MKURANGA

NA AZIZA NANGWA


Wakazi wa Kata ya Mipeko wilayani Mkuranga wameiomba serikali kusaidia ujenzi wa daraja linalounganisha eneo lao na vijiji vingine ili waweze kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii kwa unafuu.
Wamebainisha kuwa mvua zilizonyesha hivi karibuni zimesababisha kukatika kwa mawasiliano na Kijiji cha Mbande baada ya daraja lililokuwa linawaunganisha kuzolewa na maji.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao zaidi ya 9,000, Vailet Mosha, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amesema kero ya daraja hilo ni kubwa kiasi kwamba watoto wengi wanapata shida wakati wa kwenda shuleni.
Moshi amedai kuwa kuna baadhi ya watoto hawajaenda shuleni kwa zaidi ya wiki mbili sasa, kwani wanashindwa kuvuka mto ambao umefurika maji.
Mosha ameongeza kuwa kina mama ndio wanaoteseka sana kwa sababu mahitaji mengi yanapatikana katika kijiji jirani cha Mbande.
“Wanaume wanapohitaji kitu kutoka kijiji jirani wanaweza kupita kwenye mto uliofurika lakini wanawake wanalazimika kuzunguka mbali ili kufuata mahitaji. Hali ni mbaya sana,” anasema.
Anasema inashangaza kuwa baadhi ya viongozi wa serikali walikwisha kutembelea eneo hilo na kuona kilichotokea lakini hadi leo hakuna chochote kilichofanyika.
“Kuna wakati tulisikia kuwa serikali ilikuwa imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu lakini kazi ikafanyika chini ya kiwango na matokeo yake daraja lililojengwa limezolewa na maji,” anafafanua Mosha.
Mwanakijiji mwingine, Selemani Zomboko, anasema huduma za kijamii katika kijiji chao zimezorota kutokana na kuzolewa kwa daraja hilo.
“Watoto hawaendi shuleni, wamekaa nyumbani wanasubiri mvua ziishe,” anasema.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Mkuranga, Bernard Mwita, amesema daraja lililosombwa na maji lilijengwa kupitia mradi wa Tasaf mwaka 2002, kwa lengo la kuwasaidia wananchi kutokana na kero kubwa waliyokuwa wanaipata. Hata hivyo anakiri kuwa ujenzi wa daraja hilo haukuzingatia mahitaji, kwani lilikuwa na mdomo mmoja tu badala ya miwili iliyotakiwa.
Hata hivyo, hakuwalaumu wajenzi wa daraja hilo akibainisha kuwa limezolewa na maji kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha mvua kubwa kuliko kiwango kilichozoeleka.
“Tumeishaiona hali hii na hivi sasa tumefanya tathmini upya na kubaini kuwa hapa linahitajika daraja kubwa lenye milango miwili, lenye thamani ya Sh milioni 140. Tutaliweka hili kwenye maombi yetu ya fedha na tunaamini litaweza kukidhi mahitaji ya eneo hilo,” anasema.
Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Athumani Manicho, anasema shida zinazotokana na daraja hilo zimekuwepo kwa muda mrefu.
“Hili daraja ni muhimu sana kwa sababu linahudumia vijiji vya Mipeko, Mbande, Tambani na Kitongoji cha Mlamuleni. Baada ya kuvunjika ina maana hakuna mawasiliano kati ya vijiji hivi vyote,” anabainisha.
 
Mwisho

901 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!