovamia eneo wamlipe Dk. Kipilimba. Hapa ikumbukwe kuwa mimi ndiye niliyekuwa nimepewa power of attorney na mzee Mkopi ya kulipa deni alilokuwa nalo benki ili nikomboe hati moja ya shamba lote Na. 910.

“Mama Mkopi kwenye eneo ambalo alipewa na mumewe marehemu Mkopi, na ambalo halipo ndani ya eneo la shamba Na. 910; akauliza kwa watu 13 ambao tayari wakawa wameshajenga. Gerald Katawanya akaja na kudai kuwa hata hilo eneo ni lake, na kwa kweli alifanya hivyo kwa kumtegemea Dk. Kipilimba,” anasema Temba.

Kwa maelezo yake, Kipilimba ‘alivizia’ akiwa safarini akaenda kutwaa ardhi yake.

“Vilelezo vyote ninavyo, wakawa kila mmoja anaomba nimsaidie ajue mpaka wake. Sasa akasubiri nikiwa nimesafiri akaleta mafundi na askari – wakajenga ukuta chini ya usimamizi wa mitutu ya bunduki.

“Niliporejea na kumuuliza imekuwaje kavamia eneo langu, akasema tuyamalize na yuko tayari kulipa hilo eneo. Nilishajenga hapo nyumba kwa ajili ya mwanangu. Akaniuliza kama ninataka nilipwe fedha taslimu au niseme ninataka nini.

“Kwa wakati huo nilikuwa ninahitaji magari, kwa hiyo akasema niende Toyota Tanzania Limited ili kama ninataka magari anifidie kwa magari.

“Niende Toyota nikachague magari ninayotaka, kisha nimpelekee invoice (ankara) halafu atalipia nikachukue baada ya kufanya valuation (uthamini) na kupata thamani halisi ya ardhi ambayo ni kama Sh milioni 300.

“Nikachagua magari nikampelekea invoice, akaniambia anafanya utaratibu wa kuyalipia. Baada ya hapo kila siku akawa ananipiga kalenda. Ananiambia atapiga simu, wikiendi, mchana, kila mara anadai yuko bize – hadi leo hii ni stori tu.

“Sielewi kinachoendelea ingawa ninaona ukuta, lakini ameendeleza kwa kutumia madaraka yake. Amejenga kwa mabavu ya cheo na fedha,” anasema Temba.

Gazeti la JAMHURI limeziona ankara mbili kutoka Toyota Tanzania Limited za Februari 05, mwaka jana. Ankara ya kwanza ni ya gari aina ya Toyota Land Cruiser Pick-Up Single Cabin ya Sh 149,806,590; na nyingine ni Land Cruiser Station Wagon GXR ya Sh 251,744,000.14.

Temba amedai kuwa baada ya ‘kumsumbua’ mara kwa mara kuhusu haki yake, Dk. Kipilimba alimpelekea polisi wakamkamata.

“Walikuja askari kama wanamkamata jambazi. Nikapelekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam (Central).  Humo nilikaa kwa siku 15. Baada ya hapo walikuja kugundua ni migogoro ya ardhi, wakili wangu akaja nikaachiwa baada ya kujua ukweli.

Hakuna kesi iliyoendelea maana polisi waliona ninaonewa kwa sababu tu yule ni mkubwa.

Anasema alipotoka rumande aliendelea kuwasiliana naye kwa nia ya kumaliza mgogoro huo kistaarabu lakini hadi wiki iliyopita Dk. Kipilimba amekuwa hataki kupokea simu za Temba.

“Hataki mawasiliano na mimi, ame-block simu zangu. Amepiga ukuta na mpangaji amefukuzwa. Eneo lote lina hati moja kwa hiyo kila aliyeuziwa ilitumika hiyo moja.

“Nilikwenda Serikali za Mitaa Februari, mwaka jana nikaambiwa yuko tayari kumalizana na mimi, lakini haijulikani ni lini. Nikimtafuta mara zote ninaambiwa yuko bize, ninashindwa kabisa nifanye nini,” anasema.

Dk. Kipilimba amezungumza na JAMHURI na kusema: “Mwaka 1996 nilinunua shamba hilo eneo la Msakuzi kutoka kwa mzee Mkopi. Alikuwa na hati ya shamba na nilinunua mimi na Rudo [Rudolf]. Tuliandikisha kwa magistrate (hakimu). Nilikwenda kusoma, niliporudi nikakuta eneo langu limevamiwa. Ninakuhakikishia kuwa eneo lile ninalimiliki kihalali na hati zote ninazo.”

You may also like